Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Manyara, Holle Joseph Makungu akizungumza na waandishi wa habari Mjini Babati.
***************************
Na Mwandishi wetu, Babati
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Manyara,
imetoa elimu kwa umma kwa makundi tofauti ili kuelimisha jamii katika
mapambano dhidi ya rushwa.
Mkuu wa TAKUKURU Mkoani Manyara, Holle Joseph Makungu akizungumza na
waandishi wa habari mjini Babati juu ya shughuli zilizofanyika kipindi
cha miezi mitatu ya Aprili hadi Juni mwaka huu, amesema makundi
mbalimbali yamepatiwa elimu ya kupambana na rushwa.
Makungu amesema jumla ya mikutano 23 imefanyika ikiwa na madhumuni ya
kuelezea wananchi kuhusu athari za rushwa na jinsi ya kushiriki katika
kupambana nayo.
Amesema katika kutoa elimu ya mapambano ya rushwa, semina saba
ziliendeshwa kwa makundi tofauti ikiwemo tatu walizoshirikiana na
shirika lisilo la kiserikali la Sikika.
Amesema katika kipindi hicho cha miezi mitatu, uendeshaji mashtaka na
uchunguzi, kesi nane zilitolewa hukumu ambapo kati ya hizo Jamhuri
ilishinda kesi sita na mbili watuhumiwa waliachiwa huru.
“Jumla ya kesi mpya nane zimefunguliwa Mahakamani na hadi hivi sasa
kesi 40 zinaendelea katika mahakama za mkoa wa Manyara,” amesema
Makungu.
Amesema mikakati ya TAKUKURU katika kipindi cha Julai hadi Septemba
2021, ni kuendeleza na kutekeleza majukumu yao ambapo kipaumbele
kitawekwa kwenye uchunguzi wa ujenzi wa nyumba ya mkuu wa wilaya ya
Kiteto ambapo mwenge wa uhuru-2021 ulibaini mapungufu kadhaa.
“Tutajielekeza pia katika uchunguzi wa fedha wanazochangishwa wananchi
hapa mkoani kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ambazo
zinalalamikiwa kutotumika kwa matumizi yaliyokusudiwa,” amesema
Makungu.
Amesema wataendelea kufuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo
ndani ya mkoa na kudhibiti fedha katika ukusanyaji wa mapato ndani ya
halmashauri zote za mkoa wa Manyara.