………………………………………………………………..
Na Mathew Kwembe, Arusha
Naibu Waziri Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Pauline Gekul kesho anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye mchezo wa mwisho utakaoamua bingwa wa Netiboli nchini mwaka huu kati ya TAMISEMI QUEENS na Bingwa Mtetezi timu ya Mbweni JKT ya Dar es salaam.
Mwenyekiti wa timu ya taifa ya Netiboli Ray Mohamed amesema Mhe. Gekul ataushuhudia mchezo huo mkali na wa kusisimua utakaochezwa kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid Arusha.
Mchezo huo unatarajiwa kuvuta hisia za mashabiki wengi wa Jiji la Arusha ambao tangu kuanza kwa michuano hii wamekuwa wakijitokeza kwa wingi kushuhudia michezo mbalimbali ya ligi hiyo.
Ray amesema jumla ya timu 9 za wanawake na 4 za wanaume zinashiriki mashindano hayo ambayo hufanyika kila mwaka ambapo michuano ya mwaka huu ilianza tarehe 19 julai na itamalizika rasmi hapo kesho kwa mchezo huo wa mwisho ambao unachukuliwa kama fainali ya ligi hiyo.
Mbali na mchezo wa kesho kutoa bingwa ambaye atapata zawadi ya kikombe, washindi watatu wa nafasi za juu wataiwakilisha nchi katika mashindano ya netiboli kwa nchi za Afrika mashariki, na timu sita za juu zitashiriki kwenye ligi ya netiboli ya muungano ambayo imepangwa kufanyika mjini Zanzibar baadaye mwaka huu.
Timu zote mbili za Mbweni JKT zilifanikiwa kushinda michezo yao iliyopita ambapo Mbweni JKT hadi sasa inaongoza baada ya kushinda michezo yake 6 na kujikusanyia pointi 12 huku TAMISEMI QUEENS timu pekee ya Wizara inayo shiriki mashindano haya ina pointi 10 baada ya kushinda michezo yake 5.
Katika michezo inayochezwa leo, Arusha Jiji walitarajiwa kucheza na JKT Mgulani, huku TAMISEMI QUEENS ilikuwa inapimana ubavu na Eagles Queens ya Dar es salaam na mchezo wa mwisho utakuwa kati ya Polisi Arusha na Uhamiaji ya Dar es salaam.
Naye, Mwenyekiti wa Klabu ya Michezo ya TAMISEMI Philbert Rwakilomba amesema timu yake imekuja hapa Arusha kupambana ili ibebe kombe la ligi daraja la kwanza mwaka huu.
Amesema timu yake ilijiandaa vizuri kushiriki mashindano hayo na akawapongeza Viongozi wa Ofisi ya Rais TAMISEMI kwa kuiwezesha timu yake kufanya maandalizi mazuri na hatimaye kushiriki mashindano hayo.
Rwakilomba pia amewapongeza waandaji wa mashindano hayo Halmashauri ya Jiji la Arusha kwa mapokezi mazuri ambayo timu yake imeyapata na pia amekipongeza Chama cha mchezo wa Netiboli Tanzania CHANETA kwa kusimamia kanuni na taratibu za mashindano hayo.