Wakuu wa Idara na vitengo wakiwa katika picha ya pamoja na Wakurugenzi na Mwenyekiti wa Halmashauri baada ya sherehe hiyo ya makabidhiano.
Na Alinikyisa Humbo, Manyoni
ALIYEKUWA Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni Charles Fussi amemkabidhi ofisi Mkurugenzi Mtendaji mpya wa Halmashauri hiyo Melkzedeck Humbe katika hafla ya makabidhiano iliyofanyika jana wilayani humo.
Akizungumza baada ya kukabidhiwa ofisi Mkurugenzi Mtendaji mpya wa Halmashauri hiyo Melkzedeck Humbe alisema anategemea ushirikiano mkubwa kutoka kwa viongozi wa Halmashauri hiyo, wakuu wa idara na watumishi wote.
Humbe alisema kwamba bila ushirikiano hakuna kitakachoweza kufanyika ambapo alitumia nafasi hiyo kumpongeza aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Charles Fussi kwa kazi kubwa aliyoifanya kwa kipindi chote alichoweza kuhudumu hasa katika usimamimizi wa shughuli zote za maendeleo na ubunifu wa mradi wa kilimo cha korosho.
“Sijaja hapa kuanzisha kazi bali nimekuja kuendeleza kazi iliyoachwa na mtangulizi wangu Fussi na kwamba kama ambavyo kauli ya Rais Samia Suluhu isemavyo kwamba kazi iendelee basi ndivyo ninavyotamani Manyoni iendelee kazi alizokuwa akiifanya mwenzangu ziendelee”. alisema Humbe.
Alisema amefika Manyoni kuendeleza yale yote ambayo Fussi aliweza kuyaibua ikiwa ni utekelezaji wa ilani na si vinginevyo.
Kwa upande wake Fussi amewashukuru watumishi wote na kuahidi kwamba ataendelea kutoa ushirikiano pale watakapoona inafaa ili kuleta tija ya maendeleo kwa wananchi wa Wilaya ya Manyoni.
Aidha Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni, Jumanne Mlagaza alitoa shukrani kwa Fussi kwa kipindi chote walichoweza kufanya kazi pamoja na kuwa anaamini Mkurugenzi aliyekabidhiwa ofisi ataendeleza ushirikiano wa utendaji kazi kati ya Ofisi ya Mkurugenzi na ofisi yake.
Makabidhiano hayo yamehudhuriwa na Wakuu wa Idara na Vitengo vyoe na,Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni na baada ya makabidhiano ya ofisini ya nyaraka basi waliweza pia kutembelea mradi mama wa kilimo cha korosho katika maeneo yote yalipo mashamba hayo wilayani humo.