Serikali ya Marekani kupitia mradi wa Afya Shirikishi wa Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) ilikabidhi baiskeli 710 na masanduku 859 ya ukusanyaji wa makohozi kwa wahudumu wa afya ya jamii katika mikoa 8 (Geita, Mwanza, Pwani, Dar es Salaam, Katavi, Kigoma, Rukwa, and Songwe).
…………………………………………………………
Dar es Salaam,
Serikali ya Marekani, kupitia Shirika lake la Maendeleo ya Kimataifa (USAID), na Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa zilikabidhi vifaa na baiskeli kwa wanufaika nchini.
Mradi wa Afya Shirikishi wa USAID umekabidhi baiskeli 710 na masanduku ya kuhifadhi baridi 859 ya usafirishaji wa makohozi yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 235 za Kitanzania. Baiskeli na masanduku ya ukusanyaji wa makohozi ni nyenzo za kufanyia kazi kwa wahudumu wa afya katika ngazi ya jamii ambao hutoa huduma za kifua kikuu (TB) na uzazi wa mpango katika mikoa nane (Geita, Mwanza, Pwani, Dar es Salaam, Katavi, Kigoma, Rukwa, na Songwe). Amref Health Africa inasaidia mikoa hii kuimarisha utambuzi wa wagonjwa wa kifua kikuu katika jamii na kutoa huduma za uzazi wa mpango. Kabla ya kugawa zana hizo, mradi wa Afya Shirikishi umefanikiwa kujenga uwezo kwa wahudumu 735 wa afya katika ngazi ya jamii wakitumia miongozo ya utoaji mafunzo ya taifa.
Katika hafla ya makabidhiano, Mkurugenzi wa Ofisi ya Afya ya USAID, Ananthy Thambinayagam, aliishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uhusiano na ushirikiano na nchi ya Marekani ambao umedumu kwa miaka 60 sasa. “USAID inaridhishwa na mafanikio ya kupunguza idadi ya wagonjwa wa kifua kikuu hapa nchini na ongezeko la upatikanaji wa huduma za uzazi wa mpango kupitia mradi wa USAID Afya Shirikishi. Wakati Tanzania inapoelekea kwenye uchumi wa kujitegemea na kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu ifikapo mwaka 2030, USAID itaendelea kushirikiana kikamilifu na serikali ya Tanzania kuboresha huduma kwa watu wa Tanzania,” alihitimisha.
Afya Shirikishi ni mradi wa miaka mitano wa kuimarisha upatikanaji wa huduma za uzazi wa mpango, kutoa tiba na kuzuia kifua kikuu katika mikoa tisa nchini ikiwemo Zanzibar. Mradi ulianza mwaka 2019 na unatekelezwa na Amref Health Africa kwa kushirikiana na Tanzania Communication and Development Center; Mwitikio wa Kudhibiti Kifua Kikuu na Ukimwi Tanzania; na Service Health and Development for People Living Positively with HIV/AIDS. Mradi wa Afya Shirikishi unafanya shughuli zake chini ya uangalizi wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto; Wizara ya Afya Zanzibar; Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa; na Wizara ya Elimu. Katika mwaka mmoja wa utekelezaji, mradi umeweza kujenga uwezo kwa watumishi 735 katika ngazi ya jamii ambao pia walishiriki moja kwa moja na jamii katika afua mbalimbali za kupambana na ugonjwa wa kifua kikuu, ikiwemo uchunguzi wa kifua kikuu, kuimarisha rufaa ya wahisiwa wa kifua kikuu toka ngazi ya jamii kwenda kwenye vituo vya afya, kuhamasisha na kukuza uelewa, na kuhimiza matumizi ya huduma za uzazi wa mpango katika jamii.