Na Mwandishi wetu, Simanjiro
MCHIMBAJI maarufu wa madini ya Tanzanite Bilionea Saniniu Laizer, ameiomba Serikali kufanikisha upatikanaji wa nishati ya umeme kwenye vijiji vya jamii ya wafugaji Wilayani Simanjiro ili binadamu na mifugo ipate maji yaliyochimbwa visimani.
Bilionea Laizer amesema jamii ya wafugaji wa vijiji vya Lengasiti na Olchoronyori wanatumia gharama kubwa kununua mafuta ya kusukuma maji ya visima ili kunywesha mifugo yao.
Akizungumza mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro, Dk Suleimani Serera, mchimbaji huyo maarufu amesema kuna visima vitatu vya maji eneo hilo ila hakuna umeme wa kusukuma maji.
“Kati ya visima vitatu vya maeneo hayo, kimoja kilichimbwa na serikali na viwili nilichimba kwa gharama zangu ila hakuna nishati ya umeme hivyo serikali itusaidie,” amesema Bilionea Laizer.
Amesema gharama ya kununua mafuta ya diseli ya kuendesha mitambo hiyo ni kubwa kwani lita 200 zinamalizika kwa siku mbili katika kuhudumia mifugo zaidi ya 10,000.
Amesema jamii ya wafugaji wa eneo hilo wanapaswa kuangaliwa na serikali kwa jicho la huruma kwani umeme ukiwepo utarahisisha maendeleo yao.
Hata hivyo, Dk Serera amesema Serikali itahakikisha eneo hilo linapatiwa nishati ya umeme ili kufanikisha upatikanaji wa maji kwa urahisi hivyo watu na mifugo kunufaika.
Dk Serera amesema serikali itaunga mkono juhudi za wadau wa maendeleo mfano wa Bilionea Laizer ambao wanatumia fedha zao kwa ajili ya kunufaisha jamii inayowazunguka.
Amesema meneja wa wakala wa usambazaji maji na usafi wa mazingira vijijini (Ruwasa) wilaya ya Simanjiro mhandisi Joanes Martin ni kijana mchapakazi atamuagiza afuatilie hilo.
“Miongoni mwa vijana wachapakazi ninaowaamini hapa Simanjiro ni mkuu wa idara ya maji yule mhandisi Joanes anachapa kazi vizuri atasimamia hili lifanikiwe,” amesema Dk Serera.
Amesema serikali ilishahidi kuwa itahakikisha vijiji vyote vinapatiwa nishati ya umeme hivyo na wao Simanjiro watahakikisha Rea inafika maeneo yasiyo na umeme ili wapate maji.
“Tunafahamu kuwa kuna umuhimu mkubwa kwa jamii hasa zilizopo pembezoni kupatiwa na serikali huduma mbalimbali za maendeleo ikiwemo nishati ya umeme,” amesema Dk Serera.