******************************
Na Mathew Kwembe, Dodoma
Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa TAMISEMI Prof.Riziki Shemdoe ameipongeza timu ya netiboli ya TAMISEMI Queens kwa kushika nafasi ya pili katika michuano ya Klabu bingwa ya netiboli iliyomalizika mwishoni mwa wiki katika uwanja wa sheikh Amri Abeid jijini Arusha.
Akipokea zawadi ya kikombe cha mshindi wa pili wa klabu bingwa ya netiboli nchini pamoja na vikombe vya mchezaji bora wa mashindano hayo (MVP), mchezaji bora wa kati na mfungaji bora wa mashindano hayo leo ofisini kwake jijini Dodoma, Katibu Mkuu amesema kazi waliyoifanya wachezaji wa timu hiyo siyo ndogo hasa kwa kuzitoa jasho timu za majeshi ambazo hushiriki mashindano hayo kwa wingi na mara kwa mara.
Amesema kutokana na timu hiyo kuiletea heshima kubwa ofisi ya Rais TAMISEMI kila mchezaji wa timu hiyo atapewa shilingi laki tano kama zawadi na kutambua mchango wake katika timu hiyo.
“Kwa kazi nzuri mliyoifanya na kwa sababu ndiyo kwanza tunaanza mwaka wa fedha, wote mtapata kifuta jasho cha shilingi laki tano tano, “alisema Katibu Mkuu.
Mbali na kutoa fedha taslim kwa wachezaji kama motisha, Katibu Mkuu pia ameahidi kuipa kila aina ya ushirikiano timu ya TAMISEMI QUEENS kwenye maandalizi yake ya kushiriki mashindano ya ligi ya muungano ya netiboli ambayo itafanyika huko Zanzibar baadaye mwaka huu.
Pia timu hiyo inatarajia kushiriki ligi ya netiboli kwa nchi za Afrika Mashariki ambapo TAMISEMI QUEENS ikiwa mshindi wa pili itaungana na timu za JKT Mbweni na Magereza Morogoro kushiriki mashindano hayo.
Katika hafla hiyo ambayo pia ilihudhuriwa na Naibu Katibu Mkuu TAMISEMI anayeshughulikia Afya Dkt Grace Maghembe, Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali watu, Victor Kategere na viongozi wengine waandamizi kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI.
Mapema Mwenyekiti wa Klabu ya Michezo ya TAMISEMI Philbert Rwakilomba alimweleza Katibu Mkuu kuwa licha ya kuwa washindi wa pili timu yetu ilijizolea zawadi kwa wachezaji wetu watatu kati ya wanne bora kuchaguliwa kushinda tuzo za mchezaji bora wa mashindano (MVP), mchezaji bora wa kati na mfungaji bora wa mashindano.
Tuzo ya Mfungaji bora wa mashindano ilichukuliwa na Lilian Jovin, Mchezaji bora wa kati ilichukuliwa na Sophia Komba, na Mchezaji bora wa mashindano ya klabu bingwa netiboli mwaka huu ilichukuliwa na Merciana Kizenga wote kutoka timu ya TAMISEMI QUEENS.
Kwa upande wake nahodha wa TAMISEMI QUEENS Sophia Komba amesema licha ya waamuzi kuibeba JKT Mbweni anaamini timu yake ina uwezo wa kuchukua kombe la ligi ya Muungano na kombe la Afrika Mashariki kwani wachezaji wa timu yake wameonyesha uwezo mkubwa katika michuano hiyo.
Naye Kocha wa timu hiyo Maimuna Kitete pamoja na kuahidi kupambana zaidi ili kuleta vikombe zaidi katika michuano inayokuja, amewasifu wachezaji wake kwa kucheza kwa kujituma na kufanya mazoezi na kudumisha nidhamu katika timu.
Timu ya Netiboli ya TAMISEMI QUEENS ilipanda ligi daraja la kwanza ya netiboli Taifa mwaka 2018 katika mashindano yaliyofanyika Mtwara na Mwaka 2019, timu hiyo ilishiriki Ligi daraja la kwanza ngazi ya Taifa na kushika nafasi ya nne.
Nafasi hiyo iliiwezesha timu hiyo kushiriki Ligi ya Netiboli ya Muungano inayoshirikisha timu sita za bara na timu sita za Muungano.
Katika Mashindano ya Ligi ya Muungano, TAMISEMI QUEENS ilifanikiwa kuzishinda timu zote zilizoshiriki ligi hiyo na kuwa Mabingwa wa Kombe la Muungano mwaka 2019.
CAPTION
Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI Prof.Riziki Shemdoe (aliyeshika kikombe katikati) akiwa katika picha ya pamoja na viongozi na wachezaji wa timu iliyoshika nafasi ya pili michuano ya klabu bingwa netiboli nchini, mashindano yaliyomalizika mwishoni mwa wiki jijini Arusha.
Nahodha wa TAMISEMI QUEENS Dafrosa Luhwago (kulia) akimkabidhi kombe la mshindi wa pili Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI Prof Riziki Shemdoe katika sherehe fupi zilizofanyika katika ofisi yake iliyopo Mtumba jijini Dodoma leo
Mfungaji bora wa mashindano ya klabu bingwa ya netiboli nchini Lilian Jovin wa TAMISEMI QUEENS akimkabidhi Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI Prof Riziki Shemdoe tuzo ya kikombe aliyoipata katika mashindano hayo yaliyomalizika mwishoni mwa wiki jijini nArusha
Mchezaji bora wa kati wa mashindano ya klabu bingwa ya netiboli Sophia Komba kutoka TAMISEMI QUEENS akimkabidhi Katibu Mkuu Prof Shemdoe tuzo ya kikombe aliyoipata katika mashindano hayo yaliyomalizika mwishoni mwa wiki jijini nArusha