Sehemu ya Watendaji wa Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Kilimo wakifuatilia mkutano wa Waziri wa Kilimo
Mhe Prof. Adolf Mkenda Ofisini kwake Jijini Dodoma leo tarehe
28 Julai 2021 wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu muarobaini wa
kadhia ya kupanda bei ya mbolea.
Waziri wa Kilimo
Mhe Prof. Adolf Mkenda akisisitiza jambo Ofisini kwake Jijini Dodoma leo tarehe
28 Julai 2021 wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu muarobaini wa
kadhia ya kupanda bei ya mbolea. Wengine pichani ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara
ya Kilimo Prof Siza Tumbo (Kushoto) na Meneja wa Kampuni ya OCP Tanzania Dkt
Mshindo Msolla (Kulia)
Na
Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Dodoma
Serikali imetangaza unafuu kwa
wakulima kwa mbolea za kupandia aina ya NPS na NPS Zink ambazo zitauzwa kwa
kiwango cha kati ya Shilingi 60,000 na 65,000 Mtawalia Jijini Dar es salaam.
Mbolea hizo ni mbadala wa
mbolea za kupandia aina ya DAP ambayo imekuwa na bei kubwa kutokana na kupanda
kwa bei ya mbolea hiyo kwenye soko la Dunia.
Waziri wa Kilimo Mhe Prof.
Adolf Mkenda ametoa ufafanuzi huo Ofisini kwake Jijini Dodoma leo tarehe 28 Julai
2021 wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu muarobaini wa kadhia ya
kupanda bei ya mbolea
Waziri Mkenda amesema kuwa
mbolea hizo za kupandia aina ya NPS na NPS Zink ambazo ni mbadala wa mbolea
aina ya DAP zimefanyiwa utafiti wa kitaalamu na kuonyesha matokeo mazuri Zaidi ya
mbolea ya DAP kwa sababu zenyewe zimeongezwa virutubisho vya ziada ambavyo ni
Salfa na Zink.
Waziri Mkenda amesema kuwa
mbolea hizo zipo katika maeneo mbalimbali nchini na hivyo wananchi waendelee
kuzitumia bila kuwa na wasiwasi wowote.
Waziri Mkenda amesema kuwa
gharama hizo rafiki kwa mbolea zinazozalishwa na kampuni ya mbolea ya OCP ni matokeo
ya ziara ya kikazi aliyofanya nchini Morocco ambapo alitembelea kiwanda hicho.
Kuhusu mfumo wa uagizaji wa
mbolea kwa pamoja (BPS), Waziri Mkenda amesema kuwa serikali iliamua kuufuta
mfumo huo kwani haukuonyesha matokeo makubwa kama yalivyokuwa matarajio ya
serikali.
“Tumeamua kuruhusu
wafanyabiashara kuagiza bila mfumo wa uagizaji wa mbolea kwa pamoja-BPS ambayo hata
hivyo haitakuwa na kibali mpaka pale Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea nchini
(TFRA) itakapotoa kibali baada ya ukaguzi kukamilika” Amekaririwa Mhe Mkenda
Kadhalika, Waziri Mkenda amesema
kuwa serikali inaendelea kufanya mazungumzo na makampuni mengine ya mbolea ili
kuona uwezekano wa kupunguza bei za mbolea ambazo zimekuwa kikwazo kwa
wakulima.
Kwa upande wake Meneja wa
Kampuni ya Mbolea ya OCP nchini Tanzania Dkt Mshindo Msolla amesema kuwa mbolea
aina ya NPS na NPS Zink inauzwa kwa bei
nafuu kuliko mbolea zingine hivyo ametoa mwito kwa wakulima kujitokeza kwa
wingi ili kuinunua jambo litakalowarahisishia upatikanaji wa mbolea.
Amewaomba wakulima ambao
wameshatumia mbolea hiyo katika mikoa yote nchini kutoa elimu kwa wakulima
wengine ili kuona umuhimu wa mbolea ambayo bei yake ni nafuu na itarahisisha
gharama za wakulima ambazo ni kubwa kwenye mbolea zingine.
Kwa upande wake Dkt Catherine
Senkoro ambaye ni Mkurugenzi wa Kituo cha Utafiti wa Kilimo (TARI MLINGANO)
Kilichopo mkoani Tanga amesema kuwa mbolea hizo zina virutubisho vya ziada
ukilinganisha na mbolea zingine ambazo zinauzwa kwa gharama kubwa ambazo
wakulima wameshindwa kuzihimili.
Amesema kuwa baadhi ya
wakulima waliwahi kutumia mbolea hiyo tayari wameyaona matokeo mazuri katika
mazao yao hivyo wanapaswa kuziamini mbola za NPS na NPS Zink kwani Taasisi ya
utafiti wa kilimo-TARI imefanya utafiti katika kanda ya nyanda za juu kusini, Kanda
ya mashariki, Kaskazini, Magharibi na kanda ya kati katika ikolojia zote saba
za kilimo na kuyaona matokeo mazuri ya mbolea hizo.