Home Makala NYERERE AKUMBUKWA KUAGWA MWILI WA MAREHEMU PADRI RAYMOND SABA

NYERERE AKUMBUKWA KUAGWA MWILI WA MAREHEMU PADRI RAYMOND SABA

0

******************************

Adeladius Makwega

WHUSM –Dodoma.

 ‘Amewalisha kwa ngano bora, aleluya aleluya,

Amewalisha kwa ngano bora,

Amewashibisha kwa asali itokayo mwambani.’

“Labda tuanze kwa kuimba, kama nikiwa mzee nina sauti nzuri kama hii, je nilipokuwa kijana ilikuwaje?” Hayo yalikuwa maneno ya Padri Raymond Saba akisema kwa utani alipokuwa akitoa mada juu ya kanisa hilo Mwanza huku akishangiliwa kwa makofi na vigelegele, nao Mapadri na Maaskofu kadhaa wa Kanisa Katoliki wakimsikiliza.

Aliendelea kufundisha kuwa Baba Mtakatifu Francis katika hati yake mojawapo anasema kuwa dunia ni nyumba yetu ya pamoja, hakuna mwenye haki zaidi ya mwezake, kwa hiyo tuna wajibu wa kutunza nyumba hiyo.

Pengine maneno haya yaliyotamkwa na Padri Raymond Saba wakati wa uhai wake  tuyatumie kuyatafakari mno maisha ya duniani kama sehemu salama kwa kila mmoja wetu kumjali mwenzake iwe katika hali ya neema au vinginevyo.

“Hatutaweza kuisikia tena sauti mpya ya Padri Saba katika mahubiri au akiongoza misa kwani tayari ametangulia mbele ya haki, hatunaye tena tangu Agosti 3 na mazishi yake ni Jumatatu Agosti 9, 2021.” Anasema Raymond Jacob, mlei wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam.

Akiwa ni Padri kutoka Kanisa Katoliki Jimbo la Kigoma aliyewahi kushika nafasi mbalimbali kama vile Paroko wa Parokia kadhaa, Mkuu wa Seminari na hadi Katibu Mkuu wa Baraza la Masskofu Katoliki Tanzania (TEC) aliweza kufanya kazi kwa uwezo wake wote bila ya kuchoka alinijulisha Bibi Maria Katabuhaga kutoka Jimbo katoliki la Kigoma.

Akizungumza  katika misa maalumu ya kuuaga mwili wa Padri Saba Jimbo kuu la Dar es Salaam Katibu Mkuu wa TEC  Padri  Charles Kitima amesema kuwa

“Padri Saba japokuwa tulimuuguza, matumaini yetu kwa yeye kupona yalikuwa makubwa sana, kama Baraza la Maskofu. Maaskofu, mapadri wote na walei wote tunaungana na wafiwa kwani mwezetu huyu alikuwa akijali sana mahusiano yake na Mungu na hata alipokuwa mgonjwa aliendelea kuwa jirani na Mungu.” Alisema Padri Kitima

Akitoa salaam kwa jimbo la Kigoma, Katibu Mkuu wa TEC amesema kuwa Padri Saba ameacha mengi yasiyofutika katika kanisa kwani kwake kanisa lilikuwa ni kila kitu.

“Mwaka 2013 nilipewa jukumu la kujenga Chuo Kikuu cha Vikindu, aliweza kujitoa sadaka na alionesha ukalimu mkubwa na alijitoa sana na kufanikisha ujenzi wa chuo hicho.”Aliongeza Padri Kitima.

Yeye ndiye aliyetengeneza mfumo wa TEC ambapo alitumia wataalam wetu kukamilisha jukumu hilo. Aliongeza kuwa taasisi hili iliweze kwenda na mfumo wa kisasa ikawa jambo jepesi hata anapokuja kiongozi mpya TEC aweze kufahamu pale alipoishia mwenzake.

