Mbunge wa Jimbo la Mlimba Morogoro, Godwin Kunambi (wa pili kutoka kushoto) akiwa kwenye Mtumbwi akivuka Mto Mngeta Februari mwaka huu ambapo aliitembelea Mto huo ukiwa hauna kivuko
Mbunge Jimbo la Mlimba Morogoro, Godwin Kunambi akipita juu ya daraja la muda ambalo amefanikisha ujenzi wake. Daraja hili litakua na uwezo wa kupitisha Tani 10 na litadumu kwa muda wa miaka 10 hadi 15.
……………………………………………………………
SIKU Moja baada ya Mbunge wa Jimbo la Mlimba Mkoani Morogoro,Godwin Kunambi kutembelea Daraja la Mto Mngeta lililogharimu Sh Milioni 30 hatimaye Meneja wa Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA), Wilaya ya Kilombero ametolea ufafanuzi gharama za ujenzi huo.
Mhandisi Robert Magogo ambaye ni Meneja wa TARURA Wilaya ya Kilombero ametolea ufafanuzi wa Ujenzi wa mradi huo akisema gharama zilizotajwa ni sahihi huku akieleza kuwa lina uwezo wa kudumu kwa miaka 10 hadi 15.
Akifafanua ujenzi wa daraja hilo, Mhandisi Magogo amesema Daraja hilo lina urefu wa Mita 40, kina cha Mto kikiwa ni Mita 4, upana wake Mita 5 na hivyo kufanya gharama za Daraja kuwa Milioni 27.
Mhandisi Magogo ameeleza kuwa gharama ya barabara kuingia na kutoka darajani ni Sh Milioni 4 na kufanya jumla yake iwe Sh Milioni 31.
” Urefu wa wa nguzo zilizotumika ni Mita 7 na unene wake ni Mita 0.5, Mbao ni Inchi 3 kwa 8 na Inchi 3 kwa 10 na aina ya Mti ambao Mbao zake zimetumika ni za Mti aina ya Mkarati, niwahakikishie kuwa daraja hili ni imara na litakua na uwezo wa kupitisha Tani 10 na litadumu kwa miaka 10 hadi 15,” Amesema Magogo.
Kwa upande wake Mbunge Kunambi amesema Daraja hilo litaokoa uhai wa wananchi ambao kwa muda mrefu wamekua wakipata changamoto ya kivuko kwani Mto huu una mamba ambao wamekua wakisababisha Vifo vya wananchi wetu,” Amesema Kunambi.