Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-TAMISEMI Gerald Mweli alipokuwa akiongea na Watendaji wa Bodi ya Mikopo ya Halmashauri katika Ofisi za Bodi hiyo.
Kaimu Mtendaji wa Bodi Bw. Titto Mahinya akisoma taarifa ya utendaji wa Bido hiyo mbele ya Naibu Katibu Mkuu wakati wa Ziara ya Kiongozi huyo.
*************************
Na Atley Kuni-DODOMA
Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, anayeshughulikia Elimu, Gerald Mweli, ameitaka Bodi ya Mikopo ya Halmashauri kufanya tathmini ya kina kabla ya kutoa Mikopo kwa Halmashauri hizo ili kufikia tija iliyokusudiwa.
Mweli ametoa kauli hiyo Julai 26, 2021 alipofanya ziara katika Ofisi za taasisi hiyo iliyo chini ya Ofisi ya Rais – TAMISEMI kisha kufanya mazungumzo na uongozi na watumishi wa Taasisi hiyo, ambapo aliwasisitiza watendaji katika Bodi kubadili mtazamo wa kiutendaji na kuja na mawazo mbadala katika kuendesha Bodi hiyo.
“Pamoja na mimi kuja kujua changamoto zinazowakabili, lakini mnachotakiwa sasa mbadilike na mfanye kazi kwa matokeo, wakati wa Uchambuzi wa bajeti (scrutinization), tutumie fursa hiyo kuzipima Halmashauri zile zinazo weza kufanya marejesho na zile ambazo zinasuasua katika marejesho, alisema Mweli na kuongeza kuwa, lazima Bodi iwe na ajenda, Je! Fedha zinazokopeshwa kwa Halmashauri, mradi husika utaweza kurejesha fedha husika? Alisisitiza kwa kuhoji Mweli.
Mweli ameitaka Bodi kubadili mfumo wa kudai madeni, na kuwataka kufanyia kazi yale yaliyo upande wao kama Bodi na yanayohitaji maamuzi ya Wizara, yafikishwe Wizarani kwa hatua muhimu.
Awali akisoma taarifa ya Utendaji kazi, Kaimu Mtendaji Mkuu wa Bodi hiyo, Yeremiah Titto Mahinya, alimwambia Naibu Katibu Mkuu kuwa, dhumuni la Bodi hiyo nikuziwezesha Mamlaka za Serikali za Mitaa, kufanikisha miradi ya maendeleo itakayowasadia katika kuinua mapato na kuchochea shughuli za kiuchumi.
Bodi ya Mikopo ya Serikali za Mitaa iliundwa chini ya Sheria ya Fedha ya Serikali za Mitaa, Sura ya 290 RE 2002, chini ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa aidha Bodi inaendesha shughuli zake kwa mujibu wa Sheria iliyounda Bodi husika.