……………………………………………………………..
Adeladius Makwega,WHUSM –Dodoma.
Serikali imekipongeza Kituo cha Sanaa na Utamaduni kwa Viziwi Tanzania (KISUVITA) kwa kuanzisha mashindano ya Miss&Mister Deaf Tanzania ambayo yanayotarajiwa kufanyika septemba 2021.
Akizungumza Ofisini kwake Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Sanaa wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mfaume Said amesema kuwa mashindano haya washindi watakaopatikana watashiriki katika mashindano Kimataifa ya viziwi.
“Kuna vijana na warembo wengi wenye sifa zote kwa ndugu zetu viziwi, hili ni jambo jema na wizara tukishirikiana na KISUVITA maandalizi ya msingi yamekamilika.”Alisema Kaimu Mkurugenzi huyo.
Serikali imetoa na itaendelea kutoa ushirikiano wote kwa KISUVITA kwani wanalolifanya ni jambo la Watanzania na wizara yetu ndiye msimamizi mkuu wa masuala yote ya sanaa.
Akitoa maelezo ya mashindano hayo Bi Hadija Kisubi ambaye ni Afisa Utamaduni wa Wizara ya Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo amesema kuwa haijawahi kutokea mashindano makubwa kama haya ambapo yatakuwa ya kukata na shoka.
“Kama alivyozungumza Kaimu Mkurugenzi wetu Sanaa, mashindano haya yanatarajiwa kufanyika Septemba 14, 2021 katika ukumbi wa Serana Mkoani Dar es Salaam.”
Akizungumzia mashindano hayo Habibi Mrope ambaye ni Mkurugenzi wa KISUVITA amesema kuwa hapo awali waliomba msaada kutoka kwa wadau wengine lakini zoezi hilo liligonga mwamba.
“Lakini tulipowasiliana na wizara yetu jambo hili limekuwa jepesi na limeungwa mkono kwa asilimia 100 na sasa sisi kama KISUVITA tunatembea kifua mbele na hatua za mwisho za kukamilisha mashindano haya zimeshafikiwa. Nawaomba Watanzania mjitokeze kufuatilia mashindano hayo.” Alisema Mkurugenzi huyo wa KISUVITA.
Washindi wanne watakaopatikana katika mshindano hayo wataiwakilisha nchii katika mashindano ya Afrika na baadaye ya Dunia yatakayofanyika mwezi wanne mwakani huko Brazili.