Mwenyekiti cha chama cha Mapinduzi CCM Mkoa wa Morogoro Dorothy Mwamsiku amewataka viongozi wa chama hicho kuanzia ngazi ya shina hadi mkoa kuacha tabia ya kuwanyooshea vidole na kulumbana na watendaji wa Serikali wakiwemo wakurugenzi badala yake wasimamie utekelezaji wa ilani ya CCM.
Mwamsiku alitoa wito huo jana wilayani Kilosa wakati akifungua mkutano wa Halmashauri kuu ya CCM mkoa ambapo alisema kuwa ili nchi iweze kupiga hatua katika maendeleo lazima viongozi wa chama washirikiane na watendaji wa Serikali na sio kurumbana na kutunishiana misuli.
“Sisi sote ni viongozi na tunayo dhamana ya kusimamia maendeleo, tofauti kati ya viongozi wa siasa na watendaji ni kwamba sisi wanasiasa tumechaguliwa na wananchi na tunakaa madarakani kwa miaka mitano, wao wenzetu watendaji wameteuliwa na Rais ambaye ndiye mwenyekiti wa chama cha mapinduzi na muda wao wa kukaa madarakani utategemea na namna ambavyo Rais itampendeza, naomba tujishushe kwenye utendaji wetu,” alisema Mwamsiku.
Hata hivyo aliwataka watendaji wa Serikali kuwaheshimu viongozi wa CCM kwa nafasi zao kama ambavyo viongozi hao wanavyowaheshimu watendaji wa Serikali kwa nafasi zao pamoja na kuwasisitiza watendaji hao kutambua viongozi wa CCM wanayohaki ya kufuatilia, kuhoji na kusimamia miradi ya kimkakati na miradi mingine ya maendeleo pamoja na utekelezaji wa ilani ya chama.
“Tunajenga nyumba moja haina sababu ya kugombea fito, lazima tupendane na kila mmoja wetu aheshimu mamlaka ya mwenzake, miongonmi mwetu hakuna aliyrebora kuliko mwenzake wote tupo katika kuhakikisha nchi inasonga mbele,” alisema Mwamsiku.
Alisema kuwa katika kipindi chake cha uongozi na katika utendaji kazi wake hatabagua viongozi wa chama wala watendaji wa serikali na kwamba yupo tayari kupokea mawazo na ushauri wowote kwa maslahi mapana ya nchi, chama na wananchi kwa ujumla.
Katika hatua nyingine Mwamsiku aliwataka wanachama wa CCM kuvunja makundi yanayotokana na chaguzi mbalimbali ukiwemo uchaguzi uliomalizika hivi karibuni wa kumchagua mwenyekiti wa CCM ambao katika uchaguzi huo yeye alichaguliwa kuwa mwenyekiti wa CCM mkoa wa Morogoro.
Alisema kuwa kila kiongozi anayeingia madarakani ana misingi na mfumo wake wa uongozi hivyo yeye kama mwenyekiti wa CCM mkoa misingi yake ya uongozi ni kuimarisha umoja, mshikamano, upendo na amani.
“Kama wewe ulikuwa meneja kampeni wangu basi fahamu kuwa baada ya uchaguzi nimekutapika na nakuhesabu kama mwanaCCM, na kama wewe hukuniunga mkono na hukuwa miongoni mwa walioniunga mkono basi sasa hivi nitakukumbatia na kukuvuta tukijenge chama, nisingeitwa mshindi kama pasingetokea wanaonipinga,” alisema Mwamsiku.
Awali akitoa taarifa ya utekelezaji wa miradi ya kimkakati mkuu wa mkoa wa Morogoro Martine Shigela alisema kuwa uongozi wa mkoa uko tayari kushirikiana na viongozi wa CCM katika kusimamia na kulinda miradi yote ya kimkakati ikiwemo reli ya kisasa ya SGR, bwawa la kuzalisha umeme la Mwalimu Nyerere.
Vile vile Shigela ambaye ni mjumbe katika kikao hicho cha Halmashauri kuu ya CCM mkoa alitoa ufafanuzi kuhusu mashamba pori 11 yaliyofutwa na Rais Samia Suluhu Hassan hivi karibuni ambapo alisema kuwa mashamba hayo yapo kwenye mchakato wa kugaiwa wananchi.
Aliwataja watakaonufaika na mashamba hayo kuwa ni pamoja na wananchi ambao hawana ardhi kwa ajili ya kilimo, wafugaji ambao hawana maeneo ya ufugaji na wanaohamahama lakini pia wawekezaji ambao watakidhi vigezo na masharti.
Baadhi ya hoja zilizoulizwa na wajumbe wa mkutano huo ni pamoja na mradi wa umeme wa Rea ambapo walitaka kujua mradi huo umefikia wapi hasa katika baadhi maeneo ya vijijini ambayo bado hayajafikiwa na mradi huo na pia suala la tembo kuingia kwenye makazi ya watu na mashamba na kusababisha madhara vikiwemo vifo na uharibifu wa mazao.
Hoja nyingine ni ujenzi wa barabara ya Ludewa-Kilosa hadi Mikumi yenye urefu wa kilometa 24 ya kiwango cha rami ambapo kaimu meneja wa Tanroad mkoa wa Morogoro mhandisi Baraka Mwambage alisema kuwa tayari kilometa 10 za barabara hiyo zimeshakamilika kwa kiwango cha rami na kwamba kwa ujumla ujenzi wa barabara hiyo umefikia asilimia 73.
Mhandisi Mwambage alisema kuwa ujenzi huo unatarajia kugharimu zaidi ya Sh. 32.9 bilioni hata hivyo mpaka sasa tayari fedha zaidi ya Sh. 16.6 bilioni zimeshatolewa kwa ajili ya ujenzi huo.