Rufaa hiyo namba 2/2020 iliyofunguliwa na IPC ikipinga uamuzi wa Mahakama Kuu Mwanza,kurejesha mali zilizokuwa zikidaiwa (shule ya Sekondari Nyasaka Islamic,Thaqibu English Medium na kiwanja kimoja) kuwa ni mali ya TIC na hivyo kuipa ushindi katika kesi ya madai namba 23/2015 dhidi ya IPC.
Kesi hiyo ya madai ilitolewa uamuzi huo Julai 2018 na Jaji Bukuku wa Mahakama Kuu Mwanza,baada ya kusikiliza ushahidi wa pande zote uliotolewa mahakamani hapo ambapo ushahidi wa upande wa madai ulithibitisha madai yao bila kuacha ambapo TIC iliwakilishwa na Wakili Twaha Tasilima na IPC ikiwailishwa na Wakili,Kioba.
Jana Mahakama ya Rufaa Mwanza ilitupilia mbali rufaa ya IPC baada ya kuridhishwa na ushahidi kuwa mali hizo tatu (shule mbili ya msingi na sekondari pamoja na kiwanja kimoja) ni mali ya TIC, na kuamuru majina ya umiliki wa mali hizo ubadilishwe na kusomeka kwa jina la Thaqibu Islamic Centre badala ya IPC.
Rufaa hiyo namba 2/2020 iliyofunguliwa na IPC ilisikilizwa na majaji watatu,Jaji Ndika,Jaji Fikirini na Jaji Kihwelo,walikubaliana na hukumu iliyotolewa Jaji Bukuku kuwa ilikuwa sahihi,hivyo wakaitupa rufaa hiyo kwa gharama na kuamuru umiliki ubadilishwe kutoka IPC kwenda TIC.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti baada ya hukumu hiyo kusomwa jana kwa njia ya mtandao (Online) kwa dakika 30 na Msajili wa Mahakama ya Rufaa,Jaji Kihwelo, Mwenyekiti wa TIC, Mshumba Khalfan Almas, Makamu Mwenyekiti wa Bodi Mussa Omary,Muumini wa Msikiti wa Thaqibu,Alhaji Nurdin Mbaji, baadhi ya waislamu Sherally Hussein na Kuluthumu Juma, walisema mahakama hiyo ya rufaa imetenda haki.
Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya TIC, Omary alisema Watanzania na Waislamu nchini,wawe na imani na mahakama kwa kuwa zinatenda haki na kuishukuru Mahakama ya Rufaa kwa kuwapatia haki yao ya umiliki wa mali zao waziendeshe.
“Waislamu walikuwa wamekata tamaa, baada ya shule hizo kurejeshwa mikononi mwao niwatie moyo,tutazifuatilia na kuzisimamia kwa karibu zirejeee kwenye ubora wa kitaaluma maana zilijengwa ziwahudumie wailslamu kielimu badala yake ziligeuka kuwa mifumo ya kuendesha maisha ya watu wachache na kupandia ndege,” alisema.
Alhaji Mbaji alisema migogoro ya kidini kuhusu umiliki wa mali iko pande zote,na kutokana na madhira yanayowakumbuka waislamu,hukumu hiyo itaibua mambo makubwa ya kuwarejeshea mali zao ambazo watu wachache wamejimilikisha wakijiona ndio wenye mali na wenye mali hawana chao.
“Hukumu hii itafungua milango kwa taasisi zinazokali shule za waislamu na mifano ipo mingi,tumevumilia miaka mingi,Mungu anafahamu jiwe la kwanza tuliloweka kwenye shule hizo,na vita hii ni madhira waliyofanyiwa waislamu wengi nchini kwa maslahi ya vikundi ya watu wachache (wajumbe 10 wa bodi),”alisema.
Alhaji Mbaji alisema wenzao IPC wamwogope Mungu kwa kuwa haki ndivyo ilivyo na wasiendelee kufanya hiana, na kuwataka waislamu wa Msikiti wa Thaqibu kuwa watulivu na amani, wasithubutu kuvamia shule hizo hadi mahakama itakapotoa decree “tulianza na Mungu tutamalimaza na Mungu.”
Aidha Sherally alisema ushindi huo utaibua matatizo mengi yaliyojificha kwenye miamvuli ya taasisi za dini, watu wamejimilikisha mali zilizojengwa na kuanzishwa na waislamu,ambapo leo watu 10 waliodhaminiwa na waislamu wamezigeuza na kuzifanya mali zao wakati si zao.
Mahakama imetenda haki,ni uthibitisho mtu atapata haki yake na ushindi huu utaibua mengi, watu 10 (wajumbe wa bodi) si wamiliki na hawawezi kumiliki mali isiyo yao, mfano shule moja (anaitaja Thaqaafa) imejengwa na waislamu.”
“Mimi ni mmoja wa waanzilishi wa kituo hiki cha TIC, kilijengwa na walikusanyika waislamu hapa kujenga shule ya Nyasaka Islamic kwa nguvu na sadaka zao wakiwemo matajiri,TIC hawakuwa na usajili hivyo waliwaliwatumia IPC waendeshe shule kwa maendeleo ya waislamu baadaye ulizuka mgogoro wa umiliki wakidai shule ni mali zao,kama walitoa sadaka walitoa sawa na waislamu wengine, si wapewe umiliki,”alisema Sherally.
Naye mmoja waumini wanawake wa Msikiti wa Thaqibu, Kuluthumu Juma, alisema wanamshukuru Mungu kwa yaliyotokea, ni faraja kwani walichokisubiri wamekipata sababu mgogoro huo uliathiri jamii ya waislamu na wasio waislamu,vijana waliathirika kitaaluma na mfumo wa elimu ulivurugika kwa shule za Nyasaka Islamic na Thaqibu English Medium.
“Mahakama ni chombo huru,kimetenda haki kwa wanyonge na jamii ambapo awali ilitoa hukumu upande wa pili wakakata rufaa ambayo pia imetupwa,”alisema
Aidha Mwenyekiti wa TIC Mshumba Khamis Almasi alisema , “Safari ilikuwa ndefu na tumesafiri na kufikia hapa kwa uwezo wa Mola baada ya kutufikisha katika mawimbi mazito na mabonde, hatimaye mgororo huo wa umiliki wa mali tulizofanyiwa ufisadi tangu 2013 leo imekuwa historia,Mungu katurejeshea ushindi na mali zimerudishwa mikononi mwa waislamu wa Mkoa wa Mwanza.” Mshumba.