Na Mwandishi wetu, Simanjiro
MKUU wa Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, Dk Suleiman Serera, amewataka wanasiasa, viongozi na wananchi wa eneo hilo kuachana na siasa za unaharakati na kugeukia siasa za maendeleo.
Dk Serera ameyasema hayo alipotembelea na kukagua shule ya serikali ya msingi ya Bilionea Saniniu Laizer ya mchepuo wa kiingereza iliyojengwa na mchimbaji huyo maarufu wa madini ya Tanzanite.
Amesema maendeleo ya wilaya ya Simanjiro hayatapatikana endapo kutakuwa na siasa za uanaharakati badala ya kulenga kwenye malengo ya maendeleo katika sekta mbalimbali.
Amesema kila mmoja akiimba wimbo wa maendeleo watafika mbali kwa maendeleo ila wakianza kuweka kipaumbele kwenye siasa hizo za uanaharakati hawatafika popote.
“Mimi nikiwa na kauli moja, mbunge akiwa na kauli moja, Mwenyekiti wa halmashauri na madiwani tukiwa na kauli moja ya maendeleo tutaifikisha mbali Simanjiro yetu,” amesema Dk Serera.
Mjumbe wa halmashauri kuu ya CCM mkoa wa Manyara, Kiria Laizer amesema baadhi ya watu wasio na nia njema wamekuwa wanamkatisha tamaa bilionea Laizer kwa maneno ya uzushi.
“Bilionea Laizer amekuwa akisaidia jamii ila kumekuwa na wakatishaji tamaa wanajenga hoja za fitina kwa lugha ambazo hawafanyi utafiti, zinazorudisha nyuma maendelo,” amesema Laizer.
Bilionea Laizer amesema shule hiyo imekuwa tumaini kwa jamii ya wafugaji na wakulima wadogo ila wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo upungufu wa walimu.
“Nitajenga bwalo la kulia chakula hivyo tunaiomba serikali ijenge bweni ili Esto wa wafugaji na wakulima waweze kulala na tuwabane wasome na kusaidia jamii baadae,” amesema bilionea Laizer.
Kaimu Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Simanjiro, Silvanus Tairo amesema shule hiyo ilianza kujengwa madarasa mawili na hivi sasa imekamilisha madarasa yake.
“Tunampongeza mdau wetu wa maendeleo bilionea Laizer ambaye ameacha alama kubwa kwa kujenga shule hii ambayo ni ukombozi wa elimu kwani ni ya mfano kwa mkoa,” amesema Tairo.