Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Khamis Hamza Chilo akiongoza Kikao kilichohusisha watumishi wa Kikosi cha Jeshi la Polisi cha Kupambana na Dawa za Kulevya (hawapo pichani), kilichofanyika leo, Makao Makuu ya jeshi hilo Ziwani, Visiwani Zanzibar.Kulia ni Mkuu wa Kitengo cha Rasilimali Watu, Naibu Kamishna wa Jeshi la Polisi, Frasser Kashai.Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Khamis Hamza Chilo (kushoto meza kuu), akiongoza Kikao kilichohusisha watumishi wa Kikosi cha Jeshi la Polisi cha Kupambana na Dawa za Kulevya kilichofanyika leo, Makao Makuu ya jeshi hilo Ziwani, Visiwani Zanzibar.Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, Saleh Mohamed Saleh akizungumza wakati wa Kikao kilichohusisha watumishi wa Kikosi cha Jeshi la Polisi cha Kupambana na Dawa za Kulevya kilichofanyika leo, Makao Makuu ya jeshi hilo Ziwani,Visiwani Zanzibar.Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
****************************
Na Abubakari Akida,MOHA
Jumla ya Kesi 678 za Dawa za Kulevya zimekamatwa na Jeshi la Polisi kupitia Kikosi cha Kupambana na Dawa za Kulevya katika kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2018 mpaka Agosti mwaka 2021 huku jamii ikiaswa kutambua dawa za kulevya ni uhalifu kama uhalifu mwingine ili jeshi liweze kupata ushirikiano.
Takwimu hizo zimetolewa na Mkuu wa Kikosi cha Kupambana na Dawa za Kulevya Zanzibar, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Omar Khamis akisoma Taarifa za Kesi za Dawa za Kulevya kwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Khamis Hamza Chilo wakati wa kikao mkakati cha kupambana na Dawa za Kulevya kilichofanyika leo Agosti 15, Makao Makuu ya Jeshi la Polisi,Ziwani Zanzibar.
“Mheshimiwa kitengo kimefanikiwa katika ukamataji wa kesi ambapo mwaka 2017 jumla ya kesi 213 zilikamatwa,mwaka 2018 kesi 183,mwaka 2019 kesi 131,mwaka 2020 kesi 93 na hadi kufikia mwezi Agosti mwaka huu kesi 58 zilikamatwa katika maeneo mbalimbali ya Zanzibar ambapo tayari washtakiwa tayari washaanza kushughulikiwa kwa mujibu wa sheria namba 9 ya mwaka 2009 ya kudhibiti dawa za kulevya” alisema ACP Omar
“……lakini pia kumekua na muendelezo mzuri wa kesi hizo kwani kesi 188 zipo mahakamani,kesi 28 zipo kwa Mkurugenzi wa Mashtaka,kesi 190 tayari zina hati ya mashtaka huku washtakiwa wanatafutwa kufikishwa mahakamani,hapo utaona karibu asilimia 80 ya kesi zilizokamatwa zimekamilisha upelelezi” aliongeza ACP Omar
Akizungumza katika kikao hicho,Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,Khamis Hamza Chilo aliwataka watumishi wa kikosi hicho kuongeza kasi ya Misako na doria ili kuweza kukamata watuhumiwa Zaidi.
“Hali ya uhalifu wa dawa za kulevya huko mtaani ni mbaya, vijana wanaaribika,uhalifu unaochochewa na dawa za kulevya ni mkubwa sana, nawaombeni mzidishe misako,doria ili kunusuru nguvu kazi ya taifa hili,viongozi wetu wanawategemea vijana katika kukuza uchumi wa nchi hii, shirikianeni na jamii pelekeni elimu kwenye jamii kwani jamii inachukulia dawa za kulevya kama sio uhalifu tofauti na aina nyingine za uhalifu” alisema Naibu Waziri Chilo
Kwa kipindi cha mwezi januari hadi sasa Jeshi la Polisi limefanya operesheni mbalimbali za kupambana na uhalifu ikiwemo ukamataji wa dawa za kulevya huku heroine zenye uzito wa kilogramu 1 na gramu 287.51 zikishikiliwa na bangi kilogramu 120 na gramu 651.984 zikishikiliwa.