Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akizungumza na wananchi wa kijiji cha Ndundutawa wilayani Rufiji wakati wa ziara yake ya kikazi yenye lengo la kuhimiza amani na uwajibikaji.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akijibu hoja zilizowasilishwa na wananchi wa kijiji cha Ndundutawa wilayani Rufiji wakati wa ziara yake ya kikazi yenye lengo la kuhimiza amani na uwajibikaji.
Mwananchi wa Kijiji cha Ndundutawa wilayani Rufiji Bibi. Asha Rumbongo akiwasilisha changamoto kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa (hayupo pichani) wakati wa ziara ya kikazi ya waziri huyo wilayani humo yenye lengo la kuhimiza amani na uwajibikaji.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akizungumza na wananchi wa kijiji cha Chumbi wilayani Rufiji wakati wa ziara yake ya kikazi yenye lengo la kuhimiza amani na uwajibikaji.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akipokea mfano wa hundi ya shilingi Milioni 83 toka kwa Mwakilishi wa Songas, Meneja Miradi ya Kijamii Bw. Nicodemus Chipakapaka kwa ajili ya ujenzi wa madarasa ya Shule ya Msingi Shela na Kiwanga Wilayani Rufiji.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akikabidhi mchango wa bando za bati kwa viongozi wa CCM kata ya Chumbi kwa ajili ya kuezeka jengo jipya la ofisi hiyo mara baada ya kuweka jiwe la msingi.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akikata utepe kuzindua jengo la Wodi ya Wazazi kijiji cha Chumbi wilayani Rufiji wakati wa ziara yake ya kikazi yenye lengo la kuhimiza amani na uwajibikaji.
………………………………………………………………………..
Na. Mwandishi Wetu-Rufiji
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema, huu ni wakati ambao Watanzania wanapaswa kuitunza na kuilinda amani iliyopo ili kuiwezesha Serikali ya Awamu ya Sita kutekeleza azma yake ya kuleta maendeleo kwa wananchi katika sekta ya Afya, Elimu, Miundombinu, Kilimo, Biashara na Utumishi wa Umma.
Waziri Mchengerwa ametoa rai hiyo kwa watanzania kwa nyakati tofauti wakati akizungumza na wananchi wa vijiji vya Ndundutawa, Chumbi na Shela wilayani Rufiji kwa lengo la kuhimiza amani na uwajibikaji ili kuweka mazingira rafiki ya upatikanaji wa maendeleo ya taifa.
Waziri Mchengerwa amesema, Serikali inayoongozwa na Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan ipo pamoja na Watanzania wote bila kujali tofauti na itikadi walizonazo, hivyo imejipanga vizuri kuleta maendeleo katika maeneo yote nchini kwenye sekta mbalimbali.
“Serikali imedhamiria kuleta maendeleo kwenye kata zote nchini, akitoa mfano wa azma ya Serikali kujenga vituo vya afya na kutoa vifaa tiba katika maeneo yote ambayo yanakabiliwa na changamoto hizo”, Mhe. Mchengerwa amefafanua.
Ili kuunga mkono azma hiyo ya Serikali, amewataka wananchi popote walipo kwa nafasi walizonazo kufanya kazi kwa bidii kwa lengo la kuunga mkono Kaulimbiu ya Mhe. Rais ya KAZI IENDELEE ili taifa lipate maendeleo ya kiuchumi.
Kuhusiana na hoja ya wananchi wa Kijiji cha Ndundutawa kuhusu utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini, Mhe. Mchengerwa ametoa maelekezo kwa watendaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kurejea katika kijiji hicho ili kufanya upya tathmini ya kujiridhisha kama kaya zote masikini zenye sifa ya kunufaika na mpango huo zimeandikishwa ili kupata ruzuku.
Katika kuhakikisha wananchi hao wananufaika na Mpango huo, Mhe. Mchengerwa amemtaka Mkuu wa Wilaya ya Rufiji Mhe. Meja Edward Gowelle kuhakikisha anawahimiza watendaji wa TASAF walio katika wilaya yake kuhakikisha tathmini inafanywa upya kwenye Kijiji hicho.
Mhe. Mchengerwa amesisitiza kuwa, dhamira ya Serikali kuwa na Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini ni kuziwezesha kaya zote masikini nchini kuwa na uwezo wa kujitegemea kiuchumi.
Akijibu hoja ya baadhi ya Watumishi wa Umma kutokuwa waadilifu, Mhe. Mchengerwa amesema ofisi yake itafanyia kazi changamoto hiyo ili taifa liwe na watumishi waadilifu ambao wanatekeleza majukumu yao kwa kuzingatia Kanuni za Maadili ya Utendaji katika Utumishi wa Umma za mwaka 2005.
“Kama kuna mtumishi anashiriki vitendo vya rushwa, ubadhilifu wa mali za umma, mzembe na anayekwamisha utendaji kazi wa Serikali ofisi yangu itahakikisha anachukuliwa hatua za kinidhamu”, Mhe. Mchengerwa amesisitiza.
Akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Chumbi mara baada ya kuzindua Jengo la Wodi ya Wazazi lililopo katika kijiji hicho, Mhe. Mchengerwa amesema ofisi yake itamsaidia Mheshimiwa Rais kuhakikisha kunakuwa na matumizi mazuri ya fedha inayotolewa na Serikali na kuelekezwa kwenye miradi ya maendeleo kwenye ngazi ya Taifa, Mkoa, Wilaya na Kijiji.
Ili kuhakikisha kuna matumizi mazuri ya fedha za miradi ya maendeleo, Mhe. Mchengerwa ameilekeza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kuhakikisha inafanya ufuatiliaji wa matumizi ya fedha kila mahali zilikopelekwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo, kwa lengo la kujiridhisha na kuzingatia thamani ya fedha iliyotolewa.
Sanjari na hilo, Mhe. Mchengerwa hakusita kuwahimiza Watendaji wa Serikali na Chama Tawala kutatua changamoto zinazowakabili wananchi ikiwa ni pamoja na kuchapa kazi ili kutoa mchango katika maendeleo ya wananchi na taifa kwa ujumla.
Ameongeza kuwa, kila Wilaya, Kijiji au Kitongoji anakopita wananchi wanadai maendeleo, hivyo Serikali imejikita katika kuwaletea maendeleo na ndio maana ameilekeza TAKUKURU kufanya ufuatiliaji wa matumizi ya fedha zinazotolewa na Serikali kwenye miradi ya maendeleo.
Mhe. Mchengerwa amesema, kasi ya Serikali katika kutatua kero zinazoikabili sekta ya umma, afya, elimu, miundombinu, uchumi na nyinginezo, itawezesha Serikali iyopo madarakani kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya Mwaka 2020-2025.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa amehimiza Watanzania kuitunza na kuilinda amani ya taifa iliyopo ili kutoa fursa kwa Serikali kusimamia utekelezaji wa Ilani ya CCM ya Mwaka 2020-2025 ambayo imelenga kuwaletea Watanzania maendeleo.