********************************
Na Selemani Msuya
TAASISI ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT), imesema katika kuhakikisha wanafunzi wanaohitimu chuoni hapo wanapata kazi kwa urahisi, watakuwa wanawapatia mafunzo ya kuandika wasifu, kujieleza kwenye usahili na kujiajiri kabla hawajamaliza masomo.
Hayo yamesemwa na Mshauri wa Wanafunzi DIT, Yosiah Misago wakati akifungua warsha ya siku moja kwa wanafunzi hao kuhusu namna ya kuandika wasifu, barua ya kuomba kazi na kujibu maswali wakati wa usahili iliyotolewa chuoni hapo mwisho wa wiki jana.
Misago alisema DIT ni moja ya taasisi ambayo inazalisha wataalam wa aina mbalimbali katika masuala ya sayansi hivyo imeona ni muhimu kuwajengea uwezo wataalam hao wakati wakielekea kwenye ajira wakiwa na uelewa mzuri wa mchakato mzima wa kupata kazi.
“Moja ya changamoto ya vijana wengi ambapo wanamaliza mafunzo katika taasisi nyingi ni namna ya kuandika wasifu, kujieleza wakati wa usahili na kuandika barua hivyo kupitia mafunzo haya ambayo tunatoa leo hapa chuoni naamini tutakuwa tumewafungua na kuona fursa,” alisema.
Alisema DIT inaamini katika dhana ya mafunzo kwa vitendo hivyo ni wazi ujio wa mafunzo hayo ya kujiandaa na ajira ni msingi mzuri ambao utawawezesaha vijana wanahitimu kuajirika,” aliongeza.
Kwa pande wake Rais wa Wanafunzi wa chuo hicho, William Kajumba alisema mafunzo hayo ni muhimu na nayapaswa kuwa endelevu ili kuwajenga uwezo na ujasiri wahitimu.
Akitoa mafunzo kuhusu namna ya kuandika wasifu, kujielezea na barua za kuomba kazi Mkufunzi Juliana Peter kutoka Niajiri Platform aliwataka wanafunzo hao kuhakikisha watengeneza wasifu kabla ya kumaliza ili kuwa rahisi kuingia katika soko la ajira.
Peter alisema moja ya changamoto ambayo inakabili vijana wengi nchini baada ya kumaliza chuo ni kuajirika lakini changamoto inaanzia kwenye kuandaa wasifu, kujieleza na barua hivyo wanapasa kubadilika.
“Niseme kweli kuwa changamoto ambayo tunakutana nayo ni maandalizi ya wasifu, kujieleza na nyingine vnyingi kwa wahitimu hali ambayo inachangia wengi wao kutumia muda mwingi kutafuta kazi bila mafanikio.
Pia wahitimu wengi hawatengenezi wasifu kuanzia chuoni jambo ambalo linasababisha wakati wa usahili kukosa sifa,”alisema.
Mkufunzi huyo alitoa kwa wahitimu ambao watakutana na changamoto ya kukosa ajira kuwa na utamaduni wa kujitolea ili kutengeneza wasifu wao.
Naye Mwanasaikolojia Saldin Kimangale, alisema pamoja na changamoto za kuandika wasifu na nyingine pia wahitimu wengi wanakabiliwa na changamoto ya kushindwa kuendeleza malengo yao.
Kimangale alisema watu ambao wamefanikiwa duniani kote wameweza kusimama na wazo lao hivyo amewataka wahitimu hao wa DIT kusimama kwenye jambo ambalo wanaona wanatosha kwani katika kujaribu hakuna kitu cha sawasawa kwa asilimia 100.
“Ila nimalizie kwa kuwaambia kuwa njia ya kujitolea ni muhimu kwa yoyote ambaye anahitaji ajira, pia usikate tamaa kwa hoja ya kufeli kwa kuwa kwenye kufeli ndipo watu wanajifunza,” alisema.