Meya wa Manispaa ya Mpanda Haidary Sumri akiendesha kikao cha Baraza la Madiwani
Baadhi ya Madiwani wakifuatilia kikao
******************************
Na Zillipa Joseph, Katavi
Baraza la Madiwani wa HALMASHAURI ya Manispaa ya Mpanda mkoani Katavi wameazimia kuwaondoa mara moja wafanyabiashara wa mitumba wanaofanya biashara hizo katika maeneo mbalimbali ambayo si rasmi kwa biashara hiyo
Wakipitisha azimio hilo katika kikao cha nne cha kufunga mwaka 2020/21 Madiwani hao wamesema wafanyabiashara hao walishaonyeshwa eneo jingine la kufanyia biashara hiyo tangu mwaka uliopita lakini kwa miezi miwili iliyopita wameanza kurejea katika maeneo yao ya zamani huku wengine wakiibukia kwenye miti iliyo kando kando ya barabara na kuning’iniza biashara zao
Meya wa Manispaa ya Mpanda Haidary Sumri amesema wafanyabiashara wa mitumba walipangiwa kufanya biashara hiyo kilipokuwa kituo cha mabasi cha zamani
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Manispaa ya Mpanda Michael Nzyungu ametoa siku moja tu kwa wafanyabiashara hao kurejea katika eneo walilotengewa
‘Kesho nitapitisha gari ya matangazo na baada ya hapo tutapita kuwatoa kwa mara nyingine’ alisema
Awali Madiwani waliibua hoja hiyo ya wafanyabiashara wa mitumba kuvamia katika maeneo mbalimbali ya Manispaa na kusema kuwa hali hiyo haiupendezeshi mji.
‘Ni Mji gani ambao wananchi wake wanataka kujiongoza Kama hakuna viongozi? Walishaondolewa lakini sasa wamerudi kwa kasi’ alisema Joseph Kang’ombe Diwani wa Kata ya Ilembo