NA BALTAZAR MASHAKA, Kahama
TAASISI ya Tanzania Mzalendo Foundation yenye Makao Makuu yake wilayani Kahama mkoani Shinyanga imempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa uamuzi wake wa busara wa kuruhusu Watanzania kupatiwa chanjo ya kuzuia maambukizi ya ugonjwa wa Covid-19.
Alisema Rais Samia Suluhu Hassan kwa kitendo cha kuruhusu chanjo hiyo anastahili kupongezwa na kila Mtanzania mwenye mapenzi mema na nchi yake, pia hatua hiyo itanusuru maisha ya Watanzania wengi watakaokubali kuchanjwa ingawa wapo wachache wanaopingana na msimamo huo wa serikali.
“Nampongeza Rais Samia kuamua na kuruhusu kuingizwa nchini chanjo ya kinga ya Corona, yeye mwenyewe kuanza kuchanjwa chanjo hiyo ameonyesha njia na ameifanya nchi yetu kuwa miongoni mwa mataifa mengine duniani yanayowajali wananchi wake,” alisema Mgeja.
Pia aliwapongeza wadau wengine walioungana na Rais wetu ikiwemo viongozi wa madhehebu ya dini kujitokeza kuchanja chanjo hiyo,kwani suala hilo linagusa hatma ya maisha yetu,na kila atakayejisikia kuchanjwa ni muhimu tayari Rais Samia ameonesha njia.
Mwenyekiti huyo wa zamani wa Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoani Shinyanga, alitoa rai kwa Watanzania wanaotoa maneno ya upotoshaji kuhusiana na chanjo hiyo ya kinga ya Covid 19 kuwa haifai na ina madhara, waache upotoshaji huo.
Alisema ni vyema watu wanaotaka kupotosha ukweli wakakaa kimya badala ya kuendelea kuwachanganya watu kwa maneno ya uongo yasiyo ya kitaalamu na kuiomba serikali iharakishe kusambaza chanjo hiyo katika mikoa yote nchini ili watu wachanjwe.
“Jambo hili ni la hiari basi, hawa wanaotaka kupotosha tuwaombe wakae kimya,ni muhimu watu waendelee kushauriwa wajitokeze kuchanjwa, na sisi huku mikoani na wilayani tunasubiri chanjo hiyo ifike haraka ili tuchanjwe,”
Mgeja alisema hao wanaopinga ni vyema sasa wakatupa mbadala wa kitaalamu tutumie njia gani katika kujikinga na ugonjwa huu, na jambo hili ni la hatari kuona watu wasiokuwa na utaalamu wala taaluma ya utabibu (daktari) ndiyo wanaosimama kidete kupinga,waoneshe kwa vigezo kwa nini chanjo hiyo haifai.
Aidha watu hao wanaoupinga msimamo wa serikali ni vizuri wakaacha mambo ya kitaalamu yasemwe na watu wenye utaalamu wa afya,na kuonya suala la kitaalamu lisiingizwe kwenye siasa na wanasiasa wafanye kazi zao za kisiasa na kufanya hivyo ni kuchezea maisha ya watu.
Mwenyekiti huyo wa Tanzania Mzalendo Foundation alionesha kushangazwa na kitendo cha wanasiasa kuingilia masuala ya kitaalamu wakipinga kwa kuukataa ukweli na kuhoji mbona wataalamu hawaingilii masuala ya kisiasa na kuonya upotoshaji wao unaweza kuliingiza Taifa kwenye matatizo makubwa.
“Nichukue fursa hii kuwapongeza viongozi wa vyombo vya ulinzi na usalama nchini,viongozi wa kidini na wale wa CCM kwa jinsi walivyoonesha msimamo kuunga mkono uamuzi wa serikali kukabiliana na janga la ugonjwa wa Covid 19,” alisema Mgeja na kuongeza;
“Niwaombe tu Watanzania hivi sasa tupo kwenye vita ya janga zito,tukifanya mzaha tunaweza kuteketeza maelfu ya wananchi kwa jambo linaloweza kuzuilika mapema kabla halijatuletea madhara makubwa, wakumbuke ule usemi wa Rais mstaafu, Jakaya Kikwete ‘akili za kuambiwa changanya na za kwako’, watauona ukweli na msimamo wa Rais Samia.”
Juzi Rais Samia Suluhu Hassan alizindua rasmi chanjo ya kujikinga na ugonjwa wa Covid 19 akisema ingawa wapo baadhi ya Watanzania wanaopinga chanjo hiyo lakini wengi wao wanaunga mkono na kwamba serikali itahakikisha wanaotaka kuchanjwa wote wanachanjwa.