Na Dotto Mwaibale, Singida
SHIRIKA la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Singida kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi limetoa onyo kwa mtu yeyote atakayebainika akihujumu miundombinu ya njia kuu ya umeme wa 400 KV unaoanzia Singida kupitia Manyara hadi Namanga mkoani Arusha kwenda nchini Kenya.
Onyo hilo limetolewa katika mkutano wa hadhara ulioandaliwa na Tanesco wenye lengo la kutoa elimu kwa wananchi ya kulinda miundombinu hiyo baada ya kujitokeza kwa baadhi ya watu wasio waaminifu wa Kijiji cha Sagara na maeneo nengine wilayani Singida kudaiwa kuanza kuiba vyuma vya nguzo za umeme wa mradi huo.
Akizungumza kwenye mkutano huo Afisa Usalama wa Tanesco Mkoa wa Singida, Davis Mkwiche alisema inasikitisha sana kuona mradi huo mkubwa unaotekelezwa na Serikali kwa fedha nyingi zinazotokana na kodi za wananchi ukianza kuhujumiwa na watu wachache kwa kuharibu miundombinu mbinu yake.
“Njia ya mradi huu hivi sasa ipo katika hatua za mwisho za ujenzi na kama mambo yatakwenda vizuri miezi miwili ijayo itakabidhiwa kutoka kwa mkandarasi kuja kwetu lakini tukiwa katika hatua hizi za mwisho imebainika baadhi ya watu wachache wenye nia hovu wameanza kufanya vitendo vya hujuma kwenye njia ya kusafirisha umeme,” alisema Mkwiche.
Alisema watu hao wanafungua vyuma kwenye nguzo za chuma za msongo wa umeme wa 400KV vinavyo julikana kwa jina la kitaalumu miiba au vifaa vinavyowekwa kuzuia mtu asiyetakiwa, kuidhinishwa, asiye na utaalamu kuweza kupanda kwenye hizo nguzo.
Uchunguzi wa awali uliofanywa na shirika hilo umebaini kuwa vyuma hivyo vikishatolewa kwenye nguzo hizo vinaenda kutumika kwenye matumizi mbalimbali ikiwemo kuwekwa kwenye mikokoteni inayovutwa na wanyama, wengine wanaenda kutengenezea bangiri, utengenezaji wa mikuki hama mishale na wengine wanaenda kuviuza kwa wanunuzi wa vyuma chakavu.
Akizungumza kwenye mkutano huo kwa niaba ya Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Singida, Mkaguzi wa Polisi Ninga Gewe alisema kwa mujibu wa mwenendo wa makosa ya jinai Tanzania kuanzia kifungu cha 14 hadi 16 kinamruhusu raia au mwananchi mzalendo kumkamata mhalifu bila kumpiga na kumpeleka ofisi ya mtendaji wa kijiji au kituo cha polisi lakini awe ametenda kosa husika na siyo kwa kumuonea.
Alisema kosa lolote la kuharibu au kuiba miundombinu ya Tanzania ni kosa la kuhujumu uchumi wa nchi ambapo mtuhumiwa akikamatwa hakuna dhamana.
Gewe alitumia nafasi hiyo kutoa onyo kwa wananchi wa kijiji hicho na maeneo mengine kuacha mara moja vitendo hivyo vya kuhujumu miundombinu ya Serikali na jeshi la polisi alipendi kuona mwananchi hata mmoja akikamatwa kwa tuhuma za kuharibu miundombinu na kujikuta akifungwa kifungo cha maisha kwa sababu hiyo.
Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Singida katika mkutano huo Afisa Tarafa ya Mungumaji, Ally Mwendo alisema miradi hiyo ni lazima ilindwe kwa nguvu zote na kuwa mlinzi wa kwanza ni mwananchi mwenyewe na sio mtu mwingine.
Aidha ametoa maagizo kwa viongozi wote wa kijiji hicho kuwa walinzi wa mradi huo na mingine yote ambayo inatekelezwa na iliyokwisha kamilika.
Afisa Mkuu Usalama na Uzuiaji kutoka Makao Makuu ya Tanesco, Misana Gamba alisema wapo timu ya maafisa kutoka makao makuu, Mkoa wa Singida na Manyara katika ziara ya kutoa elimu ya utunzaji wa miundombinu hususani ya msongo huo mkubwa wa umeme unaoanzia Singida, Babati Manyara, Namanga hadi Kenya baada ya kuona unaanza kuhujumiwa.
Alisema idara ya usalama Tanesco makao makuu kwa kushirikiana na idara ya miradi, ofisi ya uhusiano na mameneja wa mikoa wataendelea kutoa elimu maeneo mbalimbali ya shirika hilo ili kuzuia vitendo hivyo na kuwa kumekuwa na mafanikio makubwa kufuatia utoaji wa elimu hiyo kwani wananchi wamekuwa wakiuliza maswali mengi na kuahidi kutunza mradi huo.
Afisa Uhusiano na Huduma kwa Wateja Tanesco Mkoa wa Singida, Rehema Mwaipopo, alisema ni wajibu wa kila mwananchi unapopita mradi huo kulinda miundombinu ya njia ya umeme huo ambapo alitoa namba kwa ajili ya kupiga ili kuwataja watu watakao bainika wakihujumu mradi huo kuwa ni 0755873035 na 0714477445.5.