Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhe. Joseph Joseph Mkirikiti akiongea na wafanyabiashara wa soko dogo la kijiji cha Ntendo Manispaa ya Sumbawanga ambapo ameagiza wawekewe mazingira mazuri ikiwemo paa na vibanda kujikinga na jua pia mvua.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti akikagua mlango wa chuma cha darasa wakati alipotembelea shule ya sekondari Sumbawanga. Amepongeza Jeshi la Magereza kwa kazi nzuri ya ujenzi . Kulia kwake ni Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Sebastian Waryuba na kushoto ni Mkurugenzi wa Manispaa ya Sumbawanga Jacob Mtalitinya.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Sumbawanga Jacob Mtalitinya (kulia) akitoa maelezo ya mradi wa ujenzi wa shule mpya ya msingi Ntendo B kwa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Joseph Mkirikiti (kushoto aliyevaa suti nyeusi) leo wakati wa ziara ya Mkuu huyo wa Mkoa kukagua miradi ya maendeleo.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhe. Joseph Joseph Mkirikiti (kulia) akitoa maelekezo kwa Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Mhe. Sebastian Waryuba (kushoto) kuhusu kuhakikisha miradi ya ujenzi wa madarasa kwa shule na zahanati yakamilike kabla ya mwezi Octoba mwaka huu wakati alipozunumza na wananchi wa kijiji cha Ntendo Manispaa ya Sumbawanga.
********************************
Wanachi wa kijiji cha Ntendo Manispaa ya Sumbawanga wameiomba serikali kusaidia kupatikana kwa soko la mazao yao ikiwemo mahindi ili waweze kupata fedha za kuchangia shughuli za maendeleo ikiwemo ujenzi wa zahanati na madarasa ya shule.
Wametoa maombi hayo leo (29.07.2021) kwa nyakati tofauti wakati wakiongea na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti alipotembelea kijiji hicho kukagua mradi wa ujenzi wa shule mpya ya msingi ya Ntendo B ambapo ilianza kujengwa mwaka 2018.
“Kero tuliyonayo hapa Ntendo ni soko la mazao sasa mahindi tunauza kwa bei ya chini ambapo sado moja inauzwa shilingi 800. Mimi mwaka huu nimepata gunia 40 na sasa nimeshindwa kuuza, yapo tu nyumbani. Serikali itusaidie” alisema mkazi wa Ntendo James Zumba kwenye mkutano huo.
Eliza Kachele alisema kero nyingine ya kijiji cha Ntendo ni mrundikanao wa wanafunzi kwenye shule ya msingi ambapo inasababisha wanafunzi kutosoma vizuri hivyo ameitaka Serikali kutoa fedha kukamilisha shule mpya ya msingi ya Ntendo B inayojengwa .
Akijibu hoja za wananchi wa kijiji cha Ntendo , Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti aliwashukuru wananchi hao kwa kujitokeza kwenye mkutano huo na kuwasilisha kero zao.
Mkirikiti aliwaeleza wanachi hao kuwa Serikali inaendelea kutafuta ufumbuzi wa soko la mahindi ambapo amewaeleza kuwa mahindi bado yanahitajika nje ya nchi hivyo endapo mfumo wa ushirika ukitumika unaweza kusaidia upatikanji soko.
“Mzizi pekee wa kufanya mahindi yapate bei ni kuacha kuuza kiholela . Ili tuuze mahindi vizuri tuna jukumu la kuimarisha vyama vya ushirika viweze kutafuta soko la uhakika la mahindi ili mkulima apate fursa ya soko. Mfumo wa kila mtu kutafuta soko la mahindi unasababisha wakulima wanyonywe” alisema Mkirikiti.
Mkuu huyo wa Mkoa amewasihi wananchi kufuata ushauri uliotolewa na Serikali endapo wanapata soko la mahindi nje ya nchi wasiwekewe vikwazo bali wasaidiwe kulifikia soko hilo.
Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Mkoa ameagiza Manispaa ya Sumbawanga kuboresha mazingira ya soko la wananchi wa Ntendo kwa kuliwekea miundombinu ikiwemo paa na vibanda ili waepukane na jua na mvua ambayo ni kero kwa sasa.
Kuhusu ujenzi wa madarasa ya shule mpya ya Ntendo B Mkuu huyo wa Mkoa wa Rukwa ameagiza Manispaa ya Sumbawanga kukamilisha ujenzi wake kabla ya mwezi Octoba mwaka huu ili kuwa na uhakika wa kupunguza msongamano kwenye shule iliyopo .
Akizungumzia mkakati wa halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga Jacob Mtalitinya alisema katika mwaka huu fedha 2021/22 wamepanga kukamilisha jumla ya vyumba 72 vya madarasa kwa kutumia fedha za mapato ya ndani ya ili kuwa na uhakika wa mapokezi ya wanafunzi wa kidato cha kwanza mwaka 2022.
Mkuu huyo wa Mkoa wa Rukwa anaendelea na ziara ya kikazi Manispaa ya Sumbawanga kuzungumza na wananchi na kukagua miradi ya maendeleo.
Mwisho
Imeandaliwa na;
Afisa Habari Mkuu,
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Rukwa
SUMBAWANGA
29.07.2021