Makamu wa Rais Dkt Philip Mpango ametembelea na kuweka jiwe la msingi katika mradi wa chujio la maji Mangamba unaogharimu shilingi bilioni 2.3, unaotarajiwa kutatua changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama mkoani Mtwara.
Makamu wa Rais Dkt Mpango amemtaka Waziri wa Maji Jumaa Aweso kusimamia na kufanya kazi usiku na mchana ili kukamilisha mradi kwa wakati ili kuondoa kero zilizopo na kuwapa wananchi maji safi na salama huku akisisitiza kutumia malighafi za ndani zinazokidhi mahitaji na zinazofikia viwango badala ya kuagiza nje ya nchi malighafi ambazo zinaweza kupatikana hapa nchini
Waziri wa Maji Jumaa Aweso amemhakikishia Makamu wa Rais kukamilisha mradi kwa wakati huku akieleza kuwa kwa sasa wizara inawajengea uwezo wataalamu wa ndani ili watumike kujenga miradi ya maji badala ya kuendelea kutegemea wataalamu kutoka nje ya nchi
Makamu wa Rais pia ameitaka Wizara ya Maji kuwa na mpango maalum wa makusudi kusomesha wataalamu wa maji ili kuhakikisha Taifa linakuwa na wataalamu wa kutosha kuhudumu katika sekta ya Maji nchini.