*******************************
Adeladius Makwega
WHUSM-Dodoma
Je unafahamu viwanja vya Mnazi Mmoja? Kwa wale walio wenyeji wa Dar es Salaam kama mie ni jambo la kawaida kuamka asubuhi na kuingia katikati ya Dar es Salaam na kufanya shughuli zetu .Pengine kujua maana ya jina hili na lile hiyo inakua kazi ngumu.
Leo ninachanja mbuga hadi Idara ya Maendeleo ya Utamaduni ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mji wa Serikali–Mtumba Jijini Dodoma na kukutana na Maafisa Utamaduni kufahamu asili ya jina MNAZI MMOJA.
Nakaribishwa katika idara hii ambapo nakutana na kikosi cha Maafisa Utamaduni na Maafisa Sanaa nikijulishwa kuwa idara hizi mbili wapo katika ofisi hiyo pamoja katika Wizara hii.Natambulishwa kwa mwanamama mmoja ambaye najulishwa kuwa anaitwa Bi Hadija Kisubi. Nakaribia napewa kiti naketi na kuanza kusimuliwa juu ya viwanja hivi.
“Viwanja vya Mnazi Mmoja Mashujaa vipo Kata ya Gerezani ndani ya Halmashauri ya Jiji la Ilala linaloongozwa na Mkurugenzi Jumanne Kiango Shauri, kijiografia vinapatikana mitaa yenye majina ya Kihistoria kwa upande wa Kusini vimepakana na barabara ya Uhuru, Kaskazini vimepakana na barabara ya Nkrumah jina la Muasisi mpigania Uhuru wa Nchi ya Ghana, upande wa Mashariki, umepakana na mtaa wa Lumumba, mpigania Uhuru wa Nchi ya Congo (Zaire), Magharibi umepakana na barabara ya Bibi Titi mwanamke shupavu mpigania Uhuru.”
Uwanja una ukubwa wa hekta mbili umezungukwa na vituo vya mabasi, maduka na magenge ya mamalishe kiwanja kisicho na sura nzuri cha Kidongo chekundu, pamoja na shule za Sekondari ya Dar es salaam, na maduka, na maeneo ya nyumba chakavu za Shirika la Nyumba,
Eneo la Gerezani ya kale mahali kilipo kiwanja cha Mnazi Mmoja Mashujaa. Bi Kisubi anasema kuwa wakati wa ujima mmiliki wa eneo, alikuwa ni Mwinyi Mwinyigogo, Mwinyigogo alikuwa ni Bwenyenye, mashamba haya yalikuwa ya mihogo na mpunga tu. Ujio wa Mwaarabu, Suleiman bin Ahmed alinunua mashamba hayo kwa nguo na fedha alipanda minazi yote.
Ndugu msomaji wa makala haya nilikuwa darasani nikipa elimu ya historia ya eneo hili, nikuume sikio sikutoka kwenda msalani wala nini masikio yangu yalisimama kama vile mtoto mdogo anayesubiri kuchomwa sindano na dakitari.
“Enzi ya himaya ya wajerumani 1891-1916 uwanja ulitumika kama kambi ya wanajeshi waliotoka Sudani (wanubi) walihamishwa baada ya vita kuu ya pili ya dunia. Uwanja ulizungukwa na nyumba za matope zilikuwa ni za waafrika. Palizuka moto mkubwa sana minazi yote iliungua moto ukabakia mnazi mmoja tu (kwa bahati haukuungua moto).Mnazi huo umeacha kumbukizi ya kisakale cha jina kubakia ni eneo la Mnazi Mmoja.” Niliendelea kumsikiliza kwa umakini Bi Kisubi huku maafisa wengine wakishangaa mbona baba Mwandishi katulia mno, wakidhani kuna tunazungumza habari za mahaba.
“Mwingereza akaingia Tanganyika akaja na azma yake kuwa na maeneo ya wazi mbinu waliyotumia, iliambatana na Sheria ya (Township rule ya mwaka 1923) hasa katika kiwanja cha Mnazi Mmoja. Kabla ya sheria ilitolewa Ilani ni marufuku kufanya marekebisho ya nyumba mbovu na kubomoa nyumba zote chakavu, mnamo mwaka 1927 nyumba 170 zilivunjwa mwaka 1930 mwezi Januari hadi Juni kuwa ndio mwanzo wa eneo kuwa ni la wazi.”Simulizi ikaendelea.
Pakaitwa uwanja wa wazi wa Mnazi Mmoja, mwaka 1920 Dar es salaam ikapata hadhi ya kuwa mji chini ya Himaya ya Utawala wa Mwingereza na mwaka 1949 ulipata hadhi ya kuwa Manispaa. Viwanja vya Mnazi Mmoja vilianza kutumika kwa sherehe mbalimali za kijamii.
Historia ya Minara ya Mashujaa na Mviga ( Sherehe) za kumbukumbu ya wapingania uhuru mnara wa kwanza ulijengwa enzi za utawala wa Wajerumani mnamo mwaka 1911, mnara wa Herman Von Wissamann Mjerumani aliyeongoza Majeshi ya Wajerumani kupambana na wazalendo wakati wa kueneza ukoloni wa Ujerumani katika mwaka wa1888-1889 uliondolewa baada ya Waingereza kuiteka Dar es salaam mnamo mwaka 1927.Walileta mnara kutoka Uingereza, ulioneshwa awali katika makumbusho ya London.
Nao mnara wa Askari ambao uko kwenye makutano ya barabara ya Azikiwe/Maktaba zamani ilikuwa ikijulikana kama Acacia Avenue (Samora ya leo) na Ingles (Azikiwe/Maktaba) ulijengwa ikiwa ni kumbukumbu ya askari wa Kitanganyika waliokufa kwenye vita ya kwanza ya dunia kati ya mwaka 1914-1916 na enzi hizo kila siku ya mashujaa mashada ya maua huwekwa ikiwa ni kumbukumbu ya askari waliokufa vitani.
Mnara wenye Mwenge wa Uhuru ulijengwa mwaka 1960 na kukamilishwa mwaka 1961. Enzi za Mwalimu J. K. Nyerere ambazo ni enzi za kudai uhuru ndipo mahala palipotumika katika harakati za kudai uhuru.
“Mwalimu Nyerere alilkuwa ni mahali alipokuwa akikutana na wazee mashuhuri akina Abas Sykes, Thomas Mareale, Mzee Azizi Ally na wengineo, wakati wakidai uhuru huku ngoma zikichezwa upande wa Mwenge wa Uhuru wa leo, vikao vilifanyika upande wa mpiga ngoma. Picha ya mpiga ngoma ni mbiu la mgambo la kudai Uhuru, Mwalimu akiwa ni Waziri Mkuu wa kwanza.” Niliendelea kusikiliza simulizi hii ya asili ya jina Mnazi Mmoja.
Baada ya kuweka nukta hiyo Bi Hadija Kisubi alisema kuwa habari na asili ya maeneo mengi zipo na zinajulikana lakini nawashauri Watanzania wapende kusoma na kutembelea taasisi za serikali kuna hadhina kubwa ya tafiti nyingi juu ya mambo ya kitamaduni. Niliagana naye na mie kurudi ofisini kwangu kuganga njaa.