Baadhi ya wabunifu katika tasnia ya habari kanda ya ziwa wakati wa mafunzo pamoja na Meneja wa Jamii Tanzania wa Kituo cha ubunifu tasnia ya habari cha chuo kikuu cha Aga Khan (aliyesimama katikati), Bi. Tully Mwampanga
Picha ya pamoja na baadhi ya wabunifu katika tasnia ya habari kanda ya ziwa mara baada ya mafunzo
***************************
Kituo cha Ubunifu cha habari cha Chuo Kikuu cha Aga Khan (Aga Khan University Media Innovation Centre) kinacholenga kuwawezesha wabunifu kutoka nchi za Tanzania Kenya na Uganda kwa kuwapa fursa mbalimbali wamefanya mafunzo juu ya ubunifu kwa mtumiaji kwa wabunifu katika tasnia ya habari kanda ya ziwa. Mafunzo hayo yamefanyika kufuatia mwito kwa wabunifu wote Afrika Mashariki kutuma maombi au andiko la kiubunifu katika tasnia ya habari ili kuweza kujipatia mafunzo, ushauri wa kitaalamu kwa mwaka mzima, kupata ruzuku ya dola za kimarekani 20,000 ambazo ni takribani Million 50 za kitanzania vilevile mtandao-watu na eneo la kufanyia kazi kwa ajili ya kuendeleza ubunifu wao.
Mwito huu au shindano hili ni kupitia programu ya kituo hiko cha ubunifu katika tasnia ya habari ifahamikayo kwa jina la ‘Innovators-In-Residence’ ambapo sasa ni awamu ya 3 kwa kituo hiki cha ubunifu kupokea maombi tangu kuanzishwa kwake mwaka 2019, ambapo makao makuu yakiwa nchini Kenya. Kituo hiki cha ubunifu cha chuo kikuu cha Aga Khan kinatekeleza miradi yake kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo Deustche Welle Akademie. Na kwa kiupekee kabisa, awamu hii kituo hiki kitachukua mawazo au timu 9 za wabunifu ambapo mawazo/wabunifu wanne kutoka Tanzania, na wane wengine kutoka Uganda na timu moja kutoka nchini Kenya.
Mafunzo hayo yamefanyika kwa mfululizo wa siku 3 kwa wabunifu takribani 25 kutoka mikoa mbalimbali ya Kanda ya ziwa ikiwemo Mwanza, Mara, Geita ili kuwajengea uwezo wa kiubunifu na ambapo mara baada ya kukamilika kwa mafunzo, watatuma pia maombi katika shindano hilo. ‘Kwa hizi siku tatu, nimefurahi sana kwani nimeweza kuongeza ujuzi katika bunifu yangu na kupanua mawazo zaidi, pia imekuwa faraja kukutana na wabunifu wenzangu. Tunaomba Kituo cha Ubunifu katika habari kuendelea kutoka fursa hizi tuzidi kunufaika’ – Kalphonce Mayala, mbunifu kutoka wilaya ya Kwimba, Mwanza.
Mafunzo hayo yaliyolenga kuboresha bunifu zao yamefanyika kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa ubunifu na habari wakiwemo Ennovate Hub. Mbali na hivyo Kituo kinashirikiana na wadau wengine kutoka Tanzania, Kenya, Uganda na nchi zingine nyingi ili kuwawezesha Zaidi wabunifu katika sekta ya habari.
Akizungumza na vyombo vya habari, Meneja Jamii – Tanzania wa kituo hiko, Bi. Tully Mwampanga awatia moyo na kuwasisitiza Zaidi wabunifu nchini Tanzania kutoka mijini na vijijini katika tasnia ya habari hiyo kutuma maombi kwa wingi ili kunufaika. Waweza kusoma maelezo hapa kabla ya tarehe 31 Agosti 2021 au kutemebela tovuti yetu (www.mediainnovationnetwork.org ) kupata maelezo zaidi.