Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Iringa
Serikali imeelekeza Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko (CPB) kununua mahinidi kiasi cha Tani 10,400 zilizohifadhiwa na Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula-NFRA Kanda ya Makambako kwa miaka mitatu mfululizo.
Akizungumza wakati wa ziara ya kikazi ya siku mbili mkoani Njombe iliyoanza tarehe 3 Agosti 2021, Waziri wa Kilimo Mhe. Prof Adolf Mkenda amesema kuwa Bodi hiyo imepewa jukumu na serikali la kununua na kuuza nafaka hivyo inapaswa kununua mahindi hayo ambayo yamehifadhiwa katika ubora wa hali ya juu.
Waziri Mkenda amesema kuwa mahindi hayo yaliyohifadhiwa na NFRA yanapswa kuzungushwa/kuuzwa ili kutoa fursa kwa NFRA kuingia sokoni kununua mahindi mengine jambo litakalopelekea wakulima kuwa na ahueni ya soko.
“NFRA ikiingia sokoni itatoa nafasi kwa wakulima watakaouza mahindi yao kuweza kununua pembejeo bora na kulima zaidi mazao ya nafaka” Amekaririwa Waziri Mkenda
Amesema kuwa kazi ya NFRA ni kununua nafaka na kuhifadhi ili ikitokea changamoto yoyote nchini nafaka hiyo iweze kutolewa lakini kwa kuwa hakuna changamoto yoyote iliyojitokeza nchini kwa kipindi cha miaka mitatu hivyo wanapaswa kuyauza ili kununua mahindi mengine kwa ajili ya kuhifadhi.
Waziri Mkenda amesema kuwa pamoja na mahindi yaliyohifadhiwa kwenye ghala la NFRA Makambako lakini pia kuna Tani 5009.267 za mpunga ambazo pia zinapaswa kutafutiwa masoko hususani ya nje ya nchi.
Akizungumzia kuhusu kusuasua kwa mradi wa ujenzi wa Maghala na Vihenge vya Kisasa Waziri Mkenda amesema kuwa ujenzi huo unafanywa kwa mkopo wa bei nafuu hivyo mkandarasi anapaswa kuhakikisha anamalizia kazi kwa haraka kwa mujibu wa makubaliano.
Katika ziara hiyo ya kikazi ya Waziri wa Kilimo Mhe. Prof Adolf Mkenda kwa siku mbili mkoani Njombe, Waziri Mkenda ametembelea na kukagua ghala la mbolea na Mtewele General Traders, Ghala la YARA, Ghala la ETG, pamoja na kukagua Skimu ya umwagiliaji ya Itipingi.
Waziri Mkenda anatarajiwa kuendelea na ziara ya kikazi katika mkoa wa Songwe na Rukwa kesho tarehe 4 Agosti 2021 na tarehe 5 Agosti 2021.