…………………………………………………………………
Adeladius Makwega,WHUSM-Dodoma
“Katika tamaduni nyingi za mwafrika lilikuwa ni jambo la adimu sana kuona mwanamke akipiga ngoma hadharani na kama mwanamke atafanya hivyo jua kuwa jambo hilo lina sababu nzito, si bure, Makwega ntafute kwa wakati wako nikwambie.” Niliambiwa kwa bashasha kubwa na Afisa Utamaduni Mwandamizi wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Bi Lilian Shayo tukiwa tumeketi pamoja katika Tamasha la Cigogo lililofanyika Wilaya ya Chamwino Jijini Dodoma hivi karibuni kwenye Kituo cha Sanaa cha Chamwino.
Udenda ulinitoka kwa tabasamu zito kutoka kwa afisa huyu wa Serikali. Nikavuta kiti na kumsogelea kutokana na kiu ya kujua hilo nalotaka kuambiwa, huku kwa mbele Tamasha la Cigogo likiendelea-inatoka ngoma hii inaingia hii.(Kwa kando Mshereheshaji wa tamasha- anasema sasa inakuja ngoma ya Muheme kutoka Chinangali II Ngoma hii inaitwa Muheme…)
“Ngoma hii inaitwa Muheme kutokana na sababu moja kubwa inatengenezwa kwa mti wa Muheme ambao ni mti laini sana, unachongeka kwa urahisi sana na mti huu unastawi katika maeneo makame, unauwezo wa kuyavuta maji kutoka mbali ardhini na ndiyo maana unapatikana sana hapa Dodoma.”Aliendelea kusema Mshereheshaji wa Siku hiyo.
Nikapata mshereheshaji binafsi, Lilian Shayo akaendelea kunisimulia “Ngoma ya mti wa Muheme ni nyepesi kuweza kushikwa kwa mkono mmoja na hata kuweza kupachikwa kiurahisi katikati ya mapaja wakati wa kupiga ngoma hili isimchoshe mpigaji na mchezaji wa ngoma hiyo.”
Ngoma hizo huwa zipo za aina mibili kubwa na zile ndogo ambazo zinatafautiana milio kuna ule mlio wa juu na mlio wa chini.
Nilijiuliza swali mbona washiriki wake wengi ni wanawake? Nilipata jibu kutoka kwa Afisa Utamaduni huyu kuwa hii ni ngoma ya kipekee mno japokuwa yapo makabila mengine nje ya Tanzania yenye ngoma kama hii ambazo zinatumika wakati wa tohara ya wanawake na unyago. Ikifanana na ngoma za Venda ya huko Afrika ya Kusini na Keyio na huko Kenya.“Ni kweli ngoma hii inachezwa kipindi cha tohara ya wanawake na kuna madai kuwa ina asili ya Wanyamwezi.” Hoja hii inamuibua Dkt. Kedmon Mapana ambaye alikuwepo katika tamasha hili.
“Katekista Isaya Msulwa wa Kanisa la Anglikani ambaye aliniambia kuwa Ngoma ya Muheme kwa kigogo inafahamika kama makumbi ga wadala-ngoma ya wanawake.”Aliniambia Dkt Mapana
Hoja ya Katekista Isaya Msulya iliibua maswali mengi je Wanyamwezi wa Tabora walikuwa wakifanya biashara gani na Wagogo? Jibu la Isaya Msulwa lilikuwa hafahamu jambo ambalo liliwaleta Wanyamwezi Dodoma na kuwahusisha na ngoma hii.
Je mti wa Muheme uliwahusisha vipi Wanyamwezi? Lakini pia Dkt Mapana aliibua hoja nyingine Je kabila la Wanyamwezi lilikuwa linawakeketa mabinti zao? Majibu ni mepesi mti wa Muheme unapatikana kwa wingi Dodoma na pia Wanyamwezi hawakuwa na desturi ya kukeketa binti zao.
“Sisi wenyewe tuliikuta na ilikuwa ikitumika tangu enzi za mababu na mabibi na ilikuwa ikitumika mno katika unyago, kina mama ndiyo walioshiriki ndiyo maana ikaitwa Makumbi ga wadala.” Aliongeza Dkt Mapana.
Elizaberth Masholi ambaye alikuwa na umri wa miaka 72 mwaka 1889 ambaye alinukuliwa na wamishionari waliokuja Tangayika kueneza ukristo alisema kuwa Wagogo walianza ukeketaji muda mrefu sana na hata majirani zao Wakaguru japokuwa walikuwa hawakeketi lakini mabinti wa Kikaguru waliotamani kukeketwa walifanya hivyo na Chifu wao hakuwakataza.
Darasa la leo lilikuwa la mwanafunzi mmoja na walimu wangu wawili yaani Afisa Utamaduni Mwandamizi Bi Shayo na Dkt Mapana, jambo kama hili huwa ni la nadra mno lakini Tamasha la Cigogo likanipa fursa hiyo.
Dkt Mapana aliniambia kuwa ngoma ya Muheme iligawanyika mara tatu kuna ya kabla ya tohara, ile ya wakati wa tohara na ya baada ya tohara.
“Muheme ya kabla ya tohara ilikuwa ikifahamika kama Mphongwa hii ilikuwa ikiwajumuisha akinamama kadhaa watatu wakiwa na ngoma kubwa na watatu wakiwa na ngoma ndogo na akinamama hawa huwa wamesimama kama nusu duara, huku wakipiga ngoma hizo kwa mbele akinamama wawili wakitazamana mmoja akiwa amekaa akinyoosha miguu akisugua kitu kama msala mdogo kwa kutumia kijiko cha mbao amabacho na mwingine akiwa amechuchumaa nayeye akisugua msala huo. Huku msala huo unaposuguliwa ukitoa mlio ulikuwa unachanganywa na ngoma basi ngoma Mphongwa inasikika. Hapa sasa ni wakati majumbani wanawatayarisha mabinti kwa tohara. Ikiaminika kuwa ngoma hiyo inachezwa juma moja kabla ya tukio hilo la ukeketaji kufanyika.” Aliniambia Dkt Mapana.
“Muheme ya wakati wa tohara ilipangwa vilivyo kwani katika kila kona ya tukio hilo linapofanyika walikuwepo akinamama hawa na ngoma zao. Ngoma hii siku hiyo ilikuwa ikipigwa kwa sauti kubwa ili kuwazuia wanaume wale wanaoweza kupita katika eneo hilo iwe kwa bahati mbaya au la wasisikie kabisa kelele za mabinti waliokuwa wakifanyiwa tohara. Lakin waliwazuia mabinti ambao hawajafanyiwa tohara kujua kile kinachoendelea na wakati huo ngoma hiyo iliyoambatana na sauti za juu ilisaidia kuwatia moyo na kuwapunguzia uchungu mabinti waliokuwa wakifanyiwa tohara.” Bi Shayo aliongezea.
Na Muheme ya mwisho ni ile inayochezwa baada ya tohara ambapo ngoma zinapigwa vizuri lakini ngoma kubwa zinachezwa zikiwa zimekamatwa na mapaja ya mpigaji wa ngoma ndogo zikipigwa zikiwa zimeshikwa mkononi. Wapigaji wa ngoma hii wanaweza kuingia kwa pamoja au kuingia kati mmoja mmoja kuonesha ujuzi wao.
“Tulianza kucheza ngoma za Muheme za Kisasa miaka 1960. Tulicheza wakati wa kuwakaribisha wageni wa kisiasa, kwenye mikutano ya hadhara na wakati mwingine tulicheza mbele ya wageni rasmi.” Hii ndiyo Muheme ya kisasa, anasema Bibi Elizabeth Mwimbwa mkaazi wa Mtumba.
Hapa ndipo wanaume waliweza kuingia na kucheza ngoma hii na jukumu lao likawa kucheza Kayamba tu.
“Ngoma hii, ikaanza kuchezwa kanisani, baada ya serikali ya kikiloni kukataza ukeketaji, uchezaji wa ngoma hii ulikosa mahali pa kuchezewa mara kwa mara, na watu wengi waliokuwa wakicheza ngoma hii walihamia kanisani, na kanisa lilikuwa limeruhusu watu kutumia utamaduni wao, hivyo ngoma hii ilienea kanisani kirahisi. Hasa wakati wa Askofu Stanway wa dayosisi Kati ya Tanganyika ambaye alikuwa askofu wa tatu mzungu wa Kanisa la Anglikana dayosisi hiyo.” Alibainisha Dkt Mapana.
“Kumekuwa na dhana kubwa ya ngoma ya muheme kuwa pale mchezaji mwanamama anapocheza na yupo kwenye hedhi na mambo kama yameharibika basi mchezaji ngoma anaweza kuiweka kwenye mapaja vizuri akipiga na akatoka nje ya uwanja kwenda kuyaweka mambo vizuri huko chemba. Hata namna ya kuiweka ngoma hii mapajani kuna tafsiri kubwa sana…! wanawake wanatakiwa kuwashikilia vizuri waume zao katika ndoa.” Aliniambia Bi Shayo.
Niliweka kalamu chini ili nimalizie uhondo wa Tamasha la Cigogo. Ama kweli ukitaka kujua mbuga ipi ina wanyama wakali, tembelea mbuga hiyo.