Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Selemani Jafo akitoa maelekezo kwa Kaimu Meneja wa kiwanda cha sabuni cha Royal Soap (hayupo pichani) aitishe kikao na Wananchi wanaodai fidia kutokana na uchafuzi wa mazingira uliofanywa na kiwanda hicho Jijini Dar es Salaam.
Mkuu wa Wilaya ya Ubungo Mhe. Herry James akiwasisitiza wamiliki wa kiwanda cha Nida Textile Mills kukamilisha taratibu zilizotolewa na Mamlaka ya Bonde ili wapate cheti cha kuruhusu maji yanayotibiwa kutoka kiwandani yaingie kwenye mazingira.
Bw. Imran Lohya Meneja Mkuu wa kiwanda cha nguo cha Nida Textiles Mills akitoa maelezo namna wanavyotibu maji machafu kabla hajatiririshwa kuingia kwenye Mto Ng’ombe wakati wa ziara ya Waziri Jafo kiwandani hapo
Maji yanayotoka kwenye kiwanda kuingia kwenye mto Ng’ombe.
……………………………………………………………………………
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais- Muungano na Mazingira Mh. Selemani Jafo ametoa siku 45 kwa Kiwanda cha kutengeneza nguo cha NIDA Textile Industries kuhakikisha kimepata kibali cha kutiririsha maji ambayo yanaingia katika Mto ulioko katika eneo hilo, kutoka katika Mamlaka ya Bonde Mto Wami- Ruvu kinachothibitisha ubora wa maji wanayotiririsha ni salama kwa Mazingira na hayana athari yoyote kwa mazingira.
Ametoa agizo hilo Mkoani Dar es Salaam alipotembelea kiwanda hiko kilichopo katika eneo la Tabata katika Manispaa ya Ubungo alipokua katika ziara yake ya siku moja na kubaini hakuna kibali cha kutiririsha maji ambacho ni muhimu kwa sababu Kiwanda hiko kina mfumo wa kutiririsha maji taka kwahiyo kinatakiwa kuwa na kibali hiko .
“Ninatoa siku 45 ikiwa na maana ya mwezi mmoja na nusu muwe mmeshapata kibali kutoka Mamlaka ya Bonde kuhusiana na maji taka mnayotiririsha kama ni salama au la mana maji haya hayaonyeshi kwa macho maji haya ni salama kwa mazingira na
viumbe hai” Waziri Jafo
Aidha Waziri Jafo alitembelea kiwanda cha kutengeneza sabuni cha Royal Soap and Detergents kilichopo Kata ya Mabibo katika Manispaa ya Ubungo kujionea changamoto za uchafuzi wa mazingira katika eneo hilo ambazo zimekua zikilalamikiwa kwa muda mrefu na Wananchi wa eneo hilo la Kata ya Mabibo ikiwemo hewa chafu inayotoka kiwandani hapo .
Akiwa Kiwandani hapo alisikiliza pande zote yani Upande wa Kiwanda na Wananchi ambapo waliwakilishwa na Diwani wa Kata hiyo Mh. Joseph Kleruu na hatimaye alitoa maagizo kuwa ameona kuna changamoto ya Kimahusiano kati ya Wananchi wa eneo hilo na mwenye Kiwanda hivyo ameagiza kifanyike kikao kati ya mwenye Kiwanda, Afisa Mazingira wa Manispaa pamoja Diwani na Mwenyekiti wa Mtaa huo ambao ni Wawakilishi wa Wananchi kwa pamoja wafikie makubaliano halafu taarifa ya Makubaliano hayo iende kwa Mkuu wa Wilaya ya Manispaa ya Ubungo .
‘Nimeona kuna changamoto ya kimahusiano katika eneo hili tafadhali wekeni mahusiano mazuri na Wananchi wanaowazunguka hiyo ni muhimu sana naagiza mfanye kikao ndani ya wiki mbili kupata ufumbuzi wa suala hili na ndani ya miezi sita tutakuja tena kujionea katika suala la mazingira utekelezaji wa makubaliano hayo umefanyika au la ” Waziri Jafo
Akiongea baada ya kupokea maagizo hayo Mkuu wa Wilaya Manispaa ya Ubungo Mh. Kheri James alimuhahikishia Waziri Jafo kupokea maagizo hayo na atayafanyia kazi na taarifa ya makubaliano itapelekwa Ofisini kwa Waziri kama alivyoagiza.
Naye Meneja wa Uendeshaji wa Kiwanda hiko Ntula Shalanda amemuahidi Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais- Muungano na Mazingira Mh. Selemani Jafo kupokea maagizo hayo na kuyafanyia kazi na watakutana na Wawakilishi hao wa Wananchi kama alivyoagiza.
Katika ziara hiyo Waziri Jafo aliambatana na Mkuu wa Wilaya wa Manispaa ya Ubungo Kheri James pamoja na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Manispaa ya Ubungo na Wataalamu wa Mazingira kutoka NEMC na Manispaa ya Ubungo.