********************************
Na. Damian Kunambi, Njombe.
Wakazi wa kata ya Ruhuhu wilayani Ludewa mkoani Njombe wameiomba serikali kuwakamilishia daraja la mto Ruhuhu sambamba na kuwatengenezea kivuko cha mto huo ili waweze kupata huduma ya afya kwa urahisi na kusafirishia mazao yao.
Wananchi hao wamedai kuwa awali walikuwa wanategemea pantoni ambayo kwa sasa imeharibika kwa takribani mwaka mmoja na kupelekea kuvusha mazao yao kwa kutumia ngalawa kitu ambacho kinahatarisha maisha yao.
Akiongea kwa uchungu Eksavel Ngatunga ambaye ni miongoni mwa wananchi hao amesema kuwa kuharibika kwa kivuko hicho kunawapa wakati mgumu kwani miaka yote wamekuwa wakitegemea kuuza mazao yao ya mpunga mkoani Ruvuma hivyo kwa sasa imewalazimu kuhifadhi ndani kwa kukosa soko.
Leah Haule naye ni mkazi wa kata hiyo ya Ruhuhu amesema wakazi wa eneo hilo wamekuwa wakitegemea kupata huduma ya afya katika hospital ya Peramiho iliyopo mkoani Ruvuma hivyo kwa sasa wamekuwa wakipata wakati mgumu wa kuwasafirisha wagonjwa kuwapeleka hospitalini hapo.
” Tunaiomba serikali itusaidie maana usafiri wa mitumbwi si mzuri kwakuwa muda mwingine mitumbwi hiyo inapinduka na kupelekea watu kutumbukia kwenye maji kitu ambacho ni hatari kwakuwa mto huo umezingira na mamba”, alisema Bi. Haule.
Aidha kwa upande wa mwenyeki wa serikali ya kijiji cha kipingu Alphonce Sembeya ameelekeza lawama zake kwa wakala wa ufundi na umeme (TEMESA) mkoa wa Ruvuma ambapo kivuko hicho kilipojaa maji ilibidi muendesha kivuko amtaarifu ili awape mafuta ya kukisogeza nchi kavu lakini hakufanya hivyo.
Amesema baada ya maji kupungua lililetwa scaveter kwaajili ya kukiondoa lakini ikashindikana kwakuwa kivuko hicho kilitobolewa na kivuko kingine ambacho kilizama miaka ya nyuma na kupelekea kunasa.
“Hali imekuwa ngumu kwa kiwango hiki kutokana na uzembe wa meneja wa TAMESA endapo angetekeleza ombi la muendesha kivuko tusingefika huku tulikofika sasa”, Alisema Sembeya.
Naye diwani wa kata ya Ruhuhu Athanas Haule amesema wananchi wa Ruhuhu na kata ya Manda shuguli zao nyingi ni za kutumia kivuko hicho hivyo kuharibika kwake limekuwa ni pigo kubwa sana kwao.
Amesema wanaomba serikali iwasaidie ufumbuzi wa muda mfupi na ule wa muda mrefu ambao ni kukamilisha daraja kwani toka mwaka 2016 mpaka sasa halieleweki hatima yake.
Joseph Kamonga ni mbunge wa jimbo la ludewa ambaye amefika katika eneo la kivuko hicho na kujionea changamoto wanazozipata wananchi hao na kudai kuwa amekuwa akipigiwa simu nyingi kutoka kwa wananchi juu ya changamoto hizo wanazozipitia.
Amesema tayari amesha chukua hatua za awali ambapo aliwasiliana na meneja wa TAMESA mkoa wa Ruvuma na kumuagiza kuja kukitoa kivuko hicho ili kiendelee kuwasaidia wananchi kwani haiwezekani kukiacha kivuko hicho kukaa katika hali hiyo ni kupoteza fedha ya serikali.
Sanjali na hilo pia amesema kuhusu ujenzi wa daraja hilo kabla ya mwaka huu kuisha litakuwa limekamilika kwani tayari vifaa vilivyokuwa vinasubiriwa vimeshawasili bandarini na sasa unafanyika utaratibu wa kuvisafirisha na kumalizia ujenzi huo.
“Niliongea na katibu mkuu na waziri wa ujenzi juu ya daraja hili wamesema ujenzi ulisimama kwakuwa kulikuwa na majadiliano juu ya kuweka zege au vyuma na hatimaye wamefikia muafaka wa kuweka vyuma kwakuwa muundo wa nguzo za daraja hili ni wa vyuma”, Alisema Kamonga.