Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni,Sanaa na Michezo. Mhe, Gekul akitoa neno kwa wachezaji timu ya JKT Mbweni na TAMISEMI katika fainali mashindano ya Netiboli Ligi Daraja la Kwanza katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid Arusha leo. Katika mashindano haya JKT Mbeni ndiyo wameibuka washindi wa jumla wa mwaka 2021 kwa kuwabwaga timu ya TAMISEMI kwa magoli 40 kwa 39.
Mhe.Gekul akigagua Timu ya JKT Mbweni na TAMISEMI katika fainali mashindano ya Netiboli Ligi Daraja la Kwanza katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid Arusha leo. Katika mashindano haya JKT Mbeni ndiyo wameibuka washindi wa jumla wa mwaka 2021 kwa kuwabwaga timu ya TAMISEMI kwa magoli 40 kwa 39.
Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo. Mhe, Gekul akimkabidhi Kombe na Cheti, Mericiana Kizinga ambaye ni mchezaji bora wa mwaka 2021 kutoka timu ya TAMISEMI katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid Arusha leo. Katika mashindano haya JKT Mbeni ndiyo wameibuka washindi wa jumla wa mwaka 2021 kwa kuwabwaga timu ya TAMISEMI kwa magoli 40 kwa 39. Picha na John Mapepele-WHUSM.
……………………………………………………………….
Na John Mapepele, Arusha
Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Pauline Gekul (Mb.), amesema kuanzia mwaka huu Serikali itaanza kusaidia Mashirikisho na Vyama vya Michezo hapa nchini kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Michezo ili Tanzania iweze kufanya vizuri katika michezo ya kimataifa.
Mhe.Gekul ameyasema haya wakati akifunga mashindano ya Netiboli ligi daraja la kwanza katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid Arusha leo ambapo amesisitiza kuwa kupitia bajeti ya mwaka huu wa fedha (2021-2022) Wizara imejipanga vyema kupitia mfuko huo kuzisimamia timu za Taifa na kuziwezesha kushiriki mashindano mbalimbali ya Kimataifa.
Katika mashindano haya timu ya JKT Mbweni ndiyo wameibuka washindi wa jumla wa mwaka 2021 kwa kuibwaga timu ya TAMISEMI, Dodoma kwa magoli 40 kwa 39 ambapo timu ya Netiboli ya wanaume ya Smart kutoka Dar es Salaam ndiyo wameibuka washindi.
“Natambua kuwepo kwa changamoto mbalimbali juu ya mchezo huu wa Netiboli ikiwemo kukosa Mlezi pamoja na Wafadhili. Hata hivyo tunawapongeza viongozi wa Chama kwa kuendelea kufanya kazi kwa juhudi na maarifa” Ameongeza Mhe. Naibu Waziri
Aidha amesema, Wizara kupitia Idara ya Maendeleo ya Michezo ipo katika hatua za mwisho za kukamilisha Mpango Mkakati wa Maendeleo ya Michezo, mpango ambao utasaidia kusukuma mbele maendeleo ya michezo hapa nchini ikiwemo mchezo wa Netiboli.
Amewataka viongozi wa vyama vya Michezo na Mashirikisho yote nchini kujipanga vyema katika kutekeleza Mpango huu.
Amesema mwaka huu Wizara yake inaandaa Tamasha la Wanawake litakalokuwa kubwa na la aina yake ili kuleta hamasa kwenye michezo ya wanawake.
Amemshukuru Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan, kwa kunipa jukumu la kushirikiana na viongozi wenzake katika kuisimamia michezo hususan michezo ya wanawake.
Amewapongeza viongozi wa Chama cha Netiboli Tanzania na vilabu vyote vilivyoshiriki katika mashindano haya.
“Nazipongeza timu zote zilizoshiriki na wale wote waliofanikiwa kuibuka na ushindi kwa pande zote mbli za Wanawake na Wanaume”. Amefafanua Mhe. Gekul
Amesema kupitia mashindano hayo ana imani watapatikana wachezaji wazuri, chipukizi na mahiri watakao saidia kuunda Timu ya Taifa itakayoshiriki mashindano mbalimbali na kuliwakilisha Taifa letu Kimataifa.
Pia ameupongeza Uongozi wa Chama cha Netiboli Tanzania (CHANETA) kwa kuweza kuifuata kalenda yao ya mwaka na kuendesha mashindano, kozi na majukumu yao yote na kuwaomba wadau wengine wa Michezo kujitokeza kudhamini Mashindano haya ili kuendelea kuibua vipaji vya vijana.
Ametoa mwezi mmoja kwa mikoa yote kuikamilisha uchaguzi wa viongozi wa CHANETA na baada ya hapo uchaguzi mkuu wa kitaifa ufanyike mara moja kwa kuwa hadi sasa ni mikoa minne tu ndiyo imekamilisha zoezi hili.
Kwa upande mwingine Mhe. Gekul ametoa wito kwa wana michezo wote kuzingatia njia mbalimbali za kujikinga na Ugonjwa wa UVIKO-19 ambapo amezitaka Wilaya zote nchini kuanzisha klabu za riadha kwa kuwa michezo inajenga afya, pia ametoa wito kwa Makatibu Tawala wa mikoa yote nchini kusimamia michezo na miundombinu ya michezo katika mikoa yao
Naye mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Arusha ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Arusha Mhe. Sophia Mjema amemshukuru Mhe. Gekul na kuiomba Serikali ifikilie kuturejesha mashindano haya mwakani mkoani Arusha ili kuendelea kuleta hamasa kwa wananchi wa mikoa ya kaskazini mwa Tanzania.