Mbunge Viti Maalum kupitia Chama cha Mapinduzi (NGOs Tanzania Bara) Mhe. Neema Lugangira amewasilisha mchango wa Taulo za Kike kwa wanafunzi 42 mwaka mzima, katika Ofisi za EATV, Mikocheni ikiwa ni kuunga mkono kampeni ya Namthamini.
Akizungumza baada ya kukabidhi mchango huo amesema kuwa kampeni ya Namthamini isiishie tu kwa wanafunzi mashuleni lakini pia ifike katika Magereza ili kusaidia pia wafungwa na mahabusu wakike ambao taulo pia ni changamoto kwao.
“Nimeguswa na kampeni ya Namthamini na nimekuwa nikifanya hivyo kupitia Taasisi yangu pia kuhakikisha tunasaidia Watoto wa kike kubaki Shule hasa madarasa yale ya mitihani ili Watoto hawa wasipoteze ndoto zao”, amesema Mh. Lugangira.
Mheshimiwa Lugangira ambaye pia ni Mkurugenzi Agri Thamani amesema kuwa katika kuhakikisha pia tunathamini Viwanda vya ndani, taulo za kike pia zinatakiwa kupewa nguvu katika uzalishaji wake kwa wafanyabiashara wa ndani.
“Nimeleta taulo hizi ambazo zinatengenezwa na kiwanda cha ndani ili kusisitiza Uzalendo kwanza kwa vitendo, tuthamini vya ndani, hii imekuwa ni moja ya hoja zangu hata ninapokuwa Bungeni”, amesema Lugangira.