Na Mwandishi Wetu, Michuzi TV
MPANGO wa Kuendeleza Kampuni za Wajasiriamali Wadogo na wa Kati katika Soko la Hisa la Dar es Salaam(DSE), umezinduliwa rasmi leo Agosti 3,2021 huku ikielezwa kuwa lengo ni ikiwa ni matokeo chanya ya ushirikiano wa wadau katika sekta ya masoko ya mitaji.
Akizungumza leo Agosti 3,2021 wakati wa uzinduzi wa mpango huo mgeni rasmi Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA),CPA. Nicodemus Mkama,amesema hatua hiyo ni muhimu, kwani ina matokeo chanya katika ukuaji wa sekta binafsi; umma na uchumi wa nchi kwa ujumla. Hivyo basi, uzinduzi unachangia utekelezaji wa dhamira, malengo na azma ya Serikali ya kuweka mazingira wezeshi katika Kujenga Uchumi Shindani na Viwanda kwa Maendeleo ya Watu.
Aidha amesema uzinduzi huo ni matokeo ya utekelezaji wa mipango mikakati ya Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) na Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) yenye lengo la kuwawezesha wajasiriamali wadogo na wa kati kutumia fursa zilizopo katika masoko ya mitaji, ikiwa ni pamoja na kupata mitaji ya muda mrefu ya kugharamia miradi ya maendeleo.
“Hatua hii ni muhimu, kwani inatarajia kuongeza idadi ya wawekezaji katika masoko ya mitaji, na hivyo kuchangia utekelezaji wa Mpango Kabambe wa Taifa wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha,mkakati wa upatikanaji wa Rasilimali Fedha kwa Wajasiriamali Wadogo na wa Kati na Mpango Jumuishi wa Huduma za Kifedha hapa nchini,”amesema Mkama
MKama amesisitiza kuwa anayo furaha kuzindua Mpango wa Kuendeleza Kampuni za Wajasiriamali Wadogo na wa Kati kupitia Soko la Hisa la Dar Es Salaam ambapo kampuni nane zimekidhi vigezo vya mpango huo. Kampuni hizo ni Kampuni ya Selcom, Raha Beverage Company (RABEC), Victoria Finance,Finca Microfinance Bank,African Microfinance Ltd (AML); Techno Image; Reni the Wate Experts; na AKM Gilters Ltd.
Aidha amesema uwepo wa Mpango wa Kuendeleza Wajasiriamali Wadogo na wa Kati katika Soko la Hisa la Dar Es Salaam unatarajiwa kuleta matokeo chanya, ikiwa ni pamoja na kuwezesha kampuni ndogo na za kati za ujasiriamali kupata fursa ya kuonekana na wawekeza wa ndani na wa kimataifa.
Pia kuimarisha taswira za Kampuni Ndogo na za Kati za Ujasiriamali (Enhancing branding) na kuongeza fursa za Uwekezaji; Kuwezesha kujenga utamaduni wa uendeshaji kampuni kisasa zaidi ikiwa ni pamoja na kuimarisha utawala bora katika uendeshaji wa kampuni ndogo na za Kati za Ujasiriamali.
“Kuwezesha kampuni ndogo na za kati za ujasiriamali kutumia fursa za masoko ya mitaji, ikiwa ni pamoja na kupata rasilimali fedha kutoka kwa wawekezaji mbalimbali wa ndani na wa kimataifa; na Kuwezesha upatikanaji wa huduma za ushauri wa uwekezaji na usimamizi wa Rasilimali fedha,”amesema….
Ameongeza kupitia mpango huo wa kampuni ndogo na za Kati za Ujasiriamali zitaweza kupata rasilimali fedha kutoka kwa wawekezaji wa ndani na wa kimataifa,hivyo kuwezesha kampuni hizo kukidhi vigezo vya kuorodheshwa katika Soko la Hisa la Dar es Salaam.
Ametoa rai kwa Soko la Hisa la Dar es Salaam na wadau wote katika masoko ya mitaji kuhakikisha kuwa mpango huo unaleta tija na manufaa yakiwemo kuongeza hamasa kwa kampuni ndogo na za kati za ujasiriamali kutumia fursa zilizopo katika masoko ya mitaji, Kuwezesha Watanzania waliopo nje ya nchi kushiriki katika uwekezaji katika kampuni ndogo na za kati za ujasiriamali.
Pia kuongeza hamasa ya uwekezaji kwa kundi la vijana ambao ndio wengi katika jamii; na kuwezesha wawekezaji Malaika na Kampuni za Mitaji kuwekeza na hatimaye kuorodheshwa katika Soko la Hisa la Dar es Salaam.”Ili kufikia malengo hayo, ametoa mwito kwa Soko la Hisa la Dar es Salaam na kampuni zote zenye leseni kutoka Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana kuhamasisha matumizi ya mpango huo ikiwa ni pamoja na kuingiza elimu ya matumizi yake kwenye mipango yao ya kila mwaka ya elimu kwa umma.
Aidha Serikali kupitia Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana(CMSA) itaendelea kujenga mazingira wezeshi na shirikishi kwa lengo la kufikia azma hiyo kwa maendeleo ya masoko ya mitaji hivyo kuchochea ukuaji wa uchumi wetu hapa nchini.
“Mamlaka itaendelea kutekeleza mikakati ya kujenga masoko endelevu na yenye ufanisi, ikiwa ni pamoja na namna ambayo masoko ya mitaji yanavyotumika kupata fedha za kutekeleza miradi ya maendeleo na hivyo kuwezesha kuchochea ukuaji wa uchumi wa nchi yetu,”amesema.
Ametoa msisitizo kwa kwa Soko la Hisa, Taasisi zinazotoa huduma katika soko la hisa, na Wadau wa Sekta ya Masoko ya Mitaji kuwa Dunia hivi sasa ipo kwenye Mapinduzi ya Nne ya Viwanda yaani the Fourth Industrial Revoulution ambayo yanaongozwa na biashara za wajasiriamali wadogo na wa kati.
“Kwa mantiki hiyo, wadau wote wa sekta ya masoko ya mitaji wanapaswa kwenda na mwelekeo huo, ikiwa ni pamoja na kubuni bidhaa na huduma mpya hususan kwa Kampuni hizo,”amesisitiza.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA),CPA. Nicodemus Mkama akizindua mpango wa kuendeleza kampuni za Wajasiliamali Wadogo na wa Kati (SMES ACCELERATION PROGRAM – “MPANGO WA ENDELEZA”) Katika Soko la Hisa la Dar es Salaam leo jijini Dar,ambapo Waandishi wa habari pamoja na wageni waalikwa mbalimbali walihudhuria hafla hiyo
Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA),CPA. Nicodemus Mkama akizungumza jambo mbele ya Waandishi wa habari pamoja na wageni waalikwa mbalimbali kwenye uzinduzi wa mpango wa kuendeleza kampuni za Wajasiliamali Wadogo na wa Kati (SMES ACCELERATION PROGRAM – “MPANGO WA ENDELEZA”) Katika Soko la Hisa la Dar es Salaam leo jijini Dar.
Sehemu ya Meza kuu ikishuhudia baadhi ya makapuni nane yaliyofanikiwa kuingia kwenye mpango wa kuendeleza kampuni za Wajasiliamali Wadogo na wa Kati (SMES ACCELERATION PROGRAM – “MPANGO WA ENDELEZA”) Katika Soko la Hisa la Dar es Salaam leo jijini Dar.