……………………………………………………..
MKUU wa Mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge amezindua chanjo ya UVIKO 19 kwa kuwa Raia wa kwanza mkoani Ruvuma kuchanja chanjo hiyo kwenye ukumbi wa Manispaa ya Songea.
Katibu Tawala Mkoa wa Ruvuma Stephen Ndaki alikuwa ni Raia wa pili kuchanjwa akifuatiwa na Kamati yote ya Ulinzi na Usalama Mkoa wa Ruvuma.Wazee na viongozi mbalimbali wa dini pia walijitokeza kwa hiari kuchanjwa chanjo hiyo.
Akizungumza kabla ya uzinduzi huo,Mganga Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Dr.Jairy Khanga amesema Mkoa wa Ruvuma wenye watu zaidi ya milioni 1.6 katika awamu ya kwanza umeletewa chanjo dozi 30,000.
Mgeni rasmi kwenye uzinduzi huo Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge akizungumza kabla ya kuzindua chanjo hiyo ametoa rai kwa wananchi kunawa mikono mara kwa mara kwa maji safi tiririka na sabuni,kuvaa barakoa wakati wote wanapokuwa kwenye mikusanyiko na kutumia vipukusa mikono.
Hata hivyo amewashauri wananchi mkoani Ruvuma kupata chanjo ya UVIKO 19 kwa hiari kwa kuzingatia sifa zilizoelekezwa na wataalam wa afya,kupata lishe bora na kufanya mazoezi.
“Kutokana na wimbi la tatu la UVIKO 19 katika Mkoa wa Ruvuma naelekeza viongozi wa ngazi zote waoneshe mfano kwa wananchi kwa kuchukua hatua za tahadhari za kujikinga dhidi ya UVIKO 19’’,alisisitiza RC Ibuge.
Mkuu wa Mkoa amewaagiza viongozi wa Taasisi zote wahakikishe wanasimamia upatikanaji wa vifaa kinga kama barakoa,maji tiririka na sabuni,pia ametoa rai kwa vyombo vya mawasiliano mkoani Ruvuma kutoa elimu kwa jamii kuhusu njia sahihi za kujikinga na UVIKO 19.
RC Ibuge ameziagiza Halmashauri zote kuhakikisha kuwa maeneo yote yenye mikusanyiko ya watu kama stendi,bustani za kupumzikia,misikitini na makanisani kunakuwa na vifaa vya kunawia mikono.
Amewaagiza viongozi wa dini wahakikishe kuwa waumini wote wanavaa barakoa wakati wote wa Ibada na kukaa umbali usiozidi mita moja mtu mmoja hadi mwingine na kwamba Ibada ziwe za muda mfupi usiozidi saa mbili na kwamba huduma zinazohusiana kugusana ziepukwe.
Katika hatua nyingine Mkuu wa Mkoa kuanzia Agosti 4 mwaka huu amesitisha mikusanyiko yote mikubwa ya kijamii,kidini na kisiasa hadi ugonjwa utakapodhitibiwa na kutolewa taarifa rasmi na Wizara ya Afya.
Hata hivyo amesema mikusanyiko ya lazima,wananchi watalazimika kuomba kibali kutoka kwenye Mamlaka husika.