Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa ameendelea na ziara zake za kikazi Mkoani Mbeya ambapo leo August 2, 2021 amezindua mafunzo ya Uanagenzi katika Chuo Kikuu cha Sayansi (MUST) kilichopo Jijini Mbeya.
Katika ziara hiyo Waziri Mkuu Majaliwa amepata nafasi ya kupewa taarifa za maendeleo na changamoto za Jiji la Mbeya kupitia kwa Mbunge wa Jimbo hilo ambaye pia ni Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Tulia Ackson.
Dkt. Tulia amesema”Mheshimiwa Waziri Mkuu tunakuomba utupelekee salamu na shukrani kwa Rais wetu Samia Suluhu kwa kutusaidia zaidi ya Shilingi bilioni mbili kwa ajili ya Ujenzi wa barabara za mchepuko katika Jiji letu lakini sasa tunatamani na ujenzi wa barabara kuu ya Uyole-Tunduma km 104, Uyole-Igawa km 116 ianze kwamaana barabara yetu ni finyu na tunahitaji sana msaada wake”
“Mbeya Mjini tuna mitaa 181 na asilimia zaidi ya 97 ya barabara hizo zimejaa vumbi na mimi kama Mbunge wa Jimbo hili kwakweli naomba tukumbukwe kwenye barabara za lami kwasababu sisi hatuna tofauti na majiji mengine, Jiji hili limeongoza kwa makusanyo kwa 102% hivyo hakuna sababu ya Jiji hili kuwa nyuma kwa maendeleo ya barabara”- Dkt. Tulia Ackson
“Mheshimiwa Waziri Mkuu, Pamoja na hizo changamoto za miundombinu tunaomba utupelekee shukrani kwa Rais wetu kwenye eneo la afya tumeshaletewa zaidi ya Shilingi bilioni moja kwenye kituo chetu cha Afya Igawilo kwa ajili ya kubadilisha iwe hospitali ya Wilaya, tumeletewa kwenye kata ya Iyela Milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha Afya lakini Mheshimiwa Waziri Mkuu, hapa Mbeya Mjini tuna kata 36 lakini vituo vya Aafya havifiki 10 na Zahanati hazizidi 15 kiukweli hali yetu sio nzuri tunakuomba leo useme neno utatuongezea vituo vingapi vya afya? ”- Dkt. Tulia Ackson
“Eneo la Elimu tumetengewa zaidi million 600 kwa ajili ya shule moja ya Sekondari ambayo itakamilika kabisa, kama nilivyosema tuna kata 36 na zaidi ya kata 10 hazina Shule za Sekondari watoto wanatembea mwendo mrefu, Mheshimiwa Waziri Mkuu leo tunakuomba utuambie katika kata hizo utatusaidia shule ngapi za sekondari?”- Dkt. Tulia Ackson
“Suala la Umeme utupelekee shukrani kwa Rais kwa kutusaidia sisi Wananchi wote hata tuliopo mjini kulipia Tsh: 27,000/- pekee kwa ajili ya kuunganishiwa lakini tunaomba yule mkandarasi aliyepewa kazi ya kusambaza umeme aongeze kasi ya usambazaji ili sisi wote tuwe na umeme”- Dkt. Tulia Ackson
“Mheshimiwa Waziri Mkuu, Kuhusu Maji tumetengewa zaidi ya bilioni mbili kwa ajili ya mradi wetu mkubwa wa Kiwira, mradi ule unaenda kumaliza tatizo la maji Mbeya mjini na mikoa jirani. Mheshimiwa Waziri Mkuu mradi huu unahitaji fedha nyingi bilioni mbili naamini ni kianzio hivyo pamoja na shukrani tunaomba utupelekee hiki kilio kwamba Mbeya Mjini maji bado hayatutoshi hivyo tungetamani mradi huu kukamilika kwa wakati”-Dkt. Tulia Ackson
“Mwisho, Vijana hawa ambao wamejifunza hapa tumesikia mengi waliokuwa wameomba mafunzo ni wengi na hapa Mbeya Mjini hata kwa idadi ya watu ni wengi tofauti na maeneo mengine hapa Mbeya hivyo tungeomba sana awamu inayokuja ya mafunzo kwa upekee tuongezewe idadi ya maombi ya wanafunzi na kwakuwa umeelekeza kwamba kila Halmashauri kutoa vipaumbele vya mikopo kwa Vijana wenye ujuzi tunakuahidi hapa Mbeya Mjini tutakuwa mfano wa kuwawezesha Vijana na uwezo huo tunao”- Dkt. Tulia Ackson