……………………………………………………………….
Na.Alex Sonna,Dodoma
MASHIRIKA zaidi ya 1500 yasiyo ya kiserikali yanatarajiwa kushiriki katika maonyesho ya wiki ya Azaki itakayofanyika Oktoba mwaka huu jijini Dodoma.
Hayo yamesemwa leo Agosti 12,2021 jijini Dodoma na Mkurugenzi Mtendaji wa shirika lisilo la kiserikali la Haki Rasilimali, Racheal Chagonja, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya wiki ya Azaki kwa mwaka 2021.
Amesema, maonyesho hayo tangu yameanza kufanyika nchini mwaka 2018, yamesaidia wananchi kupata uelewa mpana kuhusu kazi zinazofanywa na Azaki mbalimbali nchini.
“Tangu tumeanza kufanya maonyesho haya tumepata mafanikio makubwa sana ikiwemo wananchi kutambua nini Azaki zinafanya nchini lakini mwaka jana kutokana na changamoto ya ugonjwa wa UVIKO 19, hatuweza kuyafanya lakini hali hiyo imetuwezesha kujipanga kwa ajili ya kutathimini mapungufu na kujua kivingine mwaka huu”amesema Chagonja
Amesema wiki ya Azaki mwaka huu itajumuisha pia maonyesho ya shughuli mbalimbali zinazofanywa na mashirika hayo ikiwemo uzalishaji wa bidhaa mbalimbali.
“Kutakuwa na siku mbili ya kuonyesha bidhaa zinazaozalishwa na Asasi mbalimbali maonyesho haya yatafanyika Oktoba 23 na 24 katika viwanja vya Jamuhuri na baada ya hapo tutakuwa na midahalo ya ndani kuhusu mambo mbalimbali”, amesema
Aidha, amesema lengo la wiki hiyo pia itakuwa pia ni kujenga ushirikiano baina ya serikali, wadau,mashirika binafsi pamoja na wanachi katika kushiriki shughuli mbalimbali za maendeleo.
“Tunashukuru hivi sasa wananchi wameweza kutambua umuhimu wa Asasi hizi za kiraia katika kuleta maendeleo kwenye jamii zetu hivyo wiki hii mwaka huu tutaitumia kuendeleza kile ambacho tumekuwa tukikifanya katika miaka iliyopita”amesema Chagonja.
Kadhalika, amesema pia katika wiki hiyo mwaka huu pamoja na mambomengine pia kutakuwepo na huduma za msaada wa kisheria zitakazotolewa kwa wanachi wenye uhitaji na mashirika mbalimbali.
Mkurugenzi Mkazi wa shirika la CBM International Tanzania, Nesia Mahenge amesema katika wiki hiyo watahakikisha kuwa tahadhari zote za kijilinda na maambukizi ya ugonjwa wa UVIKO 19, zinachukuliwa ipasavyo.
“Niwahakikishie washiriki wote pamoja na wananchi kuwa taahadhari dhidi ya maambuzi ya virusi vya ugonjwa wa corona yatachuliwa kwa mujibu wa maelekezo ya wataalamu wetu wa afya,”amesisitiza Mahenge.