Afisa masoko wa GS1 Tanzania katika kituo cha uwezeshaji Kahama,Shaban Mikongoti akitoa elimu ya Barcode kwa wajasiriamali.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Mh.Jenista Mhagama akiwa na Katibu Mtendaji wa Baraza la Uwezeshaji Bibi Beng’I Issa wakisikiliza maelezo kutoka kwa mnufaika wa program za Uwezeshaji.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu akizindua kituo cha Uwezeshaji cha Kahama.
Katibu Mtendaji wa Baraza la Uwezeshaji, Bibi Bengi Issa akisikiliza maelezo kutoka kwa wanufauika wa program za Serikali za Uwezeshaji.
*************************************
Na Jozaka Bukuku
NOVEMBA 18, 2018 Mheshimiwa Jenista Mhagama,Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu alizindua rasmi Kituo cha Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi kilichopo Kahama katika kata ya Nyihogo mkoani Shinyanga.
Katika ziara hiyo aliambatana na Katibu Mtendaji wa Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) Bibi Beng’i Issa.Baraza ndio wenye dhamana ya kusimamia kituo hicho ikiwa ni pamoja na kuratibu shughuli zote za uwezeshaji Kitaifa.
Kituo hicho ni matokeo ya utekelezaji wa agizo la Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kasimu M. Majaliwa (Mb), ambaye alifanya ziara mkoani Shinyanga na baadae kwenye wilaya ya Kahama.
Akiwa Kahama alitambua mchango wa uongozi wa Serikali ya Mkoa wa Shinyanga hususan Halmashauri ya Mji wa Kahama kwa jitihada za kutenga na kugawa maeneo ya kufanyia shughuli za uzalishaji kwa Wajasiriamali.
Mhe. Waziri Mkuu alitembelea Halmashauri ya Mji wa Kahama na kubaini kuwa katika eneo la Bukondamoyo kumetengwa eneo la ekari 500 kwa ajili ya ujenzi wa viwanda vidogovidogo vya Wajasiriamali hasa vijana na wanawake.
Katika eneo hilo viwanja 623 vimepimwa, kutolewa hati na kugawanywa kwa Wajasiriamali ambapo vinatumika kwa shughuli za uzalishajimali na biashara zingine ikiwemo upasuaji wa mbao, useremala, uzalishaji, uchomeleaje wa mageti n.k.
Baada ya Mheshimiwa Waziri Mkuu kuona jitihada zilizofanyika wilayani Kahama, alitoa agizo kwa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) lianzishe Kituo Maalum cha kuhudumia wananchi kwenye masuala yote ya kiuchumi wakiwemo wajasiriamali, wakulima n.k.
Kituo cha Kahama kimekuwa cha mfano kwa Halmashauri zote nchini kutekeleza agizo la Ilani ya uchaguzi ya CCM mwaka 2020 juu ya uwezeshaji wananchi kiuchumi kupitia vituo vya Uwezeshaji.
Kituo hicho kimekuwa jawabu la kuondoa adha ya Wananchi katika kutafuta taarifa sahihi za biashara,ujuzi wa mambo ya kiuchumi, taratibu za urasimishaji wa biashara, taarifa za masoko, kuongeza thamani ya mazao, kufahamu fursa za hifadhi ya jamii, kupata elimu ya kodi na kufahamu fursa za mitaji.
Kituo kimekuwa nyenzo muhimu inayosaidia baadhi ya Taasisi za Serikali ambazo zinatoa huduma mbalimbali kupata urahisi wa kuwafikia wananchi.
Walengwa wa kituo ni wananchi wote na wajasiriamali wakiwemo wadogo, wakati na wakubwa, Vikundi na Makampuni yaliyopo katika Sekta zote za kiuchumi.
Kituo cha Kahama ni tofauti na vituo vingine ambavyo vimewahi kuanzishwa, kwa sababu lengo lake kubwa ni kumuendeleza mwananchi kiuchumi kwa kuleta huduma zote za Serikali na Sekta binafsi katika eneo moja.
Miongoni mwa Taasisi ambazo zinapatikana ndani ya Kituo ni pamoja na NEEC, SIDO, GS1 Tanzania, VETA, TRA, Benki ya NBC, VICOBA FETA, Pass Trust, Mfuko wa Pembejeo wa AGITF, Tantrade, SELF MF, NSSF, Open University na MKURABITA.
Huduma zinazopatikana kituoni ni pamoja na Urasimishaji wa biashara,Hudma za Kibenki,Elimu ya kodi,Elimu ya kuongeza thamani bidhaa,Huduma za mikopo ya masharti nafuu,Bima ya afya,Huduma za Mifuko ya hifadhi ya jamii,Elimu ya ufundi,Elimu ya vyama vya ushirika, Elimu ya uanzishwaji wa vikundi vya kijamii n.k.
Akizungumza juu ya kituo hicho, Katibu Mtendaji wa Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC), Bibi Beng’i Issa amewataka wajasiriamali kutumia fursa za uwezeshaji ambazo zinapatikana kwenye kituo hicho.
“Serikali ina dhamira njema ya kuanzisha kituo hiki hivyo ni vema wajasiriamali na wafanyabiashara wakatumia fursa zinazopatikana ili kujiendeleza na kukuza mitaji yao, ”alisema Katibu Mtendaji.
“Adha iliyokuwepo zamani hivi sasa haipo ambapo ndani ya kituo mwananchi anapata huduma zote kwa wakati mmoja kwani zipo Taasisi za kifedha,Taasisi zinazotoa elimu ya biashara,Taasisi za urasimishaji wa biashara hivyo ninawaomba wananchi wasiache kutumia fursa hii”aliongeza.