Mbunge wa Jimbo la Mlimba Mkoani Morogoro, Godwin Kunambi kufanikisha ujenzi wa daraja la Mto Mngeta ambao kwa muda mrefu umekua ukihatarisha maisha ya wananchi wa Kata ya Mngeta na vitongoji vyake.
Februari mwaka huu ikiwa ni miezi mitatu tokea aanze kazi ya kuwatumikia wananchi wa Mlimba, Kunambi alifanya ziara katika Jimbo na hasa katika kata ya Mngeta ambapo alibaini changamoto ya kivuko kwenye Mto huo kwa wananchi wake.
Wananchi wa Kata ya Mngeta kwa muda mrefu wamekua wakipata changamoto ya kivuko katika Mto huo wenye Mamba ambapo mara kadhaa wamesababisha Vifo vya wananchi waliokua wakivuka Mto huo kwenda upande wa pili kufanya shughuli zao za kila siku.
“Fabruari mwaka huu nilikuja hapa kujionea changamoto hii ya kivuko na nikawaahidi kwamba hakuna Mwananchi mwingine ambaye ataliwa na Mamba Mimi nikiwa Mbunge wenu, Imani mliyonipa mimi na Rais wetu Samia Suluhu Hassan ndio ambayo imelipa leo ambapo Sasa tumekamilisha ujenzi wa daraja hili la muda lililogharimu kiasi cha Sh Milioni 31.
Lengo langu kama Mbunge wenu ni kuhakikisha tunapata daraja la kudumu ili kuondoa kero hii lakini kwa hatua hii ya kuweka kivuko cha muda ninaimani kuwa kutachochea maendeleo ya wananchi wetu na kuongeza usalama kwa watumiaji wanaopita hapa,” Amesema Kunambi.
Akizungumzia sekta ya Afya, Kunambi amesema ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ambayo umeanza kutekelezeka katika kipindi chake unatarajia kukamilika ndani ya mwaka huu huku akimshukuru Rais Samia kwa kulipatia Jimbo hilo watumishi wa kada hiyo takribani 37.
Amesema ujenzi wa Hospitali hiyo upo katika hatua za mwisho kukamilika ambapo utasaidia kuondoa changamoto ya wananchi waliokua wakitembea umbali wa kilomita zaidi ya 70 kwenda katika Hospitali ya Mt Francis iliyopo Ifakara kufuata huduma za afya.
“Tuna kila sababu ya kumshukuru Rais Samia kwa kutupatia kiasi cha Sh Bilioni 1.5 kwa ajili ya ujenzi huu, kwa muda mrefu tumekua tukiteseka kutembea umbali mrefu kufuata huduma za afya Ifakara lakini sasa ndani ya mwaka huu tunakwenda kuwa na Hospitali yetu wenyewe na tayari Rais ametupatia watumishi wa kutosha.
Niwahakikishie Ndugu zangu kwamba tumeanza na Hospitali kubwa ya Wilaya lakini kiu yangu ni kuona kila Kata inakua na Kituo Cha Afya kila kijiji kinakua na Zahanati, lengo ni kuona dhamira ya Rais wetu kuwatumikia watanzania na wananchi wa Mlimba inatimia,” Amesema Kunambi.
Katika ziara hiyo Mbunge Kunambi amekagua pia ujenzi wa Darasa na Choo katika Shule ya Msingi Ngai ambapo pia aliitembelea Februari mwaka huu na kubaini kukosa matundu ya vyoo na upungufu wa darasa kwa wanafunzi wa darasa la Sita waliokua wakisoma kwenye darasa la wazi.
“Katika ziara yangu pia ya Februari nilifika hapa Ngai na kuona wanafunzi wa darasa la Sita wakisoma katika chumba cha wazi, nielekeze na kuhamasisha ujenzi wa Darasa lao na leo tunaona linakaribia kukamilika, ni Imani yangu kabla ya mwaka huu kumalizika tutakua tumekamilisha ujenzi wa Darasa hili,” Amesema Kunambi.
Mbunge Kunambi pia ametembelea Sekondari ya Nakaguru iliyopo Kata ya Mchombe ambayo aliiwezesha kumaliza changamoto ya maji iliyokua ikiwakabili lakini pia akiwaahidi kuwapatia Runinga kwa wanafunzi wa bweni ili waweze kufuatilia vipindi mbalimbali vya habari kwa lengo la kujifunza.
Aidha Kunambi pia ametembelea Shule ya Msingi Nakaguru ambayo pia kwa kushirikiana na Serikali amefanikisha ujenzi wa madarasa mawili yaliyogharimu kiasi cha Sh Milioni 25.