Kamisaa wa Sensa ya Watu na Makazi Anna Makinda (kushoto) akizungumza na Mkuu wa Mkoa wa Tabora Balozi Dkt Batilda Buriani (kulia) wakati apokuwa katika ziara ya siku leo ya kuangalia mandalizi ya zoezi la Sensa ya watu na Makazi Mwezi Agosti mwaka 2022.
Kamisaa wa Sensa ya Watu na Makazi Anna Makinda (kulia) akijadiliana jambo na Mkuu wa Mkoa wa Tabora Balozi Dkt Batilda Buriani (kushoto) mara baada ya kumalizi kikao kifupi leo kilichokuwa na lengo la kuangalia mandalizi ya zoezi la Sensa ya watu na Makazi Mwezi Agosti mwaka 2022
Picha na Tiganya Vincent
*****************************
NA TIGANYA VINCENT
WATANZANIA na wageni wote wametakiwa kujitokeza kushiriki zoezi la sensa ya watu na makazi mwezi Agosti mwakani katika tarehe itakayopangwa kwa ajili ya kuiwezesha Serikali kupata takwimu sahihi zitakazoiwezesha kupanga mipango ya maendeleo.
Kauli hiyo imetolewa leo na Kamisaa wa Sensa ya Watu na Makazi Anna Makinda alipokutana na Mkuu wa Mkoa wa Tabora Balozi Dkt Batilda Buriani akiwa katika ziara ya kuangalia mandalizi ya zoezi hilo kubwa katika mikoa mbalimbali hapa nchini.
“Katika siku hiyo Watanzania wote na wasafiri wote na wakimbizi wote watakuwepo katika eneo la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania watahesabiwa” amesisitiza.
Makinda amesema sensa ya watu na makazi ijayo itafanyika kitaalamu zaidi kwa kutumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano(TEHAMA ikwemo matumizi vishikwambi( tablets) wakati wa zoezi la kuheshabu watu na hivyo kupunguza matumizi ya karatasi.
Ameongeza kuwa zoezi hilo litakuwa tofauti na awamu za Sensa ya watu na makazi zilizopita kwa kuwa safari hii itafanyika hadi ngazi ya vitongoji kwa maeneo ya vijijini na mijini kwenye Mitaa.
Makinda amesema kwa Mitaa kwa kuwa watakuwa wengi watapangwa kwa kundi la watu 50.
Amesema sensa ijayo itatoa picha halisi ya idadi ya wananchi waliopo na kuwezesha Serikali kupanga mipango yake ya maendeleo kwa wananchi vizuri ikiwemo kuepuka suala la kukimbizana kila mwaka katika suala la upungufu wa madawati na huduma nyingine za kijamii.
Aidha Kamisaa huyo wa Sensa ya Watu na Makazi ameuagiza uongozi wa Mkoa huo wa Tabora kutumia vyombo vya habari na zikiwe Redio zinapatikana mkoani humo katika utoaji elimu na kuhamasisha jamii ili watu wote wajitokea hapo mwakani katika kushiriki zoezi hilo muhimu.
Amesema ni vema vyombo vya habari visaidie kutoa elimu kwa jamii kuwa sensa ya watu na makazi haina upande wote wala itikadi yoyote.
Makinda amesema watu wanatakiwa kuona ni ufahari kuwa sehemu ya watu watakahesabiwa hapo mwakani mwezi Agosti katika tarehe itakayopangwa.
Mkuu wa Mkoa wa Tabora Balozi Dkt. Batilda Buriani amesema Mkoa wa Tabora tayari umeshaunda Kamati ya Sensa ya watu na Makazi ya Mkoa na kutoa majukumu kwa kila Mjumbe.
Sensa ya watu na makazi ya mwakani itakuwa ya sita kufanyika hapa nchini tangu Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilianzishwa 1964 na imekuwa ikifanyika kila baada ya miaka 10.