Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Manyara, Holle Joseph Makungu akizungumza na
waandishi wa habari ofisini kwake mjini Babati.
***************************
Na Gift Thadey, Babati
TAASISI ya Kuzuia na Kupamba na Rushwa (TAKUKURU) Mkoani Manyara, kwa
kipindi cha miezi mitatu ya Aprili hadi Juni mwaka huu, imekagua
utekelezaji wa miezi 15 ya maendeleo ya thamani ya shilingi bilioni
2.27.
Mkuu wa TAKUKURU Mkoani Manyara, Holle Joseph Makungu ameyasema hayo
Mjini Babati ofisini kwake wakati akizungumza na waandishi wa habari
juu ya utekelezaji kazi kwa kipindi cha miezi mitatu.
Makungu amesema lengo la kukagua miradi hiyo kwenye mkoa huo wa
Manyara ni kujiridhisha na ubora ikilinganisha na thamani ya fedha
iliyotumika.
Ametaja miradi iliyofanyiwa ufuatiliaji ni ujenzi wa uzio wa Ikulu
ndogo ya Hanang’ wenye thamani ya shilingi 250,000,000 na ujenzi wa
miundombinu ya shule mpya ya sekondari Lalaji wa thamani ya shilingi
700,000,000.
Ametaja miradi mingine ni ujenzi wa miundombinu ya kituo cha afya
Mogitu ya thamani ya shilingi 400,000,000 uliokataliwa kufunguliwa na
Mwenge na kuagiza TAKUKURU Mkoa wa Manyara ichunguze.
“Uchunguzi wa TAKUKURU umeonyesha hakuna ufujaji wa fedha uliofanyika
na tumejiridhisha kuwa umejengwa kwa ubora na una akisi thamani ya
fedha iliyotumika,” amesema Makungu.
Amesema changamoto iliyojitokeza ilitokana na mapungufu katika
uandaaji wa taarifa iliyosomwa kwa kiongozi wa mbio za mwenge Luteni
Josephine Mwampashi.
Amesema uchunguzi umebaini muadnaaji wa taarifa hiyo hakuwa na taaluma
stahiki ya usimamizi wa fedha hivyo alichanganya fedha za mradi huo na
fedha za miradi miwili ya kijiji.
Ametaja mradi mwingine ni ujenzi wa choo na miundombinu ya zahanati ya
Dawar wa shilingi 22,000,000 na ofisi ya udhibiti ubora shule wa
halmashauri ya mji wa Mbulu shilingi 42,270,315.
“Mradi mwingine ni ujenzi wa bweni na nyumba ya walimu Maretadu wa
thamani ya shilingi 175,000,000 na ofisi ya udhibiti ubora shule wa
halmashauri ya wilaya ya Mbulu shilingi 181,818,181,” amesema Makungu.
Amesema mradi mwingine ni ujenzi wa zahanati ya Njia panda ya shilingi
139,000,000 matundu 10 na madarasa manne shule ya Kaloleni shilingi
47,700,000 na choo cha zahanati ya kijiji cha Njoro wa shilingi
19,000,000 maabara Kibaya shilingi 30,000,000 na madarasa saba na
choo shule ya msingi Endahagichan shilingi 47,700,000.
Ametaja mradi mwingine ni na ujenzi wa madarasa mawili na matundu nane
ya vyoo shule ya msingi Kiru Six wenye thamani ya shilingi 48,880,000
ujenzi wa wodi ya wazazi ya hospitali ya Mrara shilingi 400,000,000 na
mradi wa mitaro ya barabara ya Kibaya ya thamani ya shilingi
278,268,970.