…………………………………………………………
Na Lucas Raphael Tabora
KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida wananchi wenye hasira wamemgeuza kitoweo fisi aliyeingia ndani ya nyumba na kunyakua mtoto Mazoya Nghanya (1) na kukimbia naye porini na kusababishia kifo chake huku akijeruhi watu 3 waliokuja kumwokoa.
Wakizungumzia tukio hilo lililotokea Julai 25 mwaka huu majira ya saa 9 usiku katika kijiji cha Kangeme kata ya Zungimlole wilaya ya Kaliua Mkoani Tabora, baadhi ya wakazi wa kata hiyo wameeleza kuwa baada ya fisi huyo kuuawa na Askari wa Maliasili kwa kushirikiana na Askari Polisi kwa hasira wameamua kula nyama yake ili kupoza machungu.
Mkazi wa kata hiyo Joshua Msandeke (45) alisema ni kweli fisi huyo mla watu na yeye ameliwa na wananchi wenye hasira ili kupoza machungu ya kupoteza mtoto wao na kujeruhiwa ndugu zao.
Alibainisha kuwa wamechukua hatua hiyo baada ya kukasirishwa na kitendo cha mnyama huyo kuua mtoto wao, kuwasumbua na kujeruhi wenzao 3 waliokuwa wakiokoa mtoto.
Hamisi Kenyela mkazi wa Kangeme alieleza kuwa wanakijiji wana uchungu sana ndio maana wameamua kugawana nyama yake na kuila, na kuongeza kuwa fisi wamekuwa wakisumbua sana wakazi wa kijiji hicho kilicho karibu na hifadhi.
Mbunge wa Jimbo la Kaliua Aloyce Kwezi alibainisha kuwa kama wananchi wana hasira huwezi kuwazuia kula nyama yake, wamejipatia kitoweo kizuri.
‘Nimesikia kuwa baada ya fisi huyo kuuawa na askari wa Maliasili, wananchi wameamua kumfanya kitoweo kwa kugawana nyama yake’, alisema.
Awali Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoani hapa Kamishna Msaidizi Safia Jongo alisema kuwa tukio hilo lilitokea katika hifadhi ya Luganzo -Tongwe Kijiji cha Kangeme kata ya Zugimlole.
Aliongeza kuwa licha ya askari kupambana na kufanikiwa kumuua lakini walipoteza risasi zipatazo 49 kwa kumpiga tu hadi walipofanikiwa kumuua.
Alitaja waliojeruhiwa na mnyama huyo kuwa ni baba wa mtoto aliyeuawa Nganya Mayala (45) ambaye aling’atwa kwenye kiganja cha mkono wa kulia, Ngezi Lega (25) aliyeng’atwa mkono wa kushoto na paja na Tule Malongo (45) aliyevunjwa taya na kung’atwa mkono wa kushoto hadi sasa amelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tabora-Kitete.