……………………………………………………………………………….
Na.Elisa Shunda, Morogoro.
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimetoa siku 14 kwa uongozi wa chama hicho kwa mikoa yote nchini kuwasilisha ngazi ya taifa taarifa ya ukaguzi wa miradi inayoendelea katika mikoa yao.
Hayo yamesemwa na Katibu mkuu wa CCM, Daniel Chongolo, mkoani Morogoro, leo katika ziara ya ukaguzi wa ujenzi wa reli ya mwendokasi katika kambi ya SGR wilayani Kilosa.
“Uwepo wangu na sekretarieti ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa katika ukaguzi wa reli hii ya mwendokasi ikawe salamu kwa uongozi wa mikoa, wilaya,kata na matawi yote nchini kufanya ukaguzi na kuleta taarifa ya miezi sita kwetu ili tuone utekelezaji wa ilani ya CCM 2020 -2025 jinsi unavyotekelzwa;
“Ripoti ya miezi sita itakayoletwa kwetu ikitokea ngazi ya matawi, kata,wilaya hadi mkoa itatupa mwangaza wa kujua ni kwa jinsi gani serikali iliyopo madarakani iliyosimamiwa na CCM inatekelezaje Ilani ya chama chetu, pia tunawapongeza sana Shirika la Reli Tanzania (TRC), Mkandarasi wa ujenzi huu Yapi Merkez na Serikali kwa ushirikiano mzuri katika ujenzi wa reli hii ya mwendokasi” alisema Chongolo.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Morogoro na Mjumbe wa kamati ya siasa wa CCM wa mkoa huo, Martin Shigela, alisema serikali ya Mkoa wa Morogoro wanawashukuru viongozi wa CCM Taifa wakiongozwa na Katibu Mkuu wa chama hicho, Ndugu.Chongolo kwa kutembelea mradi huo na kuona kwa macho kinachoendelea saiti.
“Kwa niaba ya serikali ya Mkoa wa Morogoro tunawashukuru viongozi wetu wa kitaifa wa CCM kutembelea leo mradi wa ujenzi wa reli ya mwendokasi, sisi kama serikali kila siku jukumu letu ni kuhakikisha ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) inatekelezwa kwa asilimia 100% katika mkoa wetu;
“Pia serikali ya mkoa wa Morogoro tunawashukuru viongozi wa shirika la Reli Nchini (TRC) na Mkandarasi wa ujenzi wa reli hii ya mwendokasi (Yapi Merkez) kwa kutupa ushirikiano wa kutosha ilipotokea ajali ya treni kwa kutoa magari tuliyosafirishia wahanga wa ajali ile kuelekea hospitali ya rufaa ya mkoa wa Morogoro”,alisema Shigela.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Masanja Kadogosa, amemshukuru Katibu Mkuu wa CCM, Ndugu. Chongolo na sekretarieti yake kutembelea mradi huo, wao kama shirika inawapatia hamasa ya kuona serikali na chama wapo pamoja nao na kuwazidishia hamasa ya kushirikiana vyema na mkandarasi Yapi Merkez kufanya kazi usiku na mchana ili kukamilisha ujenzi huo kwa wakati.