Home Mchanganyiko MDEKHA AOMBA USHIRIKIANO TAHLISO

MDEKHA AOMBA USHIRIKIANO TAHLISO

0

RAIS wa Serikali ya Wanafunzi katika Chuo cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST) Aman Mdekha, ameteuliwa kuwa Kamishina wa Habari, mahusiano na Mawasiliano wa Jumuiya ya Wanafunzi Taasisi ya Elimu ya Juu Tanzania ( TAHLISO) na kuahidi kutoa ushirikiano wa dhati ili kufanikisha malengo ya jumuiya hiyo.

Akizungumza muda mfupi mara baada ya uteuzi huo, Mdekha alisema ameupokea kwa mikono miwili uteuzi huo na kuongeza kuwa kilichopo mbele yake kwa sasa ni kuongeza uwajibikaji ili kuwatumikia wanafunzi wote waliopo ndani ya mwamvuli wa jumuiya hiyo.

“Namshukuru Mwenyekiti wa TAHLISO Frank Nkinda kwa kuweka imani kwangu, naahidi kufanya kazi kwa bidii na kujituma katika majukumu yangu ya kuwatumikia wanafunzi wenzangu” alisema Mdekha

Kauli hiyo ya Mdekha imekuja kufutia mabadiliko ya baadhi ya nafasi za utendaji yaliyofanywa na Rais wa Jumuiya hiyo kwa lengo la kuboresha utendaji wa Tahliso ambapo mbali na Mdekha pia amemteua Rais wa Serikali ya wanafunzi kutoka chuo cha Utalii Evidence Mganyizi kuwa Kamishna wa Utalii na utamaduni wa Tahliso.

“Ninaomba ushirikiano kutoka kwa jumuiya nzima ya wanafunzi Tanzania ili tuweze kuwasemea na kutatua changamoto mbalimbali wanazokutana nazo vyuoni na maeneo mengine ya kielimu, lengo ni kuhakikisha wanapata elimu bila vikwazo ” aliongeza Mdekha

Aidha alisisitiza kwa kuwataka wanafunzi wenzake waliopo katika likizo na mafunzo kwa vitendo, kuhakikisha wanatumia vyema muda na nafasi walizopata ili pindi wanaporejea vyuoni wawe wenye weledi wa kutosha na hivyo kuchagiza ukuaji wa maendeleo ya vyuo vyao.