Mwandishi wa Habari na Mpiga picha wa Kujitegemea nchini, Andrew Chale akipata chanjo ya UVIKO 19 ya JJ mapema jana 2 Agosti mwaka huu katika ukumbi wa Karimjee iliyotolewa maalum kwa hiyari kwa kundi la Wanahabari na Wahariri wa Vyombo vya Habari nchini.
****************************
Na Mwandishi Wetu.
MWANDISHI wa Habari na Mpiga picha wa Kujitegemea Bw. Andrew Chale ametoa wito kwa Wana tasnia ya Habari nchini kuwa makini katika kutoa taarifa kwa Umma juu ya chanjo ya UVIKO 19 ambayo imeanza kutolewa kwa makundi maalum nchini kote kuanzia leo 3 Agosti baada ya kuzinduliwa rasmi na Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan hivi karibuni Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Andrew Chale amebainisha hayo wakati wa kutoa wito kwa Wanahabari kwa hiyari yao wenyewe kuchangamkia fursa hiyo ya chanjo kwani wao ni miongoni mwa makundi yaliyo kwenye hatari ya kupata virusi hivyo wawapo kwenye majukumu yao ya kila siku huku pia akiwataka kuzingatia weredi wa kuripoti taarifa za chanjo.
“Kwanza namshukuru Mungu kwa chanjo hii. Ni maamuzi yangu na nimefanya kwa hiyari. Mwili wangu thamani yangu, nimechanjwa chanjo ya UVIKO19 ya Jenseen (JJ), ili kulinda familia yangu na wengine zoezi lililofanyika jana pale ukumbi wa Karimjee” Alisema Andrew Chale
Na kuongeza kuwa, ameungana na Rais Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha Tanzania inaendelea kuwa salama dhidi ya virusi vya UVIKO 19.
“Mimi ni Mwanahabari naenda sehemu mbalimbali ndani na nje ya nchi. Nakutana na watu tofauti hivyo naamini chanjo hii niliyopata itasaidia kuzuia madhara kadri ya uwezo wake, Naungana na Rais Samia Suluhu Hassan.” Alisema Andrew Chale.
Ambapo alitoa wito kwa Wanahabari kujiepusha na tabia ya kusambaza ama kuchochea kauli za watu wa vijiweni juu ya chanjo za UVIKO 19 kwani zitaleta taharuki kubwa kwa jamii ambayo inapokea taarifa kutoka kwa watu wanaoaminika wakiwemo hao Wanahabari.
“Kumekuwa na Wanahabari kwa namna moja ama nyingine wanafanya kwa lengo la kujifurahisha ama kujiona wapo sahihi kusambaza taarifa zisizo nzuri na sahihi juu ya chanjo.
Wapo wanaosambaza viunganishi vya mitandao ya kihabari (Link) na hata picha au Maandishi wakibandika kwenye mitandao ya ya habari lakini wanajisahau kuwa kuna sheria za makosa ya kimtandao, tuache ni bora kukaa kimya maana chanjo ni ya hiyari” Alisema Andrew Chale
Aidha, ametoa tahadhari kwa vyombo vya habari kuwa makini na picha zinazoonyesha faragha ya mwili za wanaopata chanjo.
“Zoezi la chanjo duniani kote ni la hiyari ndio maana wengi wanaopata nafasi ya kuchoma chanjo wanapata picha ya ukumbusho kama kielelezo cha kuhamasisha wengine… leo tumeshuhudia picha ya Mbunge wa Viti Maalum wa CCM, Mhe. Catherine Magige aliyokuwa akipata chanjo na kutolewa na mtandao wa chombo kinachoaminika kimaadili na weredi cha Mwananchi kuruhusu ile picha.
“Huenda aina ubaya kwa aliyepiga na kupigwa lakini haikuwa sahihi kwenda hewani ama kwa matumizi kutokana na muonekano wake kwa maadili ya Mtanzania ikizingatiwa muhusika ni kiongozi na kiop cha jamii bila shaka Mwananchi wataomba radhi ama kutoa neno”. Alisema Andrew Chale.
Katika hatua nyingine Wanahabari wengine wameendelea kutoa hamasa kwa Jamii na Wanahabari kukitokeza kwa hiyari kupata chanjo.
Mwanahabari wa kituo cha ITV mkoani Morogoro Idda Mushi:
“Ni hiyari….
Lakini Binafsi nimeamua.Leo nimepata chanjo ya Johnson, kujikinga dhidi ya UVIKO 19, lakini sitaacha kuendelea kujikinga na kujilinda na maambukizi kwa kutumia barakoa kwenye msongamano, malimao, tangawizi, karafuu, kujifukiza nk
“Kinga hii sio sababu ya kutougua, lakini nina amini hata maambukizi yakija bahati mbaya kinga yangu itasaidia kupambana na maambukizi na madhara yasiwe makubwa Sana..Chukua hatua, Kinga ni bora kuliko tiba”. Alisema Idda Mushi wakati wa zoezi la chanjo kwa mkoa wa morogoro lililoongozwa na Mkuu wa Mkoa huo.
Kwa upande wake, Mwandishi wa redio Times (Radio Times fm), James Salvatory ambaye alipata chanjo hiyo siku ya kwanza ya uzinduzo alisema:
“Nimepata nafasi ya kuchanjwa toka siku ya kwanza ambapo Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan alipozindua pale Magogoni Ikulu ya Dar es salaam.
Nachoweza kusema tu toka nichanje sijapata shida yoyote ya kiafya ni mzima kabisa naendelea na kazi zangu kama kawaida niwasihi watu kuepuka maneno ya upotoshaji juu ya chanjo
Anaejua maumivu ya mwili wako ni wewe na si mtu mwingine acha na propaganda za mitaani juu ya taarifa potofu juu ya chanjo fuata maelekezo ya wataalamu wa afya wao ndiyo wanaujua ukweli.
Wahenga husema Kinga ni bora kuliko tiba nenda kuchanje wakati ni sasa” Alisema James Salvatory.
Zoezi hilo la chanjo kwa Tanzania nzima linaendeshwa kwa hiyari huku awamu ya kwanza likianza na makundi maalumu katika jamii ikiwemo wale wenye magonjwa sugu, walio na umri kuanzia miaka 50 ambapo vituo maalum ikiwemo vya afya na hospitali za Umma na binafsi watapokea chanjo hiyo.