Afisa Vipimo Mkoa wa Geita Bw. Festo Robert akitoa elimu ya Vipimo kwa wananchi wa Wilaya ya Chato
Meneja wa Wakala wa Vipimo Bw. Moses Ntungi (mwenye tisheti nyeusi) pamoja na Afisa Vipimo Bw. Festo Robert wakitoa elimu kuhusu matumizi sahihi ya Vipimo katika Maonesho ya Biashara Chato
Meneja wa Wakala wa Vipimo Bw. Moses Ntungi akitoa elimu kuhusu matumizi sahihi ya Vipimo katika Maonesho ya Biashara Chato
Wananchi wa Wilaya ya Chato na maeneo ya Karibu wakipata elimu kuhusu matumizi sahihi ya Vipimo
**************************
Wakala wa Vipimo inawakaribisha Wananchi wote wa Chato pamoja na maeneo ya karibu kutembelea katika banda lake kwenye Maonesho ya kUtalii na Biashara yanayofanyika katika Uwanja wa Magufuli Chato. Lengo kuu la Wakala wa Vipimo kushiriki katika maonesho hayo ni kutoa elimu kwa umma kuhusu matumizi sahihi ya Vipimo kwenye sekta mbalimbali.
Meneja wa Wakala wa Vipimo Bw. Moses Ntungi ameeleza kuwa uwepo wa maonesho haya umesaidia wananchi wa Wilaya ya Chato kujifunza mambo mbalimbali na kazi zinazofanywa na taasisi ya Wakala wa Vipimo ikiwa ni pamoja na kutambua umuhimu wa kutumia vipimo sahihi pamoja na kutambua vipimo vilivyohakikiwa na vile visivyohakikiwa (batili).
Meneja Ntungi ameeleza kuwa Vipimo vyote vilivyohakikiwa na Wakala wa Vipimo huwekewa alama maalumu ambayo ni stika inayosaidia mtumiaji wa kipimo kutambua kwa urahisi kama kipimo anachotumia kipo sahihi na kimehakikiwa.
Kwa upande wake Afisa Vipimo Bw. Festo Robert ameeleza kuwa Wakala wa Vipimo katika Wilaya ya Chato hutekeleza majukumu mbalimbali ili kuwalinda Wananchi. Majukumu hayo ni pamoja na kutoa ushauri wa kitaalamu kuhusu masuala mbalimbali ya Vipimo, kufanya uhakiki wa Vituo vyote vinavyouza mafuta, kufanya uhakiki wa bidhaa zilizofungashwa ili kuhakikisha mnunuzi anapata bidhaa iliyokatika Vipimo sahihi.
Pia, Bw. Festo ameeleza kuwa Wakala wa Vipimo inafanya uhakiki wa mizani zinazotumika kuuzia na kununulia zao la pamba ili kuhakikisha kunakuwa na bishara ya usawa bila kuwa na dhuluma kwa upande wowote. Kadhalika Wakala uhakiki mizani midogo inayotumika kuuzia bidhaa kwenye maduka na masoko. Vilevile Uhakiki wa Vipimo hufanyika katika masoko ya madini pamoja na mizani ya kupimia magari barabarani, na kwenye maghala ya vyama vya msingi vya ushirika.
Kadhalika, Meneja Ntungi alieleza kuwa Ushiriki wa Wakala wa Vipimo Katika maonesho ya Kuhamasisha Biashara na Utalii Wilaya ya Chato ni muendelezo wa kuhakikisha Wananchi katika maeneo mbalimbali wanafikiwa na kupatiwa elimu kuhusu matumizi sahihi ya Vipimo, lakini pia ushiriki wa Wakala wa Vipimo katika maonesho mbalimbali husaidia kusikiliza kero za wananchi kuhusu mambo ya vipimo na kuyatolea ufumbuzi ili kuendelea kuwalinda watumiaji wa vipimo kuweza kupata huduma bora.
Meneja Ntungi ametoa onyo kwa Wafanyabiashara kujiepusha na vitendo vya kuchezea vipimo kwani kufanya hivyo ni kosa na nikinyume na Sheria ya Vipimo Sura na. 340 na mapitio yake ya mwaka 2002. Endapo mfanyabiashara atakamatwa kwa udanganyifu wa Vipimo na kukiri makosa yake atapigwa faini isiyopungua laki moja (100,000/=) na isiyozidi milioni 20 endapo atakataa na kufikishwa mahakamani kwa mkosaji wa kosa la kwanza atatozwa faini isiyopungua laki tatu (300,000/=) na isiyozidi milioni 50 au kifungo kisichozidi miaka miwili (2) au vyote kwa pamoja. Pia, endapo mtuhumiwa atakuwa na makosa ya kujirudia atatozwa faini isiyopungua laki tano (500,000/=) na isiyozidi milioni 100 au kifungo kisichozidi miaka mitano (5) au vyote kwa pamoja.
Wakala wa Vipimo inawasihi wananchi kutoa taarifa endapo watabaini uchezewaji wa vipimo katika maeneo mbalimbali kupitia namba ya bure 0800 110097 au kutembelea ofisi yeyote ya Wakala wa Vipimo zilizopo katika Mikoa yote Tanzania Bara kwa lengo la kupata ushauri wa masuala ya Vipimo au kuwasilisha malalamiko yao kwa lengo la kuboresha utendaji kazi wa Wakala wa Vipimo.