Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya MICO International Halal Bureau of Certification, kushoto, Hassan Mchomvu akipokea cheti cha kimataifa cha kutoa ithibati ya Halal ya kimataifa kwa bidhaa mbalimbali ikiwemo nyama kutoka kwa ofisa wa Hafsa ya Uturuki Murat Bayka. Kulia ni Mwenyekiti wa Wanawake Waislamu Tanzania, Shamim Khan na kushoto ni Mweka Hazina wa Baraza Kuu la Waislamu (BAKWATA), Sheikh Said Mwenda. Tukio hili lilifanyika hivi karibuni
*******************************
Na Mwandishi Wetu
WATANZANIA wameshauriwa kutumia bidhaa zilizopata ithibati ya Halali ili kuepuka madhara ya kiafya wanayoweza kuyapata.
Wito huo ulitolewa jana Katibu wa MICO Halal Certification Bureau, Sheikh Jumanne Kasonso wakati akizungumzia umuhimu wa bidhaa zenye ithibati ya Halal kwenye ofisi za kampuni hiyo jengo la Butiama Magomeni jijini Dar es Salaam.
MICO ndiyo wakala wa Halal wa Baraza Kuu la Waislamu (BAKWATA) ambayo imepata cheti cha kimataifa kwaajili ya kutoa ithibati ya Halal kwa bidhaa zinazotumika nchini na zile zinasafirishwa kwaajili ya kuuzwa nje ya nchi.
“Halal ni kitu kilichoruhusiwa kisheria ambacho hakina madhara kwa binadamu ili bidhaa iwe Halal lazima ikidhi vigezo au viwango vya nchi husika mfano TBS na baada ya kukidhi vigezo hivyo ikidhi pia vigezo vya kisharia (dini), “ alisema
Hivi karibuni MICO International Halal Bureau of Certification ilipata cheti cha kimataifa kitakachoiwezesha kutoa ithibati ya Halal kutoka kampuni ya Hafsa Halal Certification and Food Import and Export Limited ya Uturuki .
Kuhusu umuhimu wa bidhaa kupata ithibati ya Halal alisema cheti hicho hutolewa na bodi ya Halal ambayo imekidhi viwango vya Halal kimataifa .
Alitaja faida za kupata cheti cha Halal kuwa ni bidhaa kukubalika katika masoko ya kimataifa hasa nyama kwenye masoko ya uarabuni na Asia ambako hawakubali bidhaa isiyo na ithibati ya Halal kutoka taasisi iliyokidhi viwango vya kimataifa
Alisema kwa MICO kupata cheti hicho cha Halal kimataifa kwa mara ya kwanza sasa Tanzania itakuwa na kampuni iliyokidhi viwango vya kimataifa vya ithibati ya Halal .
“Kwa sasa MICO ndiyo kampuni pekee hapa nchini yenye uwezo wa kutoa ithibati ya Halal kimataifa katika bidhaa zote Halal nchini iwe nyama au bidhaa zingine na tunaomba wananchi watumie bidhaa zenye ithibati ya Halal kwa afya zao,” alisema Sheikh Kasonso.
Alitaja faida nyingine kuwa ni bidhaa za Tanzania hususan nyama kukubalika kwenye soko la kimataifa kama uarabuni na barani Asia ambako huwa hawakubali bidhaa ambayo haina nembo ya Halal.
Alisema cheti hicho kitasaidia kuipatia nchi fedha za kigeni kwani kampuni za ndani zitakuwa na uwezo wa kusafirisha bidhaa mbalimbali ikiwemo nyama kwenye mataifa mbalimbali duniani.
“Nchi ilikuwa inapata hasara kwasababu makampuni ya ndani yalikuwa yanachukua ithibati ya Halal nje ya nchi kama Australia, Quatar na kwingineko lakini sasa MICO Halal Tanzania itafanyakazi hiyo na hela zitabaki hapa nchini,” alisema Sheikh Kasonso
Alisema ili kuboresha huduma za Halal, Bakwata na mdau wake MICO Halal International wanaomba serikali iwawezeshe kupata maabara ya Halal kupitia wadau mbalimbali ili kutoa huduma stahili.
Alisema serikali sasa inapaswa kuwaeleza wafanyabiashara waliokuwa wakienda nje ya nchi kutafuta ithibati ya Halal kwamba sasa wasihangaike na badala yake ithibati hiyo inapatikana hapa hapa nchini.
Mwisho