****************************
JUMLA ya walengwa 207,391 wamepatiwa chanjo kwa hiari iliyoanza kutolewa hivi karibuni katika vituo vya kutolea huduma zaidi ya 550 kwa Tanzania bara.
Katika taarifa kwa Umma leo 15 Agosti, juu ya maendeleo ya utoaji wa chanjo ya UVIKO 19 kwa Wanananchi, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kupitia kwa Katibu Mkuu (Afya), Prof. Abel Makubi amebainisha kuwa:
Tathimini ya zoezi la utoaji chanjo tangu Mikoa yote izindue tarehe 04/08/2021, inaonesha mpaka kufikia tarehe 14.08.2021, jumla ya walengwa 207,391 wamepatiwa chanjo hiyo kwa hiari.
Ambapo amebainisha kuwa, kati ya hao waliopatiwa chanjo hiyo, walengwa 121,002 ni wanaume ambao ni asilimia 58 (58.3%) na Wanawake ni 86,389 sawa na asilimia 41 (41.7%).
“Natoa maelekezo kwa watoa huduma wote, kutumia dakika chache kutoa elimu ya umuhimu wa chanjo kwa kila mteja atakaye mhudumiwa kwa magonjwa mengine ili kumpa nafasi ya uelewa na baadae yeye kuchukua maamuzi sahihi juu ya chanjo katika vituo vyote na Hospitali.
“Aidha pasiwepo na sababu yoyote ya Wananchi waliofika vituoni kukosa au kukataliwa kupata huduma ya chanjo” alibainisha kwenye taarifa yake hiyo kwa Umma.
Aidha, aliongeza kuwa, Serikali inaendelea kuratibu utoaji wa chanjo ya UVIKO-19 (COVID-19) kupitia vituo vya kutolea huduma za Afya vya umma na binafsi vilivyoidhinishwa hapa nchini.
Hadi kufikia tarehe 14.08.2021 jumla ya dozi 1,008,400 za chanjo ya UVIKO-19 zilikuwa zimesambazwa katika mikoa yote 26 na chanjo imekuwa ikitolewa katika vituo vya kutolea huduma zaidi ya 550 kwa Tanzania bara.
Katika taarifa hiyo pia amepongeza mamlaka za Mikoa, Wilaya na Mitaa kwa kuhamasisha zoezi la chanjo, ambapo ameomba pawepo pia na juhudi zaidi za kuongeza kasi katika maeneo ya pembezoni ya miji, mitaa na vijijni.
“Aidha nawaasa Wananchi waendelee kuchukua tahadhari zote za kinga dhidi ya UVIKO-19 kwa kunawa mikono na maji tiririka/kutumia vipukusi, kuvaa barakoa katika maeneo hatarishi, kuepuka misongamano isiyokuwa ya lazima na kufanya mazoezi kila mara”. Alimalizia Prof. Makubi katika taarifa yake.