***********************************
Na. Damian Kunambi, Njombe
Waziri wa ujenzi na uchukuzi Mahandisi Godfrey Kasekenya amesema serikali itahakikisha inakamilisha ujenzi wa barabara ya kutoka Lupingu wilayani Ludewa mkoani Njombe mpaka wilaya ya Kyela mkoani Mbeya ili kuweza kupunguza adha ya usafiri wa majini wanayokumbana nayo wananchi wa ukanda wa mwambao.
Hayo ameyasema akiwa kwenye ziara wilayani Ludewa ambapo aliwasili katika eneo la bandari ya Nsungu iliyopo katika kata ya Manda akiwa sambamba na mwenyeji wake mbunge wa jimbo la Ludewa Joseph Kamonga pamoja na baadhi ya viongozi serikali ngazi ya wilaya ambapo baadhi ya wananchi wanaotumia usafiri wa majini walitoa changamoto zinazowakabili kutokana na usafiri huo.
Andrea Haule ni miongoni mwa wananchi hao ambapo amedai kuwa wamekuwa wakipata shida katika kufanya safari zao kwenda mkoani Mbeya kwani walikuwa wanategemea usafiri wa meli ya MV Mbeya ambayo kwa sasa imesimamisha shughuli zake kwa takribani miezi mitatu na kupelekea wananchi hao kutumia usafiri wa boti.
Amesema changamoto wanazokumbana nazo katika usafiri huo wa boti ni nyingi hivyo wanaiomba serikali kuwarudishia usafiri wa meli ili wawezi kusafiri kwa urahisi zaidi.
” Serikali tuomba mtusaidie kuturudishia usafiri wa meli kwani hizi boti tunazozitumia ni hatari kwa maisha yetu maana iko wazi na tunasafiri kwa umbali mrefu pamoja na mizigo”, alisema Haule.
Kwa upande wa naibu waziri huyo ameziomba mamlaka husika kutatua changamoto hizo sambamba na kuahidi kushughulikia ujenzi wa barabara inayopita pembezoni mwa ziwa ili iweze kuwa mbadala pindi wanapopatwa na changamoto za namna hiyo.
Amesema barabara hiyo itakapokamilika itasaidia sana kutatua tatizo la usafiri kwa wakazi wa pembezoni mwa ziwa kwani watakuwa na uchaguzi wa usafiri kati ya maji na barabara.
“Suala la usafiri ni jambo muhimu kwa jamii na serikali ya rais wetu mama Samia Suluhu Hassan inawajali wananchi wake hivyo natumai tatizo hili litapatiwa ufumbuzi”, Alisema Mhandisi Kasekenya.
Aidha kwa upande wa mbunge wa jimbo hilo Joseph Kamonga amesema usafiri huo unategemewa na kata zaidi ya nane hivyo kukwama kwa meli hiyo kunawaathiri sana wananchi wake.
Amesema wananchi hao wanatumia usafi huo wa majini kwa kusafiri kwenda Kyela na Mbambabey kwaaji ya kununua bidhaa mbalimbali ambazo katika maeneo hayo hazipatikani kwa urahisi ukilinganisha na maeneo mengine.
“Hawa wananchi kwa asilimia kubwa usafiri huu wa meli ulikuwa na msaada sana kwao kwani wako mbali na huduma nyingi za msingi hivyo kukwama kwa meli hii kumesababisha maumivu makubwa sana kwa wakazi wa ukanda huu wa ziwani”, Alisema Kamonga.
Josaya Luoga ni katibu siasa na uenezi wa wilaya ya Ludewa amesema wanaimani kubwa na mwenyekiti wa chama cha mapindiuzi (CCM) taifa rais Samia Suluh Hassan pamoja na wateule wake ambao wamekuwa wakiwafikia wananchi kusikiliza na kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili.
Amesema viongozi wa ngazi za juu wanapowatembelea ni dhahiri kwamba wanatekeleza vyema ila ya CCM kitu ambacho kinawapa nguvu ya kuwafanya wananchi wazidi kujenga imani ya chama chao sambamba na kuendelea kutuwezesha kuendelea kuongoza.