“Aliweza kulipa madeni yote ya baraza kwani mimi (Padri Kitima) nimefika 2018 hakuna deni hata moja na mahusiano na taasisi za serikali yalikuwa mazuri, mahusiana na wafadhili wote  yalikuwa pia vizuri sana.” Aliendelea kusema kiongozi huyo wa TEC.

Hata sasa baraza lipo katika kipindi kigumu cha Corona lakini TEC inaendelea vizuri kabisa kutokana na mahusiano mazuri na wafadhili na hizo ni alama ambazo hazifutiki kabisa.Pale mtu anapofanya majukumu yake, ni vizuri kuacha alama kwa jamii kwani ufalme wa Mungu unajengwa kwa ishara, nayeye ameacha ishara nyingi kwetu kwa kuyafanya mambo makubwa.

Siku moja tulikuwa tunazungumza naye juu ya Mtumishi wa Mungu Mwalimu Julius Nyerere aliyajenga wapi maisha yake ya kiroho na ya kisiasa? Tuliyatazama mahusiano juu ya Julius Nyerere na wanasiasa waliompenda Yesu. Mwalimu alikuwa na urafiki na Kansela wa ujerumani Conrad Adenauer ambaye aliongoza iliyokuwa Ujerumani Mashariki tangu mwaka 1949 hadi 1963.

“Hakuishia hapo rafiki mwingine alikuwa ni Robert Shummer ambaye alikuwa Rais wa Ufaransa, huyu aliishi kama Padri na hakuwahi kuwa na familia. Mwalimu Nyerere alikuwa akienda huko kujifunza zaidi siasa na masuala ya kiroho. Kwa hakika hawa jamaa waliokuwa na urafiki na Mwalimu Nyerere na katika mataifa yao waliacha alama kubwa ya maisha ya kisiasa yaliyoambatana na Ukatoliki ndani ya Ujerumani na Ufaransa.” Alitoa mfano huo Padri Kitima.

John F. Kennedy aliyewahi kuwa Rais wa Marekani ambaye alikuwa Mkatoliki pia Mwalimu Nyerere alimtembelea na nayeye ndiye aliyesema “Afrika lazima isaidiwe kujikomboa dhidi ya ukoloni.” Robert Shummer alisema kuwa ni lazima mwanasiasa awe ni mtu wa sala na ndiyo maana Mwalimu Nyerere alikuwa hakosi kuhudhuria ibada za asubuhi kanisani.

Naye Conrad Adenauer alisema “Lazima haki za msingi na utu wa mtu na mafundisho ya kanisa yapenye ndani ya maisha siasa na uchumi wa taifa.” TEC waliongeza kuwa hata Padri Raymond Saba naye aliyahimiza mno mambo haya katika sala.

“Conrad Adenauer, John F Kennedy na Robert Shummer kwa sehemu kubwa ndiyo waliokuwa mfano wa kuiga kwake Mwalimu Nyerere kwani walikuwa ni wanasiasa na Wakatoliki wenzake.” Aliniambia Padri Saba akiwa hai anasema Katibu Mkuu wa TEC.

Kwa upande wake Askofu Msaidizi Mteule wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam Henry Mchamungu amesema kuwa ni kweli Padri Saba amefariki akiwa kijana na pengine kabla ya wakati wake huku akiamini  kuwa uzee wenye heshima siyo wingi wa miaka.

“Idadi ya miaka inajengwa na maisha safi kwa kila mmoja wetu.” Ameongeza kuwa kila mmoja wetu anatakiwa kuwa jirani na Mungu wakati wowote kwani hakuna anayeweza kufahamu lini atafariki.

Kwa hakika Padri Raymond Saba amemaliza maisha yake ya hapa duniani na leo hii  hatunaye tena, pole kwa familia, pole kwa watawa wote,  pole kwa Kanisa katoliki Jimbo la Kigoma na pole kwa  Kanisa Katoliki la Tanzania na pole kwa Baraza na Maaskofu Katoliki Tanzania.