Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani( kushoto) na Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati, Kheri Mahimbali(katikati) wakikagua sehemu ya mitambo iliyoungua katika Kituo cha Kupokea na Kupoza umeme cha Msamvu mkoani Morogoro, Agosti 03,2021.
Moja ya Miundombinu ya umeme iliyoungua katika Kituo cha Kupokea na Kupoza umeme cha Msamvu mkoani Morogoro, Waziri wa Nishati alifanya ziara ya kukagua kituo hicho Agosti 03, 2021.
Sehemu ya mitambo iliyoungua katika kituo cha kupokea na kupoza umeme cha Msamvu mkoani Morogoro, Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani na ujumbe wake walifanya ziara ya kukagua athari za moto katika kituo hicho Agosti 03, 2021.
***************************
Na Zuena Msuya
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani amewasimamisha kazi wahandisi watatu wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kupisha uchunguzi baada ya Kituo cha Kupoza na Kusambaza Umeme Msamvu kuungua moto na kusababisha hasara ya takribani shilingi Bilioni 2.
Aidha amemuagiza Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Kheri Mahimbali kuunda kamati ya kuchunguza na kubaini chanzo halisi cha Moto huo na hasara iliyopatika ndani ya siku tano kuanzia leo (Agosti 3, 2021).
Katika ziara hiyo, Dkt. Kalemani aliambatana na Naibu Katibu Mkuu wizara hiyo, Kheri Mahimbali, Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Edward Ishengoma, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Dkt.Tito Mwinuka pamoja na viongozi wengine waandamizi wa Wizara na TANESCO.
Sambamba na hilo aliiagiza Kampuni ya inayotekeleza Mradi wa Reli ya Umeme (SGR) kumchungumza mhandisi wake anayedaiwa kusababisha hitilafu hiyo kwa kukata waya wa umeme na kari la kuchimbua barabara wakati akitekeleza majukumu yake na kuchukuliwa hatua pindi itakapobainika.
Dkt. Kalemani alisema hayo, Mkoani Morogoro, Agosti 03, 2021 alipofanya ziara ya kukagua kituo cha Kupoza na Kusambaza Umeme cha Msamvu kilichoungua moto Jana baada ya kutokea hitilafu na kusababisha wananchi kukosa Umeme.
Dkt. Kalemani alifafanua kuwa wahandisi hao wa TANESCO, wamesimamishwa kwa kushindwa kubaini hitilafu iliyotokea katika mifumo ya kuendeshea mitambo kituoni hapo, na kusababisha harasa kubwa kwa taifa baada ya kituo hicho kuungua moto.
“Wahandisi waliokuwa zamu siku hiyo wasimamishwe kazi kuanzia Sasa kwa kushindwa kubaini mapema hitilafu iliyotokea katika mifumo na kusababisha hasara kubwa kwa Taifa, wakati walikuwepo kazini,pia matukio ya moto yamekuwa mengi lazima tuchunguze kufahamu kama kuna yeyote anahujumu miundombinu ya umeme”, alisema Dkt. Kalemani
Hata hivyo aliitaka TANESCO kufanya kazi usiku na mchana kuhakikisha umeme unarejea katika maeneo yote ndani ya saa 24 kuanzia leo,vilevile waongeze wataalam kutoka vituo vingine ili kuongeza nguvu kazi na kukamilisha kazi hiyo haraka.
Aidha Dkt. Kalemani aliwataka TANESCO kuharakisha manunuzi ya vifaa na miundombinu yoyote iliyoungua kwa kutumia mfumo wa dharura usioathiri taratibu za manunuzi ili kurejesha kituo hicho katika hali yake ya kawaida ndani ya kipindi kifupi.
Vilevile aliwata TANESCO kuhakikisha kuwa vituo vyote vya vilivyojenga zamani za kupoza na kusambaza umeme vinakuwa na mifumo maalum ya kubaini hitalafu ikitokea na namna ya kuidhibiti kabla ya madhara makubwa kutokea.
Pamoja na mambo mengine aliwaagiza kuweka alama katika maeneo yote ambayo miundombinu mikubwa ya umeme imepita chini ya ardhi hasa nyaya ili kutoa tahadhari kwa watakaokuwa wakifanya kazi au kupita maeneo hayo.
Pamoja na mambo mengine aliwataka wananchi ambao bado huduma ya umeme haijarejea kuendelea kuvuta subira wakati wataalam wakiendelea kufanya kazi zao, na kwamba tayari baadhi ya vifaa kutoka mkoani Singida viko njiani kuwasili eneo hilo ili kuhakikisha huduma ya umeme inarejea maeneo yote ndani ya muda mfupi.