********************************
Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kupitia Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) imezindua rasmi kifaa kitakachomsaidia Mwanafunzi asiyeona kusoma, kuandika na mchakato mzima wa ujifunzaji, ikishirikiana na Shirika lisilo la Kiserikali la Sense International Tanzania.
Kifaa hicho kinachoitwa Orbit Reader 20, kimezinduliwa leo tarehe 02/08/2021 Jijini Dar es Salaam.
Mgeni rasmi katika uzinduzi huo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia , Dkt. Caroline Nombo amesema watoto wenye mahitaji maalum wanakabiliwa na changamoto katika ujifunzaji, hivyo kupatikana kwa Orbit Reader 20 kutasaidia wanafunzi wasioona kukabiliana na changamoto hiyo.
Amesema wanafunzi wasioona katika shule mbalimbali hawapaswi kuachwa nyuma na teknolojia.
” Teknolojia haichagui, hivyo uzinduzi wa kifaa hiki kutawafanya wawe sambasamba na Teknolojia na kuleta matokeo chanya katika sekta ya Elimu,” amesema.
Aidha amewataka walimu 12 waliopatiwa mafunzo ya utumiaji wa Orbit Reader 20 wakawe chachu ya kuwafundisha walimu wengine.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa TET, Dkt. Aneth Komba amesema Sense International Tanzania kwa kushirikiana na TET wamechagua shule mbili za Msingi na nne za Sekondari kwa ajili ya kufanya majaribio.
Alisema wanafunzi wasioona wa darasa la 4, 5 na 6 katika shule za Msingi pamoja na wanafunzi wa kidato cha 1,2 na 3 watapatiwa Orbit Reader 20 ili wazitumie katika kuandika, kusoma na kuwasiliana na hata walimu wasioweza kusoma maandishi ya breli.
Dkt. Aneth amezitaja shule zitakazoshiriki katika mradi huu kuwa ni Shule ya Msingi Uhuru Mchanganyiko iliyopo Ilala, Shule ya Msingi Toangoma, Shule za Sekondari Mpwapwa, Kilosa, Lugoba, na Haile Selasie ya Zanzibar.
Kila shule iliyopo katika mradi huu itapatiwa Orbit 20 moja kwa kila mwanafunzi, alisema.
Pia amesema, shule hizi zitatembelewa na wataalamu wa shirika la Sense International Tanzania na TET kuanzia mwezi huu Agosti hadi Desemba, 2021 ili kutathmini utumiaji wa vifaa hivi saidizi shuleni.
Taarifa kamili ya tathmini inatarajiwa kuwa tayari mwishoni wa mwezi Desemba, 2021 Mkurugenzi huyo alisema; ambapo TET itazishauri Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali ya Zanzibar njia bora ya kutumia kifaa hiki saidizi shuleni.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi wa Sense International Tanzania, Bi. Naomi Lugowe amesema kila mtu mwenye ulemavu anaweza kupata nafasi ya kujifunza na kuishi kama watu wengine.
Amesema kwa sasa wanafunzi wasioona wanatumia maandishi ya nukta nundu (Parkins Breli) kujifunzia ambapo kifaa hiki gharama yake ni kubwa hasa katika utunzaji wake.
“Orbit Reader 20 ni kifaa chenye gharama nafuu mara mbili ya mashine ya nukta nundu, ina ukubwa wa GB 32 wa kuhifadhi kumbukumbuku,” amesema Bi. Naomi.
Aidha, amesema kifaa hiki kitasaidia kupunguza gharama za uchapaji wa vitabu vya nukta nundu.
Sense International imetoa jumla ya Orbit Reader 87 kwa shule sita hizo za Tanzania Bara na Zanzibar zitakazofanyiwa ujaribishaji.