Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza wakati alipozindua Mafunzo ya Uanagenzi Awamu ya Tatu kwenye kiwanja cha Chuo Kikuu cha Sayansi na Tekinolojia Mbeya, Agosti 2, 2021. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Tixon Nzunda akizungumza katika uzinduzi Mafunzo ya Uanagenzi Awamu ya Tatu kwenye kiwanja cha Chuo Kikuu cha Sayansi na Tekinolojia Mbeya, Agosti 2, 2021. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitembelea maonesho wakati alipozindua Mafunzo ya Uanagenzi Awamu ya Tatu kwenye kiwanja cha Chuo Kikuu cha Sayansi na Tekinolojia Mbeya, Agosti 2, 2021. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimsikiliza Rozalia John wakati alipozindua Mafunzo ya Uanagenzi Awamu ya Tatu kwenye kiwanja cha Chuo Kikuu cha Sayansi na Tekinolojia Mbeya, Agosti 2, 2021. Katikati ni Waziri wa Elimu, Sayansi na Tekinolojia, Profesa, Joyce Ndalichako (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
******************************
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali imetenga sh. bilioni tisa kwa ajili ya kugharamia mafunzo ya uanagenzi kwa vijana ambao hawakubahatika kupata nafasi kwa sasa.
“Vijana ambao hawakubahatika kupata nafasi ya kushiriki mafunzo kwa awamu hii wawe na subirá kwani tunaendelea kuandaa fursa hizi kupitia vituo vingine na tutatangaza tena.”
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumatatu, Agosti 2, 2021) wakati akizindua awamu ya tatu ya mafunzo ya stadi za kazi kwa njia na uanagenzi kwa vijana 14,440. Uzinduzi huo umefanyika jijini Mbeya.
Mheshimiwa Majaliwa amewataka vijana hao walioanza mafunzo watambue kwamba fursa hiyo waliyopata ni adimu sana na wanapaswa kuithamini na kuitumia kama ilivyokusudiwa.
“Nendeni mkajifunze kwa bidii, muwe na nidhamu kwa wote kwani bidii yenu kwenye kujifunza ni ufunguo wa kupata maarifa yatakayowawezesha kufanya kazi kwa weledi baada ya kuhitimu.”
Ametoa wito kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa zihakikishe vijana hao wanawaunganisha kwenye vikundi vya ushirika na kuwapatia mikopo ili wapate nyenzo za kufanyia kazi.
“Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa wote simamieni kwa karibu suala hili ili kuwawezesha vijana kiuchumi kwa kushiriki kikamilifu katika kujenga nchi yetu badala ya kuwa watazamaji.”
“…Vyuo vyote vinavyotoa mafunzo haya pia wafundishe vijana hawa mafunzo ya ushirika na biashara ili wafanye kazi kwa misingi ya biashara na hivyo kuwawezesha kurasimisha kazi zao.
“Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan imeamua kuimarisha Programu ya Taifa ya Kukuza Ujuzi kwa kuongeza idadi ya wanufaika.”
Amesema kutokana na umuhimu wa mafunzo hayo Serikali imeongeza vituo vya mafunzo kutoka 13 vya awali na kufikia vituo 72 vilivyoenea katika mikoa yote ya Tanzania Bara.
Waziri Mkuu amesema mbali na kuongezeka kwa vituo pia idadi ya wanafunzi imeongezeka kutoka 5,875 hadi kufikia vijana 14,440 wanapatiwa mafunzo hayo kwa gharama ya Serikali.
Waziri Mkuu amesema mafunzo hayo aliyoyazindua leo yanatarajiwa kukamilika mwezi Desemba 2021 na yatafanya jumla ya vijana walionufaika na programu hiyo kufikia 80,038.
Naye, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Jenista Mhagama amesema mafunzo yameandaliwa kimkakati ili kufungua fursa za vijana.
Waziri Mhagama amesema mafunzo hayo yamezingatia soko na fursa zilizopo na kuwajenga uwezo wa kujiamini na kujiajiri na kuhamasisha ushindani katika soko la ajira.
Kadhalika, Waziri Mhagama amesema asilimia 60 ya mafuzo hayo itatolewa kwa njia ya vitendo na asilimia 40 ni mafunzo ya nadharia darasani kulinga na aina ya fani.