Home Mchanganyiko MAAFISA HABARI WANAJUKUMU LA KUTANGAZA KAZI ZA TAASISI ZAO.

MAAFISA HABARI WANAJUKUMU LA KUTANGAZA KAZI ZA TAASISI ZAO.

0

*******************************

Adeladius Makwega 

WHUSM–Dodoma.

IJUMAA ya Agosti 6, Msemaji wa Serikali na Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo nchini Gerson Msigwa aliacha kiti chake ofisini kigulu na njia hadi Kambarage katika ukumbi wa Hazina Jijini Dodoma ambapo alikutana na Maafisa Habari wenzake kutoka Wizara na Taasisi mbalimbali za Serikali.

Kiongozi huyu alitumia muda wa kutosha kuwasilikiliza japokuwa na yeye kama mwanahabari na Msemaji wa Serikali alikuwa na yake machache kwao.

“Tumieni vyombo vya habari vya maeneo husika na siyo kusubiri chombo cha kitaifa, tumieni vyombo vya habari vya kijamii wana watazamaji, wasomaji na wasikilizaji wengi… hulka ya binadamu ni kusikia mambo yanayomuhusu, mambo yanayomhusu mtu wa Karagwe atapenda kuyasikia katika chombo habari cha Karagwe na ndivyo kitayaeleza vizuri zaidi kuliko chombo cha habari cha kitaifa, chombo cha kitaifa kitaeleza kidogo kidogo ili yafikie nchi nzima… tuwe na mipango ya matangazo na sisi tutumie fursa hiyo kuwafikia Watanzania…wale(wana habari) ni rafiki zetu, ni ndugu zetu na wenzetu” Aliendelea kusema.

Idara hii iliyo chini ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo sasa inafanya kikao cha pili na Maafisa Habari hao tangu Gerson Msigwa awe Msemaji wa Serikali na Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo. 

Hongera sana ndugu Msigwa na watendaji wote wa Idara ya Habari Maelezo. Najua kwa sasa Idara hii inafanya kazi vizuri na inakwenda na wakati. Ikumbukwe wazi kuwa aliyewahi kuwa Mkurugenzi wa Idara hii Dkt. Hassan Abbas alifanya kazi kubwa ya maboresho ya mambo makubwa mawili nayo ni vitendea kazi na rasilimali watu, jambo ambalo kwa sasa si tatizo tena, sasa ni kazi tu. Natoa heko kwa Dkt. Hassan Abbas.

Lakini kuna jambo moja, Serikali ya Tanzania ya Awamu ya Kwanza chini ya Mwalimu Julius Nyerere walikuwa na kusudio la kuanzishwa kwa Televisheni ya Taifa, aliyewahi kuwa Waziri wa Habari wa utawala huo marehemu Daud Mwakawago alipeleka hoja Bungeni juu ya kusudio hilo. Hoja ilijadiliwa na televisheni hiyo ikaanzishwa miaka zaidi ya 20 baadae ambayo sasa ni Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC).

Gazeti la Uhuru la wakati huo, likaripoti “Serikali kuanzisha Televisheni ya Taifa” katika maelezo yanayofuata katika ripoti hiyo yalimtaja Ndugu Daud Mwakawago ambaye ndiye aliyepeleka hoja hiyo Bungeni kama Waziri wa Habari kwa niaba ya serikali.

Leo hii Daud Mwakawago hayupo na pengine hata wanaosoma haya matini  hawa mfahamu hata sura yake lakini huyu huyu anayesoma uchambuzi huu anaitambua na kuitazama hiyo Televisheni ya Taifa-TBC leo hii. Kwani ananufaika kwa kupata habari katika chombo hiki.

Nachosema, jukumu la Afisa Habari kubwa ni kuisemea Serikali na siyo kumsemea  mtu mmoja ambapo ajenda zote za Serikali ziwe za muda mchache au za kudumu ni kwa manufaa ya jamii ya Tanzania. Ajenda hizo katika kila taasisi zinawekwa katika idara au vitengo zikiwa na watenda kazi wenye ujuzi wa idara hizo iwe kilimo, umwagiliaji,uvuvi, tamaduni ama sanaa na mpishi wa habari hizo ndiye  huyo afisa habari.

Serikali ya Awamu ya Nne chini ya Rais Dkt. Jakaya Kikwete walikuja na dhana ya kilimo iliyokuwa ikifahamika kama Kilimo Kwanza ambapo msimamizi mkuu alikuwa Waziri Mkuu wa wakati huo Mizengo Pinda. Walijitahidi kuhakikisha zana za kilimo za bei nafuu zinapatikana kwa wakulima vijijini. Leo hii ukizunguka vijijini ni jambo la kawaida kukutana na “Pawa Tila” ambapo linatumika kulimia, linatumika kama mashine ya kupukuchua mahindi na mazao mengine na pia kama kifaa cha kubebea mizigo mashambani.

Unaweza kumsahau Mizengo Pinda, lakini je unaweza kusahau manufaa ya Pawa Tila kwa mkulima kijijini?  Jawabu unalo.

Jina Bakheresa siyo jina geni nchini Tanzania, lakini ni Watanzania wachache sana wanaomfahamu mmiliki wa Makampuni ya Bakheresa. Huyu jamaa anajishughulisha na uzalishaji wa bidhaa za kilimo na chakula, anasafirisha mizigo na sasa anamiliki  vyombo vya habari, kiwanja cha michezo na timu ya mpira ya Azam. Jina lake Said Salim Bakheresa linafahamika mno kama tajiri mkubwa barani Afrika na Duniani.

Lakini unapotaja jina Bakhresa sura inayokuja kichwani ni bidhaa zinazozalishwa na makampuni yake tu si picha ya mfanyabiashara huyu.

Swali la kujiuliza ni moja tu, Je? Said Salim Bakheresa anashindwa kuijengea jamii wajihi wake na muonekana wake ulivyo? Kama ni mrefu, mnene nakadhalika? Jibu ni kuwa anaweza lakini hiyo haina maana kwa soko lake ya biashara kubwa ni bidhaa, kubwa ni kile kinachofanywa na taasisi yake. Hii ni kwa kampuni ya mtu binafsi vipi kwa Serikali? Hili linatakiwa kuwa mara dufu.

Kama ilivyokuwa kwa Televisheni ya Taifa kwa Daud Mwakawago, Pawa Tila Kwa Mizengo Pinda na bidhaa kwa Said Salim Bakheresa na ndivyo inavyotakiwa kuwa kwa Wizara, taasisi zote za umma kuwekeza mno kusemea kile kinachofanywa na taasisi hizo.

Naweka kalamu yangu chini kwa kusema kwamba kila Afisa Habari wa Serikali kama alivyo mpishi anapaswa kuhahakikisha kile kinachokwenda kuliwa mezani ni kile kinachotakiwa na walaja kwa manufaa ya miili yao na siyo vinginevyo